TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA
KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA NA VIONGOZI WA MADEREVA
WA BODABODA MJINI DODOMA
11/06/2013
Zangu Viongozi, Wawakilishi wa madereva wa Bodaboda na
viongozi wengine mliopo hapa.
Kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutupa
afya kuweza kukutana hapa leo.
Pili niwashukuru kwa kuitikia wito na kukubali kuja ili
msikilize ninachotaka tuzungumze ili wote tutoe maoni ili tuweze kuboresha
zaidi utendaji wa kazi zetu za kila siku na kukabiliana na ajali
zinazotuandama.
Kama mtakumbuka hiki ni kikao changu cha pili baina yangu nanyi.
Kikao cha kwanza tulifanya tarehe 27/03/2013 na agenda zetu zilikuwa ni:-
1.
Kufahamiana na kujenga mtandao wa mashirikiano
ili kuzuia uhalifu na ajali za barabarani.
2.
Kujadili mazingira ya kazi yenu
3.
Utii wa Sheria Bila Shuruti.
Baada
ya majadiliano ya mada hizo baadhi yenu mliuliza maswali na kutoa maoni
mbalimbali.
Kikao
cha leo lengo lake ni kutaka tujadiliane pamoja tatizo linalotukabili hasa
ninyi waendesha Bodaboda la AJALI ZA BARABARANI na lingine tutazungumzia nama
ya kuendesha shughuli zenu kwa usalama zaidi kwa kushirikiana na Polisi na
wadau wengine.
Ajali
za barabarani zipo ambazo kwa namna yoyote ile zinapotokea, watu wanasema
haiepukiki. Mfano, dereva amepatwa na ugonjwa wa ghafla na kushindwa kumudu
chombo cha moto anachoendesha, kikakosa uelekeo na kupinduka ama kikagonga mtu
au chombo kingine cha moto au watu walio pembezoni mwa barabara.
Nyingine
inaweza ikawa chombo cha moto kimepata hitilafu katika mfumo wa umeme na
ukasababisha ajali ikatokea, mifano inaweza kuwa zaidi ya hiyo.
Lakini
ajali nyingi kulingana na utafiti uliofanyika asilimia 72 (72%) zinasababishwa
na binadamu mwenyewe (aidha madereva au watumiaji wengine wa barabara).
Sababu zinazochangia ajali nyingi
kutokea ambazo zinasababishwa na binadamu mwenyewe ni kama ifuatavyo:-
1.
Kutokuzingatia sheria za usalama barabarani.
2.
Mwendo kasi (hapo ndipo penye balaa).
3.
Kutokuzingatia alama za barabarani.
4.
Ulevi wa pombe na madawa ya kulevya.
5.
Dharau n.k.
Sababu
hizo hapo juu ndizo zinazochangia ajali zote zinazotokea sehemu mbalimbali na
hapa kwetu Dodoma kwa upande wa waendesha bodaboda.
Mfano
hapa kwetu Dodoma kuanzia Januari hadi Juni 7/2013 ajali arobaini na nane (48)
zilizohusisha bodaboda zimekwishatokea. Kati ya ajali hizo, zilizosababisha
vifo ni kumi na saba (17) na waliokufa ni watu kumi na tisa (19).
Zilizosababisha majeruhi ni ajali thelathini na moja (31) na waliojeruhiwa ni
arobaini na saba (47). Katika ajali hizo zote arobaini na nane (48),
zilizosababishwa na madereva wa bodaboda ni arobaini na mbili (42).
Ajali
hizi kama madereva hawa wangekuwa makini na kufuata sheria na kuepuka yale
niliyotaja hapo juu ambayo yanasababisha ajali, vifo hivi na majeruhi hawa,
hatungekuwa tumekaa hapa tukizungumzia leo.
Mtu
akisikia watu kumi na tisa (19) wamefariki kwa upeo wa kibinadamu anaweza kuona
ni idadi ndogo lakini siyo hivyo ni kubwa sana tukizingatia zimesababishwa na
uzembe na zimepunguza nguvu kazi ya taifa na kuwaacha wategemezi wengi na shida
zaidi ya walizokuwanazo wakati walipokuwa na mtegemezi wao ambaye watakuwa
wamempoteza kwa ajali.
Niwaombe
nguvu ambazo huwa mnatumia na ushirikiano mnaoonyesha kwa misururu ya pikipiki
mnapomsindikiza mwenzenu aliyekufa kwa
ajali maana hao kumi na tisa (19) waliofariki miongoni mwao waendesha bodaboda
wapo kumi na moja (11) mzitumie pia kuonyana nyinyi kwa nyinyi kuepuka mwendo
kasi maana ndiyo unawaua zaidi. Kufuatia sheria na alama za barabarani na
pale ambapo hakuna alama ujue ni nani umpe kipaumbele cha kupita kwanza (mfano
sehemu ambayo haina taa za barabarani au alama yoyote unayotakiwa umpe nafasi
aliye kulia kwako nafasi ya kupita kwanza).
Nguvu
hizo na ushirikiano huo utumieni kukaa vikao vya kuonyana ili mjiepushe na
ajali ambazo zinaepukika.
Jambo
lingine napenda niwaombe muendelee kuimarisha vikundi vya Ulinzi Shirikishi
vilivyopo na kuanzisha vingine ili kuzuia uhalifu usitokee dhidi yenu na katika
maeneo yenu. Lipo tatizo pia la baadhi yenu kukaa kwenye vituo au kufanya
biashara ya kubeba abiria hadi saa nane hata tisa usiku. Jambo hilo ni hatari
kwa maisha yenu, onyaneni ili kuacha mtindo huu. Sisi Polisi tutaanza kuchukua
hatua zinazostahili kadri sheria inavyotuelekeza.
Nisisitize
tena kwenu tuzingatie UTII WA SHERIA BILA SHURUTI.
Fanya
shughuli zako kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na hakuna
atakayekubughudhi na itakusaidia kuepuka ajali zisizotarajiwa.
Pia
naomba kila mmoja atambue kuwa Usalama unaanza na WEWE MWENYEWE, MIMI MWENYEWE
NA SISI SOTE.
DAVID
.A. MISIME - ACP
KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA
POLISI MKOA WA DODOMA
DAWATI LA HABARI, ELIMU NA MAHUSIANO,
Phone:
0715 006523, Luppy Kung’alo – Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP)
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment