Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki Kipawa, Ilala jijini Dar es Salaam, Joseph Mashaka akiongoza ibada.
PAROKO
Msaidizi wa Kanisa Katoliki Kipawa, Ilala jijini Dar es Salaam, Joseph
Mashaka amesema biashara ya madawa ya kulevya imechafua sura nzuri ya
Tanzania iliyokuwa nayo nje ya nchi hususan Uingereza, baada ya vijana
wengi kujihusisha nayo kwa kusafirisha na kutumia.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa
ibada maalum ya kumuombea marehemu Leberatus Damian Matemu (55),
aliyefariki dunia Agosti 31, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Alisema wakati akianza kujifunza kazi ya upadri katika mojawapo ya
nchi za Ulaya, Tanzania ilikuwa nchi yenye heshima kutokana na usafi wa
wananchi wake na viongozi, sifa ambayo hivi sasa imetoweka kabisa.
“Maadili tuliyokuwa nayo tangu na baada ya kupata uhuru yametoweka,
hivi sasa tumepoteza uadilifu kiasi kwamba hata hatuelewi tunafanya
nini,waumini wenzangu lazima tutambue kuwa kuna Mungu, tujiandae kwa
kila namna, kwa matendo mema ili hata siku za mwisho tuweze
kupokelewa katika uzima wa milele,” alisema padri huyo.Alisema siku
moja akiwa nje, alipoonyesha hati yake ya kusafiria na kuonyesha kuwa ni
Mtanzania, alimwagiwa sifa nyingi za kuisifu nchi yetu kitendo ambacho
kilimpa faraja kubwa, tofauti na hali inayoendelea hivi sasa.
“Lakini leo hii nchi yetu inasemwa vibaya, kitu ambacho si kizuri
hata kwa vijana imekuwa ni gumzo, ninawaomba tupendane na kushirikiana
kwa uadilifu kama zamani, tumche Mungu kwani hakuna ajuaye siku wala
saa,” alisema.
Katika ripoti ya mwaka huu, Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa
ya kulevya ilitoa takwimu ya Watanzania 403 waliokamatwa na kuhukumiwa
wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya sehemu mbalimbali duniani
na wengine wakisubiri kuhukumiwa.
GPL
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment