Dk. Kitima alitoa kauli hiyo jana mkoani hapa mbele ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Masatu Wasira, ambapo
alisema CCM imeonyesha idhaifu mkubwa katika kusimamia baadhi ya mambo.
Wasira na Dk. Kitima walikuwa kwenye mjadala wa Dira ya Maendeleo ya
Serikali, uliofanyika mbele ya wanafunzi wa chuo hicho cha SAUT Nyegezi,
jijini Mwanza.
Dk. Kitima alisema licha ya Wasira kutokuwa fisadi na ni mwanafunzi
mzuri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alimtaka
awaambie wenzake wajiandae kuondoka kwa aibu.
“Mfano mzuri, Singapore wao walianza kusimamia utalii, lakini serikali
yetu ilikosea sana kutokutekeleza mambo ya uzalishaji. Na msipotekeleza
hili, CCM mtaondoka madarakani.
“Ulaji mkubwa wa fedha umeingia sekta ya elimu, hamtekelezi kwa
vitendo sera na dira za taifa. Nasema msipobadilika serikali ya CCM
itaondoka na hata mkiiba kura, lazima mtaondoka tu, tunawaandalia
wapinzani,” alisema Dk. Kitima kisha ukumbi mzima ukamshangilia kwa
nguvu.
Dk. Kitima ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema Rais Jakaya
Kikwete anao mawaziri watatu tu ambao wana mrengo chanya wa kuikomboa
nchi.
Alibainisha kuwa kitendo cha serikali kuruhusu wawekezaji kuingia
nchini na kudharau wazawa na mali zao hilo litakiangusha chama tawala.
Alisema kwa sasa katika vikao vya Bunge, hoja za msingi zinapingwa
huku mtoa hoja akizomewa, lakini mambo ya kipuuzi ndiyo yanayoshabikiwa
na wabunge wengi.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven
Masatu Wasira, amewashukia watumishi wote wanaojihusisha na ubadhirifu
wa mali za nchi na kusema lazima watu hao wahenyeshwe kwa kuchukuliwa
hatua bila kuonewa aibu.
Wasira ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi, alianza kwa kusema: “Mimi
nachukizwa sana na wanaoiba mali za nchi. Sipendi wizi na siwezi kuiba
wala simung’unyi maneno kusema hili.”
Alisema wapo baadhi ya watumishi wanapoingia kwenye ajira kazi yao ni
kuanza kuiba badala ya kujenga taifa, jambo ambalo ni hatari kwa
maendeleo ya nchi, na kwamba fedha za EPA zilizorudishwa na wezi na
zimetumika kuinua kilimo.
Waziri Wasira alisema kupungua kwa uadilifu hapa nchini ni tatizo
kubwa, na linaweza kuleta mgogoro mkubwa na kudidimiza zaidi uchumi wa
nchi, hivyo lazima kila Mtanzania awe muumini mzuri wa uzalendo.
“Rasilimali zote za nchi lazima zitumike kuwanufaisha Watanzania wote. Na bila hivyo hakuna nchi.
“Kupungua kwa uzalendo na uadilifu ni tatizo kubwa sana kwa nchi.
Lazima tuenzi amani na upendo...ukishindwa kulinda na kuiheshimu
Tanzania wakati na wewe ni Mtanzania hufai,” alisema Wasira.
Alisema rasilimali zote yakiwemo madini, maziwa, utalii na nyinginezo
nyingi ni vema zikageuzwa kuwa mali zinazonufaisha na kuleta maendeleo
kwa wananchi na kwamba dira ya maendeleo ya taifa ni kuboresha fursa
nyingi za kiuchumi.
Alisema ili kufikia malengo halisi, mpango wa serikali uliopo sasa ni
kuboresha huduma za viwanda, reli, viwanja vya ndege, kilimo bora,
bandari, maliasili, miundombinu na nishati.
Kuhusu udini, Wasira alisema wamemeishi miaka 50 kwa amani, upendo na
utulivu lakini sasa kuna chokochoko za baadhi ya watu ambao hawataki
kuiona nchi ikitulia.
0 comments:
Post a Comment