MPANGO mchafu wa kukichafua Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Iringa umefichuka, huku Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Philipo Mangula akituhumiwa kuratibu harakati hizo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya CCM, zimebainisha kuwa, chama hicho kimechapisha mamia ya kadi za CHADEMA ambazo zimesambazwa kwa watu maalumu walioandaliwa ambao wameambiwa wazirejeshe leo wakati wa mkutano wa hadhara na kumkabidhi Mangula, wakidai wameihama CHADEMA.
Imebainika kuwa, zaidi ya wanafunzi 200 wa Chuo Kikuu kishiriki cha Mkwawa tayari wamekabidhiwa kadi hizo, na fedha za kujikimu ambapo watajitangaza kama wana-CHADEMA waliohamia CCM baada ya kuchoshwa na upinzani katika viwanja vya Mwembetogwa Manispaa ya Iringa.
Mbali na kadi, CCM pia imetengeneza fulana za CHADEMA walizopewa wanafunzi hao, na kwamba chama hicho kimemwaga maelfu ya fedha kwa wasomi hao kama njia ya kufanikisha mpango huo.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, Mtama Joseph amekiri kusikia taarifa hizo, lakini akadai kuwa kama ni kweli basi, utakuwa ni mpango unaotumika na watu waliopoteza mwelekeo.
“Ni kweli kuna taarifa hizo zimezagaa hapa chuoni kwamba kuna wanafunzi 200 ambao wamepewa sh 5,000 kila mmoja, na kadi zenye nembo ya CHADEMA ili warudishe kwenye mkutano wa CCM utakaofanyika kesho (leo) katika viwanja vya Mwembetogwa,” alisema.
Mtama alisema kama habari hizo ni za kweli, litakuwa jambo la kusikitisha na linaloonesha kuwa watu walioshindwa kufikiri na kuwajibika hutumia mbinu chafu kwa kuwa hawana fikra zingine zaidi ya rushwa.
Mmoja wa vijana wanaodaiwa kutumiwa katika mpango huo (jina limehifadhiwa) amekiri kuwa miongoni mwa viongozi wanaoratibu mpango huo na kwamba yeye na wenzake wameahidiwa sh 500,000 kila mtu pindi watakapofanikisha hujuma hiyo.
Kijana huyo aliyeomba jina lake lisitajwe kwa kuhofia usalama wake, alisema tayari kuna vijana 17 ambao wameandaliwa pamoja na kuratibu, lakini pia kufanya kazi ya kuichafua CHADEMA kwa namna watakavyoelekezwa pindi wakifika mkoani hapa kwa ajili ya mikutano ama shughuli nyingine.
Mbali na hilo, kijana huyo alisema CCM pia imeandaa magari kusomba wanachama wake kutoka vijijini kuletwa katika mkutano wa leo kwa madai ya kutaka ionekane ina wanachama wengi, hivyo kuondokana na aibu ya kukosa watu katika mkutano wake.
Katibu wa CHADEMA Manispaa ya Iringa, Suzan Mgonukulima alisema kuna mbinu chafu zilizobainika kutumika kuhujumu CHADEMA ambazo wananchi wanatakiwa kuwa nazo makini.
Alisema kufichuka kwa siri hizo, ni ishara wazi kuwa watu wanaojitangaza kurudi CCM sio wanachama halisi, bali waigizaji na kuonya kuwa mchezo huo ni ishara ya wazi kuwa sasa serikali inatishiwa na CHADEMA.
Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi (CHADEMA) ambaye pia ni mjumbe wa kamati tendaji ya wilaya, alisema propaganda za CCM zimepitwa na wakati na kwamba ni dalili za kutapatapa kwa sababu wanajua kuwa mwaka 2015 wanaachia ngazi.
Via Tanzania Daima

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top