Vurugu katika Wilaya ya Masasi, zimekuwa ni mwendelezo wa fujo ambazo juzi, zilisababisha mali nyingi na nyumba za viongozi wa taifa mkoani humo kuchomwa moto.
Mbali na hayo, magari 12 yakiwamo ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, nyumba ya Mbunge wa Masasi Mariam Kasembe (CCM), kituo kidogo cha Polisi Sokoni na Ofisi ya Wilaya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vimeteketezwa kwa moto.
Mbali ya nyumba hiyo, nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum na Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Anna Abdallah nayo ilichomwa moto.
Mbali ya kuchomwa moto, wananchi hao waliwapiga wafanyakazi na mlinzi wa nyumba hiyo na kuwajeruhiwa.
Habari kutoka Masasi zilieleza kuwa mji huo pamoja na vitongoji vyake, jana uligeuka uwanja wa mapambano ya wananchi na polisi ambao walizidiwa nguvu na kukimbia.
Kitendo cha polisi kukimbia kilisababisha wananchi waliokuwa wakirusha mawe na kila aina ya silaha kupata upenyo wa kwenda kwenye gereza na kuvunja milango yote.
Habari zinasema, vurugu hizo zilianza saa 2.00 asubuhi baada ya kundi kubwa la wananchi wakiongozwa na waendesha pikipiki, bajaj na baiskeli, kuandamana hadi kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya, wakitaka gesi isisafirishwe kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Maandamano hayo yaliyoanzia Mtaa wa Mkuti eneo la Yatima, yalianza kwa utulivu, lakini kadrii walivyosegolea kituo hicho mambo yakaanza kubadilika.
Baada ya polisi kuona wananchi wamekuwa wengi, walianza kupiga mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya lakini wananchi hawakutawanyika.
Baada ya kuona mabomu yamezidi, wananchi hao walibadili mwelekeo na kuelekea Kituo Kikuu cha Mabasi kilichoko mtaa wa Madukani, ambako huko walifanya kila aina ya fujo na polisi walifika kupiga mabomu mengi.
“Inavyoonekana polisi waliishiwa mabomu ya machozi na kuamua kurudi kituoni. Kitendo hiki kiliwapa mwanya kwenda kuchoma moto kituo kidogo cha Polisi Sokoni, Ofisi ya CCM Wilaya na kuharibiwa magari ya Halmashauri ya Wilaya pamoja na Ofisi ya Mahakama ya Mwanzo Masasi ya Masasi.
“Wananchi hawa walikuwa wakiimba nyimbo za kuhamasisha gesi isitoke Mtwara, walivamia na kuteketeza kwa moto nyumba ya Mbunge wa Masasi, Mariam Kasembe (CCM) iliyopo Mtaa wa Mkuti karibu na Baa ya Kibo Park.
Habari zinasema, baada ya polisi wilayani Masasi kuzidiwa, waliomba msaada wa askari wa ziada kutoka Mtwara mjini, ambao walifika na kuanza kupiga mabomu ya machozi na risasi za moto, hasa katika mtaa wa Machinjioni ambako kuna nyumba nyingi za watumishi wa Serikali.
“Huwezi amini wananchi walivamia mtaa huu, ambao wanaishi wafanyakazi wengi wa Serikali na kuchoma nyumba kadhaa, ikiwamo ya polisi mmoja ambaye inasadikiwa ameuawa,”alisema mmoja wa wananchi walioshuhudia tukio hilo.
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye kutoka Makao makuu ya Jeshi la Polisi nchini zilielezwa kuwa Kamanda wa Operesheni Kamisha Paul Chagonja na maofisa wengine wamewasilia Mtwara kuongeza nguvu.
NEWALA
Habari zilizoifikia MTANZANIA Jumapili, zinasema fujo za aina hiyo zimeanza kuibuka wilayani Newala.
Habari zinasema wananchi waliokuwa na hasira, walianza kuelekea kwenye nyumba ya Mbunge wa Newala, Kapteni George Mkuchika kwa ajili ya kuichoma moto.
VIONGOZI WA DINI
Vurugu zinazoendelea nchini zimeonekana wazi kuwatisha viongozi wa dini ambao wamaetoa matamko mbalimbali;
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Peter Kitula aliliambia MTANZANIA JUMAPILI kuwa Serikali inapaswa kuchukua jukumu lake la kusimamia amani kwa kukaa na wananchi wenye malalamiko kutafuta muafaka wa kudumu.
Alisema amani inaendelea kupotea taratibu huku serikali ikishindwa kujua kiini cha vurugu hizo.
Dk. Kitula ambaye pia ni Rais wa Tume ya Kikristo Tanzania (CSSC), alisema Serikali inapaswa kuchukua nafasi yake kwa kukaa pamoja na wananchi, badala ya kutumia mabomu.
“Msimamo wangu kama kiongozi wa watu, ninaona kitendo cha Serikali kuachia mambo haya kuendelea kama ilivyo sasa ni hatari.
“Amani imeanza kutoweka taratibu kana kwamba tumefungwa ufahamu, nawasihi wananchi wenye mgogoro na Serikali kuwa na subira, watoe hoja zao bila jaziba ili hatimaye muafaka upatikane.
“Lakini pia serikali nayo iwe wazi kwa wananchi wake, nchi hii tumepewa bure na Mungu, hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine, kufanya mambo kwa kificho ndiyo kumetufikisha hapa,” alisema Dk. Kitula
MZEE WA UPAKO
Naye Mchungaji wa Kanisa la Maombezi lililoko Ubungo Kibangu i Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako, amesema vurugu zinazoendelea ni matokeo ya watu kukata tamaa na kukosa imani na viongozi wao.
Alisema viongozi wa Serikali wanafanya mambo watakavyo matokeo yake wananchi wanaamua kujichukulia sheria mkononi kusaka haki zao.
“Hakuna dawa kwa Serikali kukabiliana na vurugu hizi, kinachotakiwa ni kuwa na dhamira ya dhati ya kutenda kile wanachokisema, kukaa pamoja na watu wanaolalamika.
“Ushirikishwaji wa wananchi usiwe wa juu juu tu, uwe kwenye dhamira zao, vinginevyo mambo haya hayatakwisha. Serikali inadhibiti wananchi wake kwa siasa si kwa mabomu wala mtutu wa bunduki.
“Duniani kote hakuna serikali iliyowahi kushinda umma kwa mtutu wa bunduki. Huwezi kuwapelekesha wananchi kama ng’ombe halafu ukafaulu, utashindwa tu. Viongozi wawaeleze wananchi kinagaubaga siyo kuwaburuza,” alisema Mchungaji Lusekelo.
MCHUNGAJI MWAMALANGA
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kipentekosti la Kiinjili Tanzania, William Mwamalanga, alisema mgogoro wa gesi unaoendelea mkoani Mtwara unaratibiwa na kampuni zinazofanya biashara na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mchungaji huyo ambaye hivi sasa yuko Mtwara na timu yake kwa lengo la kuombea ufahamu kwa wananchi, alisema kampuni hizo zimezoea kuvuna fedha nyingi kutokana na kuliuzia shirika hilo mali ghafi za kuzalisha umeme na sasa zinaona ‘ulaji’ huo unaelekea ukingoni.
“Kampuni hizi na nyingine ziko nyuma ya mgogoro huo kwa sababu hazitaki kuona Tanzania inaondokana na tatizo la umeme ambao unatarajiwa kuzalishwa kwa wingi kutokana na gesi.
“Mchezo huo umeingizwa kwa wananchi wadogo wasiojua maana ya uchumi. Ni mbinu za wakandamizaji wa uchumi wa Tanzania wanataka waendelee kunufaika na mapato yatokanayo na umeme wanaowauzia Tanesco.
“Ni mkono wa mataifa ya nje, mbinu ya kuzuia gesi kuja Dar es Salaam ni mbinu hatari kwa uchumi na maisha ya Watanzania wenyewe.
“Nawashauri wanasiasa na wachumi kama Profesa Ibrahimu Lipumba, Zitto Kabwe na wengine wasiingize siasa chafu katika suala hili.
“Gesi kuja Dar es Salaam haina maana Mtwara na Lindi gesi hiyo haitatumika na si kweli kwamba mikoa ya kusini haitanufaika. Mpango wa Serikali ni kuleta manufaa kwa Mtwara yenyewe na taifa kwa Ujumla.
Via Mtanzania TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment