HATIMAYE mvutano kati ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na
Serikali umefikia kikomo baada ya pande mbili hizo kukubaliana na Rais
Jakaya Kikwete kuboresha Katiba ya mwaka 1977 na kuingia kwenye Uchaguzi
Mkuu mwakani.
Hatima hiyo ilifikiwa jana kwenye kikao kilichofanyika kati ya Rais
Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinachoundwa na vyama
vyenye wabunge ambavyo ni CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, TLP, UDP na
UPDP inayowakilisha vyama visivyo wa wabunge, kilichofanyika Ikulu ndogo
mjini Dodoma.
Mkutano wa awali wa viongozi hao ulifanyika Agosti 31, mwaka huu,
katika Ikulu ya Kilimani, mjini Dodoma ambapo walipeana majukumu ya
kufanya ili kuangalia namna bora ya kufikia mwafaka.
Katika mkutano wa jana, chanzo cha habari kutoka ndani ya mkutano huo
kilieleza kuwa viongozi hao walikubaliana kuwa kutokana na mazingira ya
sasa, ni vigumu kupata Katiba mpya ambayo itatumika mwakani.
Kutokana na hali hiyo, viongozi hao walikubaliana kuwa ni vyema vyama
hivyo vikakaa na kuangalia mambo muhimu ya kuwekwa kwenye Katiba ya
sasa.
“Vyama vinatakiwa vikae na kuangalia ni nini cha kuchukuliwa na
kuwekwa kwenye Katiba hii ya sasa, baada ya kumaliza Uchaguzi Mkuu ndiyo
sasa turudi kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya,” alisema.
Alisema kuwa baada ya vyama hivyo kukaa na kukubaliana kitu cha
kuweka kwenye Katiba inayotumika sasa, watayapeleka mapendekezo hayo
serikalini kisha muswada wa marekebisho ya Katiba utapelekwa bungeni.
Kwenye suala la kuahirishwa kwa Bunge, chanzo kingine kilisema kuwa halikuzungumziwa, lakini busara inatarajiwa kutumika zaidi.
Mwenyekiti TCD.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao
hicho, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, alisema kuwa wamekubaliana
kindugu.
Waandishi wa habari walipotaka afafanue kauli yake na kama
kukubaliana huko kunamaanisha kusitisha Bunge ama Ukawa kurudi bungeni,
Cheyo alisema: “Mimi naongea kama mwenyekiti wa vyama vyote,
tumekubaliana kindugu, mazungumzo yalienda vizuri na kesho nitatoa
taarifa kamili.”
Mwanasheria Mkuu
Agosti 16, mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema,
alizungumzia ugumu wa rais kuvunja Bunge la Katiba na kusema Katiba
mpya ikishindwa kupatikana, iliyopo sasa itafanyiwa marekebisho.
Jaji Werema alikuwa akizungumzia hatima ya upatikanaji wa Katiba mpya
na mwenendo wa vikao vya kamati za Bunge Maalumu vinavyoendelea sasa
Dodoma, ambavyo vimesusiwa na wajumbe wanaounda Ukawa.
Alisema tathmini iliyofanyika ya mwenendo wa vikao hivyo, imeonyesha
kuwa theluthi mbili inayohitajika ili kupitisha vifungu vinavyojadiliwa
inapatikana, isipokuwa wasiwasi umebaki kwenye kupitisha vifungu hivyo
wakati wa vikao vya pamoja vya wabunge wote.
Jaji Werema alisema kwa kutambua hilo, iwapo akidi ya theluthi mbili
ya wajumbe haitapatikana wakati wa kupitisha Katiba iliyopendekezwa,
baadhi ya vifungu vitakavyopitishwa vitachukuliwa na kupelekwa kwenye
Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kuingizwa kwenye Katiba ya
sasa ya mwaka 1977.
“Kwa sasa akidi kwenye kamati inatosha, tukifikia Bunge kuja na
Katiba inayopendekezwa na kama hakuna theluthi mbili, tutarudi kwenye
Bunge la kawaida (Bunge la Jamhuri ya Muungano) na kukubaliana,
yaliyokuwa hayana ubishi tutayaweka na kuyatumia kwenye Katiba ya sasa,
likiwamo suala la mgombea binafsi,” alisema Jaji Werema.
Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment