Ofisi ya Bunge la Katiba itamtuma ofisa wake kwenda Makka, Saudi
Arabia kusimamia upigaji kura kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa
wajumbe wa Bunge hilo wanaokwenda Hijja.
Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Bunge hilo,
Yahya Khamis Hamad alipotakiwa kueleza idadi kamili ya wajumbe wa Bunge
hilo wanaotarajiwa kuwa nje ya nchi na jinsi watakavyopiga kura.
Juzi, Bunge hilo lilizifanyia marekebisho kanuni
zake ili kuwaruhusu wajumbe watakaokuwa nje ya Ukumbi wa Bunge wakiwamo
wanaokwenda Hijja kuipigia kura Katiba inayopendekezwa, iliyokabidhiwa
kwa Kamati ya Uongozi jana.
Chini ya marekebisho hayo, mjumbe aliye nje ya
Bunge, ataruhusiwa kupiga kura ya wazi au ya siri kwa njia ya fax au
mtandao kama itakavyoelekezwa na katibu kwa kushauriana na mwenyekiti.
Hamad alisema hadi kufikia jana mchana walikuwa
wamewatambua wajumbe wanane ambao watakwenda Hijja huko Uarabuni lakini
orodha ya watakaokuwa nchi nyingine bado haijajulikana.
Hamadi alisema ofisa wake huyo atasimamia kura za
wajumbe wanaokwenda Hijja katika upigaji kura unaotarajiwa kuanza
Septemba 29 hadi Oktoba 2 mwaka huu.
Alisema ni vigumu kutaja vituo watakavyopigia kura
sasa kwa sababu bado hawajawauliza wajumbe wengine waliopo nje ya nchi
ambao wangependa kupiga kura wakiwa huko.
Kuhusu iwapo watapiga moja kwa moja kwa mtandao au
watapiga kwenye karatasi na kutoa vivuli, Hamad alisema suala hilo
litaamuliwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge chini ya Mwenyekiti, Samuel
Sitta.
Ukawa wapinga
Wenyeviti wenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia wamelishukia Bunge hilo
kwa kuruhusu upigaji kura nje ya nchi.
Akizungumza jana, Profesa Lipumba alisema
kilichofanywa na Sitta na wajumbe wake ni uchakachuaji unaoweza
kuliingiza Taifa kwenye mgogoro mkubwa.
“Kwanza taratibu za kura mabunge ya Jumuiya ya
Madola ni kura zote zinapigwa ndani ya Bunge. Unapozungumzia akidi
imetimia ni wajumbe walioko ndani ya Bunge,” alisema Profesa Lipumba.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Kanuni mpya ya 30 (1) baada ya marekebisho yaliyofanyika juzi
inasomeka, “Akidi kwa kila kikao cha Bunge Maalumu itakuwa ni nusu ya
wajumbe wote wa Bunge Maalumu.”
Awali, kanuni hiyo iliweka sharti la lazima kwamba
akidi ya kikao itakuwa ni nusu ya wajumbe, isipokuwa kwa kikao
kinachohusu kupitisha uamuzi wa Bunge Maalumu.
“Mwenyekiti hawezi tu kutangaza kuwa akidi
imetimia kwa sababu nimepata barua kuna wajumbe wako nje kwa hiyo
watapigia kura huko. Ni uvunjifu wa sheria na taratibu ulio wazi,”
alisisitiza.
“Hakuna maridhiano lakini zaidi ya hapo huu
mchakato wote umeshaharibika. Kinachofanyika hapo ni Sitta kujaribu
kuhalalisha matumizi ya Sh20 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya Bunge
hilo,” alisema.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF,
alisema kinachofanywa na Sitta ni kuhakikisha wanatoka na Katiba hata
kama haina uhalali wa kisiasa.
“Kwa hiyo inabidi lazima atoke na kitu ili aseme
tumepitisha uamuzi tumetoka na Katiba hii ili kuhalalisha matumizi,”
alisema Lipumba na kuhoji uharaka huo wa Sitta ni wa nini?
“Kama muda hautoshi kwenda kwenye kura ya maoni
kulikuwa na sababu gani ya kuendelea na mchakato huo. Mchakato wa Katiba
unakwenda katika utaratibu wa sheria,” alisema.
Profesa Lipumba alisema sheria iko wazi na iliweka
utaratibu kuwa baada ya kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, isipite
siku zaidi ya 120 bila kura ya maoni kufanyika.
“Ni wazi sheria yenyewe itabidi ibadilishwe. Rais
atakayekuja akiwa makini hawezi kukubali kuanza na Katiba iliyowagawa
Watanzania. Rais gani atakubali kuanza na migogoro ya kisiasa?” alihoji
Lipumba.
“Waziri wa Katiba wa SMZ (Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar) hashiriki, AG (Mwanasheria Mkuu) wa Zanzibar hashiriki Katiba
ya nchi, watu wa Zanzibar hawashiriki utasemaje ina uhalali wa kisiasa?”
Mbatia alisema anamshangaa Sitta kujigamba kutokana
na Katiba inayopendekezwa wakati itakwenda kukaa kabatini kusubiri
utashi wa rais ajaye.
“Hatuna kura ya maoni kwa hiyo haiwezi kutumika.
Kwa hiyo ikishapokewa inawekwa kabatini. Rais ajaye ni mwingine, sisi
tunaendelea na mikakati yetu ya marekebisho ya 15 ya Katiba,” alisema.
Kuahirishwa kwa kura ya maoni kunatokana na makubaliano kati ya viongozi wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Jakaya Kikwete yaliyofikiwa Septemba 8, mwaka huu.
MwananchiKuahirishwa kwa kura ya maoni kunatokana na makubaliano kati ya viongozi wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Jakaya Kikwete yaliyofikiwa Septemba 8, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment