YANGA WAIPIGA MWELEKA TANZANIA PRISONS
Kikosi cha Yanga
Kikosi cha Prisons
Mabingwa wa Afrika Mashariki na kati YANGA SC wamezidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu  Tanzania Bara, baada ya jioni hii kuitandika Prisons ya Mbeya mabao 3-1 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 32 baada ya kucheza mechi 14, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa wastani wa pointi tano, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba 26 Matokeo mengine ya mzunguko wa pili ligi kuu Tanzania kwa michezo iliyopigwa jana.
Simba 3 – 1  African Lyon
Azam 3 – 1   Kagera Sugar
Mtibwa 0 – 1 Polisi Morogoro,
JKT Oljoro 3 – 1 Toto Africans,
Coastal 3 – 1Mgambo Shooting,
Ruvu Shooting 1 – 0 JKT Ruvu Stars
PAMBANO LA LYON, SIMBA LAINGIZA MIL 53/-
Mechi namba 92 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Januari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 limeingiza sh. 53,756,000.
Watazamaji 9,408 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 12,499,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 8,200,067.80.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 6,355,806.33, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 3,813,483.80, Kamati ya Ligi sh. 3,813,483.80, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,906,741.90 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,483,021.48.
PINGAMIZI ZA KUMWAGA UCHAGUZI MKUU WA TFF
WAGOMBEA wote wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu, wamewekewa pingamizi wasigombee uongozi kwa sababu mbalimbali.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, amewaambia Waandishi wa Habari mchana huu katika ukumbi wa Mikutano wa TFF, uliopo Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kwamba, jumla ya pingamizi 14 zimewafikia tangu Jumatatu wiki hii hadi zoezi hilo linafungwa jana.
Angetile aliwataja wagombea waliowekewa pingamizi kuwa ni Jamal Malinzi, Athumani Nyamlani wanaogombea Urais wa TFF, nafasi inayoachwa wazi na Leodegar Tenga anayeng’atuka, Michael Wambura anayegombea Umakamu, nafasi inayoachwa wazi na Nyamlani anayehamia kwenye Urais.
Angetile alisema kwamba kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu, wagombea wa Uenyekiti Yussuf Manji, Ahmad Yahya Juma na Mgombea Umakamu, Mohamed Said pia wamewekewa pingamizi.
Aidha, wagombea wa nafasi za Ujumbe, Epatha Swai, Eliud Mvella na Athumani Kambi nao wamewekewa pingamizi.
Nyamlani amewekewa pingamizi mbili, moja na Mtanga Yussuf Gacha na nyingine ya Menard Justinian, wakati Malinzi amewekewa pingamizi moja na Agape Fuwe na Wambura ana pingamizi mbili, moja ya Osiah Samuel Msengi na nyingine ya Saidi Rubeya.
Epatha Swai amewekwa pingamizi na Ramadhan Sesso na Sos Chalamila, Eliud Mvella amepingwa na Saidi Kiponza, Abdul Changawa na Peter Namengi, wakati Athumani Kambi amepingwa na Jeremiah John Wambura
Wakati Manji amewekewa pingamizi mbili, na mwanachama maarufu wa Simba, Daniel Tumaini Kamna na mwanachama wa Yanga, Juma Ally Magoma, Frank Mchaki amewawekea pingamizi Ahamd Yahya na Mohamed Said.
Angetile amesema Kamati itakutana Jumatano kujadili pingamizi hizo na amewakumbusha wote waliowekewa pingamizi kufika ofisi za TFF saa 4:00 asubuhi siku hiyo kusikiliza pingamizi zao. TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top