VIONGOZI na mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) jana walifanya maandamano na kuhitimishwa kwa mkutano wa
hadhara uliofanyika Temeke, jijini Dar es Salaam ambako chama hicho
kilitangaza nia ya kuandaa hoja ya kuwang’oa viongozi wa Bunge.
Hoja hiyo itawasilishwa katika mkutano ujao wa
Bunge kwa ajili ya kuwapigia kura za kutokuwa na imani na Spika wa
Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai kwa madai ya kukwamisha
mijadala yenye masilahi ya wananchi bungeni.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Uwanja wa Temeke Mwisho, Dar es Salaam, wabunge wa chama hicho
wakiwa na uongozi wa juu, waliwataka wananchi waliohudhuria mkutano huo
kujiandaa na maandamano ya kuwang’oa maspika hao. Kana kwamba hiyo
haitoshi, wabunge hao walitangaza namba za simu za viongozi hao wa Bunge
ili wananchi wazitumie kuwashinikiza wang’oke.
Akihutubia katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu
wa chama hicho (Bara), Zitto Kabwe alisema Spika Makinda ameshindwa
kuwajibika na hivyo anapaswa kung’olewa kutokana na kutaka kuirudisha
nchi kwenye kipindi cha kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu
(Epa).
Akizungumzia kitendo cha Spika Makinda kuifuta
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto aliyekuwa
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema imefutwa kwa mbinu za CCM kuzima sauti
ya wabunge wa upinzani wanaozungumzia masilahi ya wananchi.
Huku akishangiliwa na umati wa wananchi
waliohudhuria mkutano huo, Zitto alitaja mbinu za kumng’oa Spika Makinda
akisema kuwa hoja hiyo imeshakamilika.
“Kuna njia za kumng’oa Spika Makinda, kwanza kwa
kupeleka hoja ya kutokuwa na imani naye na nimeambiwa hapa kwamba
imeshakamilika. Au tuandamane hadi pale Shule ya Msingi Bunge… au
tutumie namba zake kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mikononi…”
alisema Zitto na kumruhusu Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema kutaja
namba za Spika Makinda na Naibu wake.
Baada ya kutaja namba hizo wananchi walionekana wakizipiga na wengine kutuma ujumbe wa simu.
Mwananchi lilipompigia simu Spika Makinda, simu yake ilikuwa inaita, kisha inakatika bila kupokewa.
Akizungumzia zaidi kuhusu kamati hiyo, Zitto alisema:
“Kamati hii iliundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Spika
Samuel Sitta kwa ushauri wa kina Dk Slaa (Willibrod, Katibu Mkuu
Chadema), waliona kuwa haiwezekani nchi yenye zaidi ya mashirika 200
yenye thamani ya zaidi ya Sh10 trilioni yasidhibitiwe na Bunge…Lakini
Serikali ya CCM ikaona upinzani umepata sehemu ya kuzungumzia, sasa
wameifuta,” alisema Zitto.
Alitaja sababu ya kufutwa kwa kamati hiyo kuwa ni
utendaji wa kamati hiyo uliogundua matumizi ya zaidi ya Sh1 trilioni
kutoka kwenye mifuko ya pensheni zilizotumika katika kampeni za CCM
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma, Hombolo na Chuo
Kikuu cha Arusha.
Chanzo: Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment