Papa Benedict XVI ajiuzulu 

PAPA Benedict XVI, ametangaza kujiuzulu wadhifa huo, baada ya kuutumikia kwa muda wa miaka minane.Papa Benedict alitangaza hatua hiyo jana kuwa anatarajia kuachia ngazi rasmi saa 2:00 Februari 28, mwaka huu akieleza kuwa hii ni kutokana na umri wake kuwa mkubwa. Hivi sasa Papa Benedict XVI ana umri wa miaka 85.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 600 iliyopita kwa kiongozi mkuu wa kanisa hilo kujiuzulu, tangu alipojiuzulu Papa Gregory XII mwaka 1415.
Papa Gregory alijiuzulu katika mpango wa kumaliza mgogoro uliokuwepo wakati huo kati ya makadinali wa Great Western kugombea kiti hicho.

Kujiuzulu kwa Papa Benedict XVI kunatoa mwanya wa kuchaguliwa kwa Papa mpya kabla ya Machi mwaka huu. Akitangaza uamuzi huo jana kiongozi huyo alisema anatambua umuhimu wa nafasi yake na uzito wa mapokeo ya uamuzi wake, lakini anachukua uamuzi huo baada ya kutathmini na kujiridhisha dhamira yake mbele ya Mungu.

“Baada ya kuitazama dhamira yangu mbele ya Mungu, nimekuwa na uhakika kwamba nguvu zangu kutokana na miaka kuwa mingi, siwezi kuwa tena kwenye hii nafasi ya kuwa kiongozi wa Wakatoliki,” alisema na kuongeza:

“Ninajua kwamba madhehebu haya kwa jinsi yalivyo na asili muhimu ya kiroho, lazima uongozi uchukuliwe si tu kwa maneno na matendo, bali pia kwa sala na mateso.”

Papa Benedict XVI aliendelea kueleza: “Katika dunia ya leo kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara na yanayotikisa na kuzua maswali ya kina kwa ajili ya maisha ya imani, kuongoza kanisa kunahitaji mtu awe na nguvu kimwili na kiakili.”
“.., nguvu ambazo kwa miezi michache iliyopita zimepungua kwangu kiasi cha kugundua kupungua kwa uwezo wangu kufanya kazi ambayo nimepewa.”

Alisema uamuzi wake huo ni muhimu kwa uhai wa Kanisa Katoliki duniani lenye waumini zaidi ya bilioni moja. Kujiuzulu kwa Papa Benedict XIV kunaweza kusiwe hatua ya kushtua kwa baadhi ya wale wenye kumbukumbu ya maneno yake ya awali mara tu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Mara tu baada ya kuchaguliwa, Papa Benedict alisema kwamba alikuwa akiomba sana asichaguliwe kushika wadhifa huo kwa kuwa alidhamiria kuzeeka kwa amani katika umri mkubwa aliokuwa nao.

Katika utumishi wake ndani ya Kaisa katoliki, Papa Benedict XVI aliweka bayana msimamo wake kuhusu kutokubaliana na suala la wanawake kushika nafasi za uongozi ndani ya Kanisa, hasa upadri na uaskofu, suala la kuruhusu utoaji mimba kwa namna yoyote na kuzalisha kwa kutumia njia mbadala za kisayansi.

Katika Upapa wake, mada kuu ambayo alikuwa akiisimamia ni utetezi wa maadili ya kimsingi ya Kikristo katika kile alichokieleza kwamba ni kusikitishwa kwake na kuporomoka kwa maadili ndani ya kanisa, katika mataifa mengi ya Ulaya.

Papa Benedict XVI, alilitumikia kanisa hilo wakati likiwa katika dhoruba kali kwa miongo kadhaa, likikabiliwa na kashfa ya unyanyasaji wa watoto, ambapo alianza kukata mzizi wa kadhia hiyo.

Maaskofu nchini washtushwa
Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini, wamepigwa butwaa kwa hatua ya Papa Benedict XV1 kujiuzulu kwa sababu ya umri.

Chanzo:Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top