STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.1.2013
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
ameungana na maafisa na askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama wa
Serikali ya Jamhuri nya Mungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ambao wameshiriki katika gwaride la kutimiza miaka 49 ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika chakula maalum cha mchana alichowaandalia.
Hafla
hiyo fupi imefanyika katika viwanja vya Polisi Ziwani mjini Zanzibar na
kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vikosi vya Ulinzi na Usalama
pamoja na viongozi wa Serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na viongozi wengine.
Akitoa
salamu za shukurani na pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa maandaalizi hayo
maalum ya chakula cha mchana kwa vikosi hivyo, kwa niaba ya vikosi hivyo
Kamanda wa Brigedia ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali Sharif Sheikh
Othman alisema kuwa hatua hiyo imewapa faraja kubwa kutokana na ushiriki
wake binafsi katika chakula hicho cha mchana alichowaandalia.
Alisema
kuwa hatua hiyo itavisaidia kwa kiasi kikubwa vikosi hivyo kukaa pamoja
na kubadilishana mawazo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya gwaride
hilo waliloshiriki hivi karibuni pamoja na kuweka mikakati ya maandalizi ya gwaride lijalo la kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Brigedia
Jenerali huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa vikosi vya Ulizni na
Usalama vitaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na
mali zao.
Nae
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Mwinyihaji Makame Mwadini akitoa neon a shukurani kutokana na ushiriki
wa vikosi hivyo katika hafla hiyo, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar,
alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha
ushirikiano na vikosi hivyo ili kuleta mafanikio zaidi.
Alisema kuwa Serikali
inatambua na inathamini mchango mkubwa unaotolewa na vikosi hivyo
katika masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu
katika kusimamia ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wake, kushiriki
katika maafa, michezo pamoja na ushiriki wao mkubwa katika gwaride la
sherehe za Mapinduzi.
Dk.
Makame alisema kuwa sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi matukufu
ya Januari 12,1964 zilifana na kupata sifa kubwa sana kwa kila
aliyeziona jambo ambalo limechangiwa zaidi na gwaride lililochezwa na
vikosi hivyo ambalo lilifana sana.
Pamoja
na hayo, Dk. Makame alivieleza vikosi hivyo kuwa juhudi za makusudi
zitachukuliwa katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinafanyiwa kazi
kwa lengo la kujiweka tayari na kujitarisha kwa sherehe za kutimiza
miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hapo mwakani.
Hafla
hiyo ni muendelezo wa Dk. Shein katika kuvipongeza vikosi vya Ulinzi na
Usalama vilivyoshiriki gwaride katika sherehe za Mapinduzi ambapo hapo
mwaka jana pia, hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Kambi ya Jeshi
la Ulinzi na Usalama Bavuai Migombani, mjini Zanzibar kwa kuwaandalia chakula maalum cha mchana na kula nao pamoja.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein aliwaandalia chakula cha mchana vijana wa Chipukizi
na Halaiki walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi huko
katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar ambapo pia, Dk. Shein
amewaandalia chakula hicho maalum cha vijana hao katika hoteli hiyo hapo
kesho.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment