Zaidi ya watu 1,000 kutoka Afrika Mashariki na
sehemu nyingine duniani wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wa siku tatu wa
Nishati ya Petroli na Maonyesho utakaofanyika mjini Arusha, kati ya Februari 6
na 8, 2013.
‘’Lengo kuu la Mkutano na Maonyesho haya ni kukuza
uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi kwa kuionyesha dunia rasilimali ya
nishati hiyo iliyopo katika kanda na kubadilishana taarifa juu ya hali ya
uendelezaji wa sekta hiyo katika kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC),’’ Dk. Nyamajeje Weggoro,Mkurugenzi wa Tija na Sekta ya Jamii
wa EAC aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongeza kwamba mkutano huo utatoa mada mbalimbali
za kiufundi zinazoonyesha maendeleo ya sekta ya mafuta ya petrol na gesi katika
EAC na duniani kwa ujumla wake.
‘’Hii ni nafasi ya kipekee kwa Afrika Mashariki
kuonyesha ugunduzi wa hivi karibuni wa uwepo wa mafuta na gesi na kuona ni
namna gani bora ya kuweza kuchimba rasilimali hiyo katika nchi wananchama,’’
alisema Dk. Weggoro. Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais Jakaya
Kikwete.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni : ‘’Kanda ya Afrika
Mashariki,eneo linaloibukia kwa uwekezaji na upatikanaji wa mafuta na gesi kwa
siku za usoni kwa maendeleo endelevu.
‘’Tumechagua kauli mbiu hiyo kwa sababu upo
ugunduzi mkubwa wa mafuta na gesi katika miaka miwili iliyopita Magharibu mwa
Uganda na katika maeneo mengine,ugunduzi wa gesi Kusini mwa Tanzania na ukanda
wa Pwani, ugunduzi mkubwa wa mafuta Kaskazini mwa Kenya na gesi pia ukanda wa
Pwani wa Kenya,’’ alieleza Dk. Weggoro na kuongeza ‘’hali hii imeifanya kanda
hii kuwa na mvuto wa aina yake kwa wawekezaji kutoka duniani kote.’’
Wajumbe waliothibitisha kushiriki katika mkutano
huo ni pamoja na viongozi wa biashara katika sekta ya nishati,mawaziri wa
shughuli za EAC, mawaziri wanaoshughulikia nishati, fedha na mipango toka nchi
tano za EAC na sekta nyingine muhimu, wawakilishi toka sekta binafsi, bodi
mbalimbali za kitaaluma, vyuo vikuu na kampuni kubwa za uchimbaji petroli na
gesi.
Mkutano huo wa Afrika Mashariki wa Nishati ya
Petroli unaofanyika kila baada ya miaka miwili ulizinduliwa rasmi mwaka 2003 na
unafanyika kwa mzunguko miongoni mwa nchi wanachama.
BN/NI
0 comments:
Post a Comment