Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema akiwa na Askofu
Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Kardinali Pengo wakiingia katika ukumbi wa
mkutano wakati wa kikao cha Mashauriano kati ya Jeshi la Polisi na viongozi wa
makanisa ya kikatoliki uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini , IGP Said Mwema akizungumza
katika kikao cha Mashauriano kati ya Jeshi la Polisi na viongozi wa makanisa ya
kikatoliki.kikao hicho pia kilihudhuriwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki
nchini Kardinali Pengo .Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi
Imeelezwa
kuwa Viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika jamii ya kupunguza
uhalifu kwa kuwa wao wanauwezo wa kuwabadili watu kimatendo na kifikra kwa kufanya doria ya mwili na roho kwa pamoja hivyo wanaweza kusaidiana na Polisi katika kupunguza uhalifu.
Hayo
yalisemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema wakati
alipokuwa akizungumza katika mkutano wa mashauriano baina ya Jeshi la
Polisi na Viongozi wa dhehebu la Romani Katoliki uliofanyika jijini Dar
es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Askofu Mkuu wa
Jimbo kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinali Pengo.
Mwema
alisema katika kipindi hiki viongozi wa dini pamoja na Jeshi la Polisi
wanatakiwa kula njama ya kupambana na uhalifu kwa kuhakikisha kuwa
wahalifu wote wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria na
Viongozi wa dini wanatakiwa watumie nafasi walizonazo katika kuhakikisha
kuwa waumini wao wanajua mbinu za kujilinda na kuhakikisha taifa
linakuwa salama.
Aidha
amewataka kutumia takwimu za uhalifiu zinazotolewa na Jeshi la Polisi
katika kazi zao za kila siku ili kuhakikisha kuwa wale wahalifu wote
wanaacha kutenda vitendo hivyo na wanarejea katika nyumba za ibada na
kuwa watu wema.
Kwa
upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam
Mwadhama Kardinal Pengo amesema viongozi wa dini hawawezi kukwepa jukumu
lao la kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua hapa nchini kwa kuwa jukumu
hilo linaanzia kwao.
Pengo
alisema kuongezeka kwa uhalifu ni changamoto kwa viongozi wa dini kwa
kuwa wao ndio wenye kazi ya kujenga maadili katika jamii na polisi
kusimamia sheria na kuwachukulia hatua wale wanaokaidi
Akisoma
maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho Askofu Msaidizi wa Kanisa
Katoliki Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Mhashimu Eusebius Nzigilwa alisema
wamekubaliana kuziimarisha kamati za ulinzi na usalama katika nyumba za
ibada zilizopo hivi sasa wakati wakiendelea kupata mafunzo ya ukamataji
salama kutoka Jeshi la Polisi.
“Parokia
ambazo hazijaunda kamati za ulinzi na usalama zihakikishe zinafanya
hivyo ndani ya mwezi huu na zile ambazo zimeundwa lakini hazifanyi kazi
mziimarishe ili kwa pamoja tuwe salama katika nyumba zetu za
ibada”Alisema Askofu Nzigilwa.
Picha na Frank
Geofray-Jeshi la Polisi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment