Waziri Mkuu Mizengo Pinda 
 WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Mlima Kilimanjaro unaweza kutumika vizuri zaidi kwenye vita ya kupambana na ugonjwa wa malaria kwa wanamichezo na watu mashuhuri kuupanda mlima huo na kuchangisha fedha za kusaidia kampeni ya kupambana na ugonjwa huo.


Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumamosi, Februari 9, 2013) wakati akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki mjadala kuhusu juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa malaria uliofanyika kwenye kituo cha mikutano cha Sandton, kilichopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini.


Alisema katika majadiliano yake na baadhi ya wajumbe walioshiriki mjadala huo, wengi waliunga mkono wazo alilolitoa la kutumia Mlima Kilimanjaro katika kampeni za kupambana na ugonjwa huo.


“Nimeongea na baadhi ya wajumbe katika hafla hii hapa Johannesburg, wengi wameliafiki wazo la kutumia Mlima Kilimanjaro kutangaza mapambano haya... kila mwanamichezo atakayepanda mlima huu atatangazwa kwamba ameshinda vita dhidi ya malaria na fedha atakayochangisha itatumika katika kampeni ya kupambana na malaria barani Afrika,” alisema.


Alipoulizwa ni kitu gani cha tofauti alichojifunza katika mjadala huo, Waziri Mkuu alisema jambo kubwa aliloliona ni jinsi ya kutumia mbinu mbadala za kupeleka ujumbe kuhusu mapambano dhidi ya malaria. “Kila mtu ana dhamana ya kuchangia vita dhidi ya malaria. Hawa wenzetu wameitisha viongozi wa makampuni makubwa kutoka Afrika Kusini na nje ya nchi hiyo, wako wadau mbalimbali jioni ya leo walioshiriki mjadala huu,” alisema.


Akitoa mfano wa Tanzania, Waziri Mkuu alisema tangu mwaka 2000 idadi ya wagonjwa wa malaria imekuwa ikishuka lakini vilevile idadi ya wafadhili wanaochangia jitihada za kupambana na ugonjwa huo nayo pia imekuwa ikishuka. Ndiyo maana nimesema kuna haja ya kutumia wadau wengine kama vile Bunge, NGOs na Serikali za Mitaa ili kuona wanaweza kusaidia vipi katika vita hiyo,” alisema.


“Wenzetu hawa, (akimaanisha - Muungano wa Mashirika ya Kimataifa yanayopambana dhidi ya Ugonjwa wa Malaria – United Against Malaria (UAM) wametumia mashindano ya AFCON kupeleka ujumbe wa kupambana na ugonjwa huu unaoua watu wengi Afrika sababu ni moja tu: watu wengi wanapenda mpira wa soka iwe uwanjani au kuangalia kwenye luninga kwa hiyo wanajua fika kuwa ujumbe ukitolewa pale utawafikia watu wengi sana na kwa haraka zaidi. Sisi Tanzania tulishaanza na sasa tunaangalia uwezekano wa kutumia basketball, netball na michezo mingine kufikisha ujumbe huu,” alisema.


Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wanaopambana na Malaria (TAPAMA- Tanzania Parliamentarians Against Malaria), Bi. Riziki Lulida ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe waliofuatana na Waziri Mkuu Afrika Kusini, alisema Tanzania bila Malaria inawezekana na wao kama Wabunge wanaweza kwenda vijijini kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.


Naye Dk. Hamisi Kigwangalla ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa TAPAMA alisema atatumia fursa ya kushiriki mjadala huo kama njia ya kujifunza mbinu mbadala za kuishirikisha jamii kwenye vita dhidi ya ugonjwa wa malaria. “Leo tumeona wenzetu wakiwatumia watu maarufu kama Yvonne ChakaChaka, Mark Fish – mchezaji wa zamani wa BafanaBafana na pia Drogba yuko kwenye matangazo yao kuhamasisha wananchi watumie vyandarua kujikinga na malaria… sisi pia tunaweza kutumia wasanii na wanamichezo wetu kuelimisha umma kuhusu mapambano dhidi ya malaria,” alisema.


Naye Mbunge wa Chonga, Pemba, Dk. Haroub Mohammed Shamisi ambaye pia ni mjumbe wa TAPAMA alisema ushirikishwaji mkubwa wa jamii kwenye vita dhidi ya malaria umesaidia sana kushusha viwango vya maambukizi ya malaria kule Zanzibar.


“Zanzibar imepiga kasi sana katika vita hii na sababu kubwa iliyochangia ni ushirikishwaji wa karibu wa wananchi kwenye kampeni dhidi ya malaria. Baadhi ya wabunge tuliamua kuungana ili tupeleke ujumbe huu kwa wananchi kwa urahisi ili tuweze kufanikiwa kwa haraka zaidi,” alisema.


Waziri Mkuu amerejea nchini mchana huu na kwenda moja moja Dodoma kuhudhuria vikao vya Chama cha Mapinduzi.

  
IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI 10, 2013 TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top