OFISI ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo imeeleza Dira yake kuu hapa nchini ni kuwa na uchumi endelevu unaokuwa kwa kiwango kikubwa na usimaizi mzuri wa fedha na uwajibikaji katika kupambana na umasikini.
 

Hayo yameelezwa leo na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.

 

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee alishiriki pamoja na viongozi na watendaji mbali mbali wa Wizara hiyo.

 

Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame alisema kuwa dhamira ya Ofisi hiyo katika kufikia Dira hiyo ni kuwa na taasisi bora yenye kuwezesha ukuaji haraka wa uchumi.

 

Pia ukuaji wa  Sera bora za ukusanyaji mapato na utaalamu kupitia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano na hivyo kusaidia utendaji wa shughuli mbali mbali za uchumi na jamii, usimamizi wa fedha za umma na maendeleo vijijini.

 

Ili kufikia Dira na dhamira hiyo, Ofisi hiyo ilieleza kuwa inaendelea kutekeleza majukumu ya kimsingi ambayo hayajabadilika na yameendelea kutekelezwa ambapo miongoni mwao ni pamoja na kuandaa na kusikamia mipango mikuu ya maendeleo ya Serikali na kuratibu utekelezaji wake kupitia sekta mbali mbali nchini.

 

Aidha, Uongozi huo wa Wizara hiyo ulieleza mafanikio iliyoyapata ikiwa ni pamoja na ukuaji mzuri wa uchumi uliofikia asilimia 10 kutokana na mwenendo mzuri wa sekta ndogo ndogo za utalii, usafirishaji na mawasiliano, biashara na uvuvi.

 

Pamoja na hayo, ukusanyaji mzuri wa mapato kwa kuvuka lengo ambapo Wizara kupitia taasisi zake za ukusanyaji mapato iliweza kukusanya vizuri mapato yake.

 

Wizara hiyo pia, ilieleza mafanikio iliyoyapata katika kuendesha kwa mafanikio zoezi la sensa ya watu na makaazi hapa Zanzibar pamoja na kuanza kwa mradi wa majaribio wa kuwasajili katika Mfuko wa Hifadhi ya jamii wanachama wanaojiajiri wenyewe kwa upande wa Unguja wakiwemo wajasiriamali.

 

Kwa upande wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), uongozi huo ulieleza kuwa tayari mkandarasi ameshaanza ujenzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto, Kariakoo na na tayari kwa upande wa pembea wameshatia saini kwa kiwanja hicho hapa Unguja na kueleza kuwa pembea nyengine zitapelekwa kiwanja cha Tibirinzi Pemba ambako ujenzi wa kiwanja hicho nao unatarajiwa kuanza si muda mrefu.

 

Mbali na mafanikio hayo, Wizara ilieleza changamoto inazozikabili ambapo miongoni mwao ni pamoja na athari za kushuka kwa uchumi wa dunia, Pia, Wizara ilieleza kuwa bado kuna upungufu katika uwajibikaji wa hiyari kwa walipa kodi walio wengi hapa nchini.

 

 Nae, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa upande wake alitoa  shukurani na pongezi kwa Wizara hiyo kwa jinsi ilivyowasilisha utekelezaji wa shughuli zake za kawaida na za maendeleo kwa ustadi mkubwa.

 

Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mashirikiano makubwa yaliopo katika Ofisi hiyo hatua ambayo imepelekea kupata mafanikio makubwa hali ambayo imejionesha katika uwasilishaji wa utekelezaji huo.

 

Alieleza kuwa juhudi zinazochukuliwa na uongozi pamoja na watendaji wa Wizara hiyo matunda yake yamekwua yakionekana huku akiusisitiza uongozi huo kuendelea kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa pamoja na kuwepo kwa mashirikiano na Wizara nyengine kwani nazo zinahitaji msaada mkubwa kutoka Wizara hiyo.

 

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Wizara hiyo mafanikio makubwa yameweza kupatikanwa katika ukusanyaji wa mapato na kuweza kusaidia katika ulipaji wa pencheni na hata kuwawekea mazingira mazuri wastaafu.

 

Alisema kuwa hatua hiyo imeweza kuwatia moyo hata washirika wa maendeleo ambao wameendelea kuiunga mkono Zanzibar na kuisaidia kwa kadri ya uwezo wao katika uimarishaji wa miradi mbali mbali wa maendeleo kutokana na juhudi zake hizo.

 

Mikutano ya kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kipindi cha Aprili-Juni 2011-2012 na Julai-Septemba 2012-2013, chini ya mwenyekiti wake Dk. Shein imemaliza leo ambapo Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango wa maendeleo ndio iliyofunga dimba.