Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu kunyongwa hadi kufa  washtakiwa sita  katika kesi ya mauaji ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa mkoani Morogoro na mfanyakazi wa Benki ya NMB.
 
Mauaji hayo ambayo yalipata umaarufu na kupewa jina la mauaji ya Ubungo Mataa yalifanyika Aprili 20,2006  jijini Dar es Salaam.
Jaji Projest Rugazia amewataja washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kuwa ni Mashaka Pastory, John Mndasha, Martine Mndasha, Haji Kiweru,  Wycliff Imbora na Rashidi Abdikadir.
Jaji Rugazia anasema aliwatia hatiani washtakiwa hao na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa,  kufuatia ushahidi ulitolewa na mashahidi 29 wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 78 vilivyowasilishwa mahakamani hapo na ushahidi wa utetezi.
“Maungamo ya washtakiwa, ushahidi wa kitaalam na utambuzi wa washtakiwa kutambuliwa eneo la tukio inaonesha wazi walikuwa na nia ya kujaribu kupora takribani Sh 150 milioni mali ya benki ya NMB zilizokuwa zikisafirishwa kutoka  Dar es Salaam kwenda  Morogoro tawi la Wami.” Anasema Jaji Rugazia.
Anasema siku hiyo ya huzuni  ya Aprili 20,2006  majambazi hao walilivamia gari  hilo kwa lengo la kupora lakini  bila ya kuwa na huruma yoyote walilimiminia risasi na kuwaua  D 6866 Konstebo Abdallah Marwa na mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest Manyonyi.
Walifanya tukio hilo nyakati za saa 6:30 mchana, eneo la Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Jaji Rugazia aliwaachia huru washtakiwa Rashid Lemblisi, Philipo Mushi, Yassin Juma,
Hamisi Daud, MT 77754 Nazareth Amurike, MT 76162 Emmanuel Lameck, James Chamangwana na Hussein Idd baada ya kuwaona hawana hatia katika kesi hiyo.

Kwa upande wa washtakiwa, Jackson Issawangu aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo na Mussa Mustafa aliyekuwa mshtakiwa wa 10 waliachiwa huru awali baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa hawana kesi ya kujibu.

Hadi wanaachiwa huru jana, washtakiwa hao walikuwa wamekwisha kaa  rumande kwa muda wa zaidi ya miaka 8.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top