SERIKALI imekubali kuzungumza na wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kuhusu jinsi gesi ya asilia inayotoka katika mikoa hiyo itakavyowanufaisha wao na taifa zima kwa ujumla. “Tutaendelea kuzungumza na kuelimishana na wananchi wa Mtwara kuona namna gani itawamnufaisha wao… na taifa zima,” alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Pinda alikuwa akizungumza kwenye mkutano kati yake na wahariri wa vyombo vya habari, viongozi wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) na maofisa na wajumbe wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), nyumbani kwake Oysterbay Dar es Salaam juzi usiku.

Alisema kutokana na gesi hiyo asilia ni wazi kwamba Mikoa ya Mtwara na Lindi itakuwa na mabadiliko makubwa ya maendeleo katika miaka michache ijayo.

Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya kuulizwa swali la kama serikali itakuwa tayari kuzungumza na wananchi wa Mtwara juu ya kuhusu suala la gesi ya asilia kutoka mkoani humo kutokana na vurugu zinazoendelea hivi sasa mkoani humi.

Wananchi hasa wa Mkoa wa Mtwara wamekuwa wakifanya maandamana na vurugu kupinga hatua ya serikali kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kuzalisha umeme na matumizi mengine.

Vurugu za kupinga hatua hiyo ambazo hadi sasa zinaendelea katika maeneo mbalimbali mkoani humo zilianza kwa maandamano yaliyofanyika Desemba 27 mwaka jana.

Inaelezwa kwamba wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanataka mtambo wa kuzalisha umeme kutokana na gesi hiyo asilia ujengwe hukohuko Mtwara licha ya manufaa mengine.

Pinda alisema wananchi wa Mtwara na Lindi wana haki ya kuhoji manufaa watakayoyapata kutokana na gesi hiyo inayotoka mikoani mwao.

“Ni bahati mbaya kwamba elimu ya kutosha haijatolewa ili wananchi hao waelewe manufaa watakayoyapata wao na taifa zima kwa ujumla,” alisema.



Alisema serikali itaendelea kuzungumza na wananchi pamoja na makundi mbalimbali ili suala hilo liweze kueleweka kwa wote.

“Mimi mwenyewe nitakwenda Mtwara… Tutaendelea kuelimishana kwa kila hali nchi isiende pabaya,” alisema.

Hata hivyo alisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi rasilimali zote nchini hazina budi ziwanufaishe wananchi wote na siyo pale zilipo tu.

Alisema gesi asilia ina matumizi mengi kama vile kuzalisha umeme na kutumika viwandani kama vya saruji, mbolea na matumizi ya majumbani na katika magari.

“Lakini ieleweke kwamba gesi iliyogundulika nchini ni nyingi mno, kiasi kikubwa kikiwa chini ya bahari kilomita 180 kutoka nchi kavu... gesi hiyo haijachimbwa hadi sasa,” alisema.

Alisema bomba linalotarajiwa kujengwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, hatua itakayowezesha taifa kuondokana na matatizo ya sasa ya umeme na hivyo kuchangia kuinua uchumi wa nchi kwa haraka.

“Pamoja na kuzalisha umeme gesi hiyo itakayosafirishwa Dar es Salaam pia itatumika viwandani, majumbani na baadaye hata katika magari,” alisema.

Pinda alisema bei ya umeme kwa walaji nchini pia itaweza kupungua kutoka kiasi cha sasa cha wastani wa senti 40 kwa uniti hadi senti 7 hadi 8 kwa uniti.

Alisema mkoani Mtwara pia utajengwa mtambo wa umeme, kiwanda cha mbolea na cha saruji na viwanda vingine wakati mkoani Lindi pia kitajengwa kiwanda cha saruji na vingine.

Hata hivyo alisema hadi sasa gesi ambayo imekwisha kuchimbwa na asilia saba tu huko Songosongo na kiasi kikubwa hakijachimbwa kikisubiri ukamilishaji wa miundombinu muhimu likiwamo hilo bomba.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Nishati na Madini, gesi asilia iliwisha kugundulika nchini ni mita za ujazo trilioni 31 baharini pwani ya Mtwara, Msimbati Mnazi Bay (Mtwara) trilioni mbili, Songosongo trilioni 1.2.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa katika visima vinne vilivyoko Msimbati ni kimoja tu kinachotumika kuzalisha umeme wa megawatt 18 unaotumika Mtwara na Lindi hivi sasa.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kwamba ni asilimia 16 tu ya gesi asilia kutoka Mtwara ndiyo itakayopitishwa katika bomba litakalojengwa hadi Dar es Salaam.

Mkutano huo wa juzi wa Pinda na wahariri wa vyombo vya habari pia ulihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jasmine Kairuki.

Via Mtanzania TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top