Tanzania bado inakua ikiwa na changamoto ya uwezo katika Sekta ya Nishati ambayo ni muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wake kwa ujumla.

Rais Kikwete amesema hayo wakati anachangia katika mjadala maalum kuhusu uhamasishaji  wa sekta binafsi katika kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati barani Africa ambayo imeongozwa na shirika la misaada la Marekani la USAID na kuratibiwa na kiongozi wake bw. Rajiv Shah.

"Uwezo  wa kuzalisha na kuusambaza bado ni changamoto kwetu, tunataka kuacha kutegemea umeme wa maji pekee na kuanza kuzalisha kwa njia zingine mbadala lakini bado uwezo wetu Kama serikali ni mdogo na tumeamua kuwashirikisha watu binafsi ili umeme huu uweze kuwafikia wananchi walio wengi zaidi". Rais ameeleza.

 Rais Kikwete yuko mjini Davos, Uswis kuhudhuria kikao cha kila mwaka cha uchumi ambapo viongozi mbalimbali wa nchi, wakurugenzi wa mashirika na makampuni makubwa duniani huhudhuria kwa ajili ya kujadili changamoto, matumaini na mapendekezo kadhaa kwa lengo la kukuza na kuimarisha uchumi duniani.

Kikao cha kujadili uwekezaji wa Nishati barani Afrika, umehudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Bw. Tony Blair , Waziri Mkuu wa Ethiopia Bw Haile Mariam Desalegne  na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) Donald Kaberuka.

Katika kikao kingine ambacho kimehusu Kilimo na Usalama wa Chakula barani Afrika Rais Kikwete amesema Tanzania imetengeneza mkakati maalum kuhusu Kilimo ambao unatekelezwa Kama ulivopangwa na kuelezea kuwa kumekua na upotoshwaji kuhusu uwekezaji mkubwa katika Kilimo ambao umetafsiriwa Kama uporaji aw ardhi ya wananchi.

"Tanzania tunayo ardhi, na ardhi tunayotoa kwa wakulima wakubwa ni ardhi iliyotengwa na serikali kwa ajili ya wakulima wakubwa (land bank)" ameeleza.

Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo pia kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa nchi na wa makampuni binafsi waliopo Davos kwa ajili ya mkutano uchumi.

Rais Kikwete pia amepata fursa ya kuzungumza katika chakula maalum kilichoandaliwa na shirika la Roll Back Malaria ambapo washiriki wamezungumzia suala la diplomasia na Afya ambapo Rais Kikwete amesema serikali pekee haziwezi kutatua changamoto za Afya hivyo zinahitajika pia juhudi za nchi rafiki na mashirika binafsi.

"Tunahitaji kuimarisha huu uhusiano na kuendelea kufanya kazi pamoja kwani serikali zinahitaji sana wenza katika kutatua changamoto nyingi zilizopo katika Sekta ya Afya kwani kunahitajika nguvu zaidi ya zile za serikali" Rais amesisitiza.

Mwisho,

Imetolewa na Premi Kibanga
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi.
Davos-Switzerland
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top