TAARIFA YA
NDUGU ZITTO KABWE (MB) KUHUSU YANAYOENDELEA
MTWARA NA
MRADI WA BOMBA LA GESI ASILIA
Serikali
iache kutafuta mchawi, iende Mtwara
Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo,
malumbano na vurugu kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa
kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko
miradi mingine yote ya miundombinu
iliyopata kutokea hapa nchini. Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani
1.2 bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.
Wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27
Desemba 2012 wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa ya kusini kutokana na
mradi huu wa bomba la gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita
wahaini, watu hatari na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba
hawataki gesi itoke Mtwara.
Kimsingi Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya
wananchi wa Mtwara kuhusu mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa
ikijaribu kupotosha madai ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya
habari.
Tangu maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya
hadhara na
hatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya
watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya
mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya
kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona
namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo,
kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo.
hatimaye matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya
watu na majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya
mradi huu, imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya
kwenda Mtwara kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona
namna ya kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo,
kusikiliza na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea mkoani humo.
Mwezi uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya kushughulikia
tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro
huu.
Leo hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali
za wananchi zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza maisha. Tunalaani
matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea Mtwara si Utanzania.
Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu kwa kuwashirikisha, hali
itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.
Hivi sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia
suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje
yanachochea mgogoro huu.
Kwanza, Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala
hili limechukuliwa kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa baadhi
ya makampuni ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichochea
wananchi wa Mtwara.
Katika mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa ‘management by press conferences’ jana
Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu George Simbachawene aliwaambia
wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe ninachochea wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na
si mzalendo. Vile vile alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga
bomba la gesi ni gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.
Katika kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika
Mtwara. Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu,
kama Mtanzania kuhusu suala hili.
Nimeandika makala nne na zimechapishwa katika magazeti
kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (http://zittokabwe.wordpress.com/).
Niliandika: Utajiri
wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi. Nikaandika
tena: Tusipuuze mandamano
dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha Uwajibikaji; Nikaandika tena:
Mtwara
: Serikali inavunja nchi kwa kutosikiliza Wananchi; ni baadhi
ya makala nilizoandika kuhusiana na suala la Mtwara.
Sitaki kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya
Serikali kwa sasa. Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na
kurushiana maneno wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi
bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.
Yanayotokea Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya
kukabili changamoto za utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya
yanayotokea Mtwara yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya iwapo
tutaweka uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye unyonyaji wa
maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.
Rais Kikwete
Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara
Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power
System Master Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais
Jakaya Kikwete aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu mradi
huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na kujenga msongo wa
umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi? Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 12
Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka
makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export
Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia
kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi
Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100
kutoka Mtwara hadi Singida. Mradi huu ungegarimu dola za kimarekani milioni 684
na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana. Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini
Serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa
Mtwara? Taarifa ya Ikulu kuhusu mradi huu
imeambatanishwa hapa.
Tufanyeje?
Hapa tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio
cha wananchi wa Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa
Mtwara na Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje’? Jibu la swali hili si ahadi za
miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia suala
hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha.Viongozi wa kisiasa wenye
ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara
kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize kwanza.
- Lazima viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si kuwahutubia tu. Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa mwafaka. Rais mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu suala hili. Ni wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara, kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili. Wakati hatua hii inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yeyote ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana.
- Wakati juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya dola za kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya Nishati na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri katika mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo njia pekee ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.
- Wakati tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema Serikali ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya Serikali yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na rasilimali ya gesi asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara wanataka uwajibikaji wa Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka na porojo za orodha ya miradi isiyotekelezwa.
Viongozi twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi
inaungua na hatuwezi kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama
vita vya MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi wangu
wa chama kutoa ridhaa.
ZITTO KABWE
Mbunge, Kigoma Mjini (Chadema)
Waziri Kivuli wa Fedha
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment