Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
ametangaza tarehe rasmi ya kuanza kwa mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya
wilaya, huku akiwaonya watu wa kada mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa
kutokuingilia mikutano hiyo.
Vilevile Jaji Warioba alieleza sababu za Tume hiyo
kupendekeza Serikali tatu, huku akisisitiza kuwa suala hilo lilikuwepo
tangu siku nyingi na Tume iliamua kupendekeza Serikali tatu kwa kuwa
ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuulinda muungano.
Kauli hiyo inaonekana kama kukijibu Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambacho kimependekeza kuwepo kwa Serikali mbili, ikiwa
ni siku chache baada ya kutolewa kwa Rasimu ya Katiba.
Mikutano hiyo inafanyika baada ya Juni 3 mwaka
huu, Tume hiyo kutoa rasimu ya Katiba na kusambaza katika vijiji, mitaa
na shehia kwa ajili ya kujadiliwa na wananchi, ambao nao watachangia
mawazo yao kwa wawakilishi wao waliowachagua kuwa wajumbe wa Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, inaeleza
kuwa mikutano hiyo itaanza Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu na
kutakuwa na jumla ya Mabaraza 177, Tanzania Bara 164 na Zanzibar 13.
Tayari Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo katika
mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa mapendekezo yake yanapitishwa huku
kikitumia wajumbe wa Mabaraza ya Katiba wakiwemo wa ngazi ya mtaa, huku
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye akiwaeleza
wajumbe wa mabaraza ya Katiba jijini Dar es Salaam juzi azma ya chama
hicho kuwa na rasimu mbadala.
Wakati CCM wakieleza hayo, Kamati Kuu ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana leo na kesho katika kikao
cha dharura jijini Dar es Salaam ili kujadili pamoja na mambo mengine
Rasimu ya Katiba Mpya.
Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere,
anayemaliza muda wake, Profesa Issa Shivji, Juni 21 mwaka huu alisema
kama Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano ikikubaliwa bila
mabadiliko makubwa itasababisha kuvunjika kwa Muungano.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji
Warioba alisema hairuhusiwi kwa makundi, vyama vya siasa au mtu yeyote
kuingia katika mabaraza hayo kwa lengo la kushawishi kukubaliwa na maoni
ya aina fulani. Alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali na gazeti
hili, juu ya taarifa zilizopo kwamba baadhi ya vyama vya siasa nchini
vimeandaa rasimu zao kwa lengo la kuwashawishi wajumbe wa mabaraza
kupitisha maoni yao.
“Mikutano na Mabaraza ya Katiba siyo ya kupiga
kura bali ni kujadili na kutoa hoja ambazo zitakuwa na msingi kwa
masilahi ya taifa na siyo kutetea masilahi ya kundi au watu fulani,”
alisema Jaji Warioba na kuongeza;
“Hilo la vyama kuandaa rasimu zao kwa lengo la
kuingilia utaratibu huu sijalisikia, ila kikubwa ni kwamba si ruhusa
kuingilia mchakato huu kwa sababu utafanyika kwa mujibu wa taratibu
zilizopo,” alisema Warioba na kusisitiza; “Wananchi watoe maoni ambayo
yatasaidia kuiboresha rasimu iliyotolewa kwa kuweka mbele masilahi ya
taifa na kuepuka ubinafsi wa mtu mmojammoja au makundi ya aina yeyote.”
Alisema Tume yake itapokea maoni na mapendekezo
yote ambayo yatakuwa na lengo la kuiboresha rasimu ambayo itaweka umoja
wa kitaifa na siyo kuwagawa Watanzania.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Tunazidi kuwaomba wasiishie kutoa maoni na hofu zao, bali
wasaidie tume kutoa mapendekezo ambayo yataisaidia tume katika kazi yake
ya kuwapatia Watanzania katiba iliyokuwa bora,” alisema.
Akizungumzia sababu za kupendekeza Serikali tatu,
Warioba alisema kama wangependekeza Serikali ya mkataba ilikuwa lazima
kuvunjwa kwa muungano na kuwepo kwa Serikali mbili ambazo baadaye
zingekaa na kuamua kushirikiana ama laa, jambo ambalo lingekuwa gumu.
“Wapo waliotaka Serikali mbili, lakini katika hilo
wapo waliosema kuwa Zanzibar wana wimbo wao wa taifa na bendera, pia
wamejiunga na OIC na hata Katiba yao inasema kuwa Zanzibar ni nchi,
Watanganyika nao wangeanza kuhoji Tanganyika iko wapi,” alisema.
Alisema ndiyo maana walipendekeza Serikali tatu na
kwamba kama wangeamua kuvunja muungano operesheni za sheria tulizonazo
zingewatenganisha wananchi, kama soko la pamoja, sheria ya ardhi,
mwingiliano wa pande mbili, biashara, matibabu na shule.
Alisema Serikali tatu ndiyo suluhisho la kudumisha
muungano kuliko Serikali moja au mbili, na kwamba katika kura ya maoni
jambo la uwepo wa Serikali tatu linategemea uamuzi wa viongozi.
Akizungumzia idadi ya wajumbe wa mabaraza hayo
alisema Tanzania Bara kutakuwa na wajumbe 18,174 na Zanzibar 1159 na
kwamba tume itatumia siku 54 kuendesha Mabaraza ya Katiba nchi nzima.
“Ili kuweza kufika sehemu zote za nchi, tume
imejigawa katika makundi 14 na kila kundi litaendesha mikutano ya
Mabaraza ya Katiba ya wilaya katika Mamlaka za Serikali za mitaa 12 au
13 na mikutano itafanyika kwa siku tatu,” alisema.
Alisema mikutano ya kwanza itafanyika katika mikoa
ya Kagera, Shinyanga, Mara, Kigoma, Tabora, Lindi, Arusha, Kilimanjaro,
Tanga, Mkoa wa Kusini Unguja, Mbeya, Rukwa, Mtwara na Njombe.
CCM
Tangu rasimu hiyo ilipotolewa mapema Juni mwaka
huu, chama hicho kilionyesha kutokuridhishwa na rasimu hiyo na kuahidi
kuipeleka kwa wanachama wake.
Katika kuonyesha kutokuridhshwa huko, Katibu wa
Itikadi na Uenezi Nape Nnauye aliwaeleza wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
jijini Dar es Salaam juzi azma ya chama hicho kuwa na rasimu mbadala.
Nape ambaye aliitumia siku nzima ya Alhamisi
kuzungumza na wajumbe hao wa mabaraza, alisema wameandaa rasimu yao
ambayo imeandikwa vitu wanavyohitaji na wanachama wote wanapaswa
kuvisimamia.
Kauli ya Shivji
Alisema ili kurekebisha kasoro hizo CCM kimeandaa rasimu ambayo
imetengenezwa katika mazingira ya kisiasa na kitaalamu ambapo haitokuwa
mzigo kwa chama hicho.
Alisema katika vitu muhimu ambavyo wanapaswa wajumbe wa chama hicho kuvipigania ni pamoja na suala la Serikali tatu.
Nape alisema kipengele cha Serikali tatu ambacho
kinaitwa Serikali ya shirikisho kinapaswa kupiganiwa kifutwe kutokana na
nchi kutokufikia hatua ya kuwa shirikisho.
Alisema kitengo cha kuweka Serikali tatu kinaweza kuongeza urasimu pamoja na kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali hizo.
Alisema harakati za kutangaza rasimu ya CCM
zinafanyika nchi nzima kwa kutumia makada wa chama hicho katika baadhi
ya mikoa ambapo katika Visiwa vya Zanzibar zoezi hilo lilifanyika Julai
tatu.
Alisema rasimu hiyo inatarajiwa kwenda kupelekwa
katika kikao cha Wajumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) itajadiliwa na wajumbe
wote ili kuweza kupata mawazo mengine ya wajumbe.
Chadema nao wakutana
Taarifa iliyotolewa na chama hicho imetaja mambo
mengine yatakayojadiliwa kuwa ni pamoja na taarifa ya hali ya siasa
nchini, taarifa juu ya mfumo wa uendeshaji wa chama kwa kanda (uzinduzi)
na taarifa juu ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 26,
uliofanyika Juni 16, 2013.
Kauli ya Shivji
Kauli hiyo ya Shivji aliitoa katika Ukumbi wa
Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati akitoa mhadhara wa kuaga
wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Kigoda hicho kwa Wanakigoda wenzake na
jumuiya ya chuo hicho.
Profesa Shivji aliainisha upungufu uliomo katika
rasimu hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ambapo alisema
yanaweza kusababisha kuzuka kwa migogoro mingi na mikubwa itakayovunja
Muungano.
Alibainisha rasimu hiyo imekosa maelezo ya wazi na
thabiti kuhusu ukuu wa Katiba ya Muungano juu ya katiba nyingine za
washirika wa Muungano, hali itakayosababisha migongano na kutokuelewana
kati ya mamlaka za washirika wa Muungano na mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano.
Alisema kuwa Ibara ya nane ya rasimu hiyo inayozungumzia ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa ina kasoro kubwa kwani imeeleza kuwa ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano utakuwa katika mambo ya Muungano tu na si vinginevyo.
Mwananchi
Alisema kuwa Ibara ya nane ya rasimu hiyo inayozungumzia ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa ina kasoro kubwa kwani imeeleza kuwa ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano utakuwa katika mambo ya Muungano tu na si vinginevyo.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment