Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetofautiana na Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, katika pendekezo
la kutaka muundo wa serikali tatu katika rasimu ya Katiba iliyotolewa
hivi karibuni.
Katika kupingana na maoni ya tume ya Jaji Warioba, Kamati Kuu (CC)
ya Halmashauri Kuu ya CCM, imeamua kupeka rasimu hiyo kwa wananchi wake
kuanzia ngazi ya matawi na kutaka yaundwe mabaraza ya Katiba ya chama
hicho ili kujadili rasimu hiyo hususani muundo wa Serikali ya Muungano.
Wakati CC ikipitisha azimio hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Warioba, amesisitiza kuwa suala la serikali tatu kwa
sasa haliepukiki kwani zisipokuwapo kuna hatari ya muungano kuvunjika.
Kauli ya Warioba imekuja huku kukiwa na mbinyo wa ndani na nje ya
CCM, wakiwamo viongozi waandamizi wa chama hicho tawala na makundi ya
urais 2015, kupinga pendekezo la kutaka kuwe na muundo wa serikali
tatu.
Habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa CC kutoka visiwani Zanzibar,
waliliambia gazeti hili kuwa wajumbe wa Zanzibar walicharuka na kuhoji
kwanini Jaji Warioba aliamua kuingiza pendekezo hilo kwenye rasimu ya
Katiba wakati msimamo wa chama anaujua.
Wajumbe hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walimshambulia
Warioba kuwa si kweli kwamba Wazanzibari wengi walioulizwa kuhusu
muundo wa serikali walipendekeza serikali tatu.
Katika kikao hicho mahususi kwa ajili ya kujadili rasimu ya Katiba
kilichofanyika jana chini ya Rais Jakaya Kikwete, Kamati Kuu (CC) ya
CCM imeazimia kuipeleka rasimu hiyo kwa wanachama wao kuanzia ngazi ya
matawi ili ijadiliwe kwenye mabaraza ya Katiba ya chama kwa kuzingatia
maoni yaliyopelekwa awali kwenye tume ya Jaji Warioba.
Hatua ya CC kushindwa kutoa msimamo na kuamua kuipeleka rasimu hiyo
kwenye matawi yake imeongeza hofu ya CCM kuhusu muundo wa serikali tatu
zilizopendekezwa na tume wakati chama hicho tangu awali msimamo wake ni
muundo wa serikali mbili kama ilivyo sasa.
Tayari baadhi ya vigogo waandamizi wa chama hicho akiwamo Waziri wa
Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, wamepinga
kipengele hicho cha rasimu kinachopendekeza serikali tatu.
Hofu ya Sitta na wenzake wanaopinga ni kwamba mchakato wake umelenga kuvuruga muungano na kuibebesha mzigo serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Katibu wa
Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kauli na
misimamo ya kina Sitta ni maoni yao binafsi na kwamba wana haki ya
kufanya hivyo kama Watanzania wengine.
Alisema msimamo wa chama utatolewa baada ya rasimu hiyo kujadiliwa na
wanachama wao kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa ambapo katika ngazi ya
taifa itajadiliwa na vyombo vikuu vya uamuzi vya Sekretarieti, Kamati
Kuu na NEC.
Nape alifafanua kuwa wanachama watakachoamua ndicho
kitakachochukuliwa na kupelekwa kwenye tume ya Jaji Warioba kama msimamo
wa CCM.
“Kamati Kuu imekiagiza chama kijipange kujadili rasimu hiyo ndani ya
chama kama baraza la kitaasisi la Katiba na kuwataka wanachama na
wapenzi wa CCM wajitokeze kwa wingi na kushiriki kwenye mabaraza,”
alisema.
Aliongeza kuwa jumuiya za chama za Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa
Wanawake (UWT) na Wazazi zimekusudia kushiriki kama mabaraza ya Katiba,
hivyo kuongeza ushiriki wa wanachama na wapenzi wa CCM katika mchakato
huo.
“CCM kama baraza la Katiba la kitaasisi litapitia rasimu
iliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kwa kuzingatia maoni ya chama
yaliyotolewa mwanzoni kabisa mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba,
wanachama wenu watashiriki kutoa maoni yao,” alisema.
Nape aliongeza kuwa pamoja na kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
CC inaiomba tume hiyo kueleza vizuri mchakato mzima kutoka rasimu ya
kwanza mpaka rasimu ya mwisho ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu
ya mchakato mzima hasa baada ya rasimu ya kwanza kutoka.
Alipoulizwa ni kwanini CCM inapata kigugumizi kutoa msimamo kuhusu
rasimu hiyo kama walivyokwisha kufanya vyama vingine, Nape alisema wao
hawakurupuki pasipo kuwashirikisha wanachama wao.
“Hiki ni chama kikongwe, haiwezekani kila kiongozi kutoa msimamo wake
bila utaratibu. Sisi lazima tuoneshe mfano, si umesikia CUF Mwenyekiti
wao, Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif,
wanapingana kuhusu muungano,” alisema.
Jaji Warioba apigilia msumari
Wakati pendekezo la kutaka kuwe na serikali tatu limewagawa
Watanzania, Jaji Warioba amesisitiza kuwa bila serikali tatu muungano
utavunjika.
Jaji Warioba aliyasema hayo juzi usiku wakati alipokuwa akizungumza
katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa hewani na kituo cha
televisheni cha ITV, huku akionesha dhahiri kujibu maoni ya vigogo kama
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta na wadau
mbalimbali, waliolalamikia muundo wa serikali tatu wakidai kwamba ni
gharama kuuendesha.
“Huwezi kung’ang’ania gharama, ulazimishe kwa sababu watu wanaogopa
gharama, kuna hatari ya muungano kuvunjika, ni lazima uangalie watu
wanataka nini na ndicho ambacho tumefanya kwamba kama tukilazimisha
serikali mbili, kuna hatari ya muungano kuvunjika.
“Zanzibar wanataka madaraka yao, uchumi wao waumiliki wao wenyewe na
ndiyo mabadiliko waliyokuwa wanataka. Bara wanasema kama Zanzibar
wanataka hayo itakuwa imekuwa huru, utawafanya nini, huwezi kufanya
mabadiliko? Kwahiyo mimi naona ukifanya hivyo hatari ya kuvunjika ni
kubwa zaidi, sasa uone kama unataka muungano gharama zitakuwapo kwani
hata tulipoanza gharama zilikuwapo.
“Sasa tumefika hapa tunasema ni afadhali tuwe na serikali tatu
lakini tujitahidi kupunguza matumizi. Tunavyoona ni afadhali tuwe na
serikali tatu…mi nitakuwa mnyonge sana muungano ukiwa dhaifu,” alisema
Jaji Warioba.
Alieleza kwamba ikiwa wananchi wanataka kukwepa gharama muungano
uvunjwe, lakini ikiwa wanautaka ni bora gharama ziwepo na kusisitiza
kwamba aonavyo yeye ni muhimu zaidi nchi hizo kuwa pamoja kuliko
vinginevyo, kwani hali hiyo inasaidia kupunguza gharama kuliko nchi
hizo zikiachana, kwani gharama zitakuwa kubwa.
Alisema katika kukusanya maoni yao wamepata mambo mengi muhimu ambayo
pengine hata wananchi hawayazungumzi, akatolea mfano suala la maadili
ya viongozi.
“Tulipopita tulisikia watu wakisema kuhusu maadili, matatizo mengi
yapo hata ya wananchi kutokuwa na imani. Walizungumza wakitaka hatua
zichukuliwe.
“Na matatizo mengine yanayotokea ni kwa sababu ya maadili ya viongozi kuporomoka,” alisema Jaji Warioba.
Muundo wa serikali tatu kukopa
Kuhusu suala hilo Jaji Warioba alisema atakayekuwa na jukumu la kukopa kwenye muundo huo ni Serikali ya Muungano.
Alisema hata serikali hizo mbili zikija zitaweza kukopa kwani hata hivi sasa utaratibu huo upo.
“Lakini hata sasa hivi kuna utaratibu kuwa serikali zote wanakopa
lakini serikali zote zitakuwa na nafasi yake kwenye kukopa,” alisema
Jaji Warioba.
Kuhusu mpaka wa mkopo kwa nchi, mwenyekiti wa tume hiyo ya Mabadiliko
ya Katiba alisema inategemea na serikali yenyewe kwani hata hivi sasa
utaratibu huo upo na ikiwa serikali ya Zanzibar inataka kukopa
hudhaminiwa na Serikali ya Muungano.
Kukwepa kutaja Serikali ya Tanganyika
Kuhusu kukwepa kusema Serikali ya Tanganyika, Jaji Warioba alisema
walikuwa wanatengeneza Katiba ya Muungano ambayo inafahamika kuwa ni
Tanzania Bara na Zanzibar.
Alieleza kuwa kwa Katiba ijayo ikiwa suala hilo litawekwa, Zanzibar
wanaweza kuchagua majina yao bila kuingiliwa, kwani halikuwa jukumu lao
kuwachagulia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, ikiwa Tanzania Bara watakapotunga katiba
yao watataka jina libaki Tanganyika, itakuwa juu yao, lakini kwa Katiba
ya sasa inahusu Tanzania Bara na Zanzibar.
Bunge la Katiba Novemba
Kuhusu Bunge la Katiba, Warioba alisema litakaa baada ya tume yake
kukamilisha rasimu ya pili ya Katiba ambayo itatokana na mapendekezo
ya wananchi.
Alisema wanatarajia kuikamilisha kazi hiyo mwishoni mwa Septemba mwaka huu.
“Mawazo yao yatarudi kwetu na tutaangalia kama kuna umuhimu wa
kubadili popote au kuacha kama ilivyokuwa ili kutengeneza rasimu ya
mwisho.
“Utaratibu wa kisheria ambao umewekwa tunatakiwa tumalize kazi yetu
mwisho wa Oktoba ili Novemba Bunge la Katiba likutane,” alisema Jaji
Warioba.
Alieleza matarajio ni kwamba mwishoni mwa Septemba watakuwa
wamekamilisha rasimu ya pili ambayo pia wataitangaza na baada ya mwezi
mmoja, Bunge la Katiba litakutana.
Pamoja na mambo mengine alisema iwapo katika mapendekezo ya wadau
wataona kuna jambo zito wanaweza kuliingiza watafanya hivyo lakini
mpaka waliridhie kwamba suala hilo ni bora zaidi.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, sheria inaelekeza kwamba baada ya
kuiandaa rasimu waitangaze kwenye gazeti la serikali na umma kisha
iende kuzungumzwa na wananchi kwenye mabaraza yao pamoja na makundi
mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment