Ni wengi katika jamii ambao hawafahamu umuhimu wa kupata muda mzuri wa kulala katika maisha yao.
Pia, wengi hawatambui jinsi ukosefu wa usingizi wa
kutosha ulivyo na athari kwao na kuwa kulala kwa muda mfupi kunapunguza
kichochezi dume kiitwacho testosterone.
Mwonekano wa mwanamume yeyote duniani na kupata sifa ya kuitwa mwanamume husababishwa na kichochezi hiki testosterone.
Kichochezi hiki kiletacho tabia na maumbile ya
kiume na kumpa mtu sifa ya kuitwa mwanamume kinaweza kuathiriwa na
ukosefu wa usingizi wa kutosha.
Kichochezi hiki kinazalishwa katika sehemu za
uzazi za mwanamume katika korodani na hutiririshwa kutoka korodani na
kusambaa kwenye sehemu mbalimbali za mwili kupitia njia ya damu.
Homoni hii ndiyo inayotoa maumbile na kazi za
kimwili kwa wanaume na hufanya maumbile ya kiume kuwa na misuli iliyo
kakamavu, mifupa imara, kuota ndevu, kupata ndevu za kifua, kuongezeka
maumbile ya viungo vya uzazi, kuwa na sauti nzito, kumfanya mtu apate
hamu ya kujamiiana, kuwa na mikono iliyojitokeza kwa nje, kutembea
kibabe.
Pia, kichochezi hiki hasa kwa wanaume hutokea kuwa na upara kichwani.
Nini athari ya kupungua kichochezi hiki?
Wanaume wengi wanapofikia umri wa miaka 30 au
zaidi, wengi wao hudhani kuwa kupungua kwa uwezo wao wa kujamiiana
kunasababishwa na umri mkubwa, kumbe sivyo.
Hilo si sahihi, bali ni kupungua kwa kichochezi
hiki cha testosterone. Moja ya athari ya kupungua kwa kichochezi hiki ni
kupungua kwa nguvu za kiume na kutofika kileleni, kukosa mwamko wa
kujamiiana, kupata ugumba kwa wale walio katika umri wa uzazi.
Mambo haya yakitokea humwathiri mhusika
kisaikolojia na kumfanya kuwa na sonono (depression), kuwa na tabia za
ukali, msongo wa mawazo, unyongofu, kujitenga na jamii kwa kule kuhofia
kunyanyapaliwa, misuli ya mwili kupungua uzito na uimara, huwa katika
hatari ya kupata maradhi ya moyo.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wenye upungufu wa homoni hii hufa mapema kulinganisha na wale wasio na tatizo hili.
Nini kinatokea mtu akikosa usingizi?
Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha wanaume wengi
wanaolala kwa muda mfupi huwa na kiwango kidogo cha kichochezi hiki.
Utafiti uliochapishwa mwaka 2006 katika jarida la Sleep and Sports
Health uliohusisha wazee wa umri wa zaidi ya miaka 50 unashangaza.
“Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa
wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala
nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone
wakati wa asubuhi,” anasema Plamen Penev kutoka Chuo Kikuu cha Chicago,
Marekani.
Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi
huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi
kwa wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea
kushiriki kwenye utafiti huo.
Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.
Matokeo ya uchunguzi huo yalionyesha kuwa kiasi
cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango
cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi.
Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu
(walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati
wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha
chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa saa sita.
“Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu
yanaonyesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria
cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya
utafiti huu yanatoa picha ya nini kinachotokea mwilini mtu asipopata
usingizi wa kutosha.
Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili
kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya
homoni katika mwili,” anasema Dk Penev.
Ushauri
Ili kuimarisha kiwango cha kichochezi hiki ni vyema kuepukana na mambo yanayoweza kuingilia usingizi wako.
Kwa mfano, kuzima kompyuta, simu, taa, runinga, redio na kuacha kulala na vikuza sauti masikioni.
Tengeneza mazingira ya chumba chako yawe na joto
la wastani na uende haja ndogo kabla ya kulala. Inafaa kuongeza muda
wako wa kulala kwa saa kumi na muhimu kula lishe bora na mazoezi ya
wastani.
Kadri unavyopata usingizi ndivyo kiwango chako cha testosterone huongezeka na kuipa uimara misuli yako ya mwili.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment