Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa
masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu,
Mzee Timothy Apiyo kilichotokea usiku wa jana, Jumatatu, Juni 10, 2013, katika
Hospitali ya Millpark, Johannesburg, Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa
matibabu.
Rais Kikwete
amesema kuwa kifo cha Mzee Apiyo kimeinyang’anya taifa la Tanzania mmoja wa
watumishi wa umma hodari na wazalendo waliotumikia umma wa Watanzania kwa
uaminifu na uadilifu.
Katika salamu
zake kwa Balozi Ombeni Y. Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea
kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Mzee Timothy Apiyo ambacho
nimejulishwa kilitokea usiku wa jana katika Hospitali ya Millpark, Afrika
Kusini.”
“Kwa hakika
kifo cha Mzee Apiyo kimelinyang’anya taifa letu mmoja wa watumishi wa umma
hodari, wazalendo ambao walitumikia umma wa Tanzania kwa bidii, uaminifu na
uadilifu mkubwa,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika nafasi
zote ambazo alizishikilia katika utumishi wa umma ukiwamo Ukatibu Mkuu na
Ukatibu Mkuu Kiongozi, Mzee Apiyo alionyesha umakini wa kiwango cha juu
ulioongozwa na ushikiliaji wa kuigwa wa misingi ya utumishi wa umma.”
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Kwa hakika, Mzee Apiyo ataendelea kuenziwa kama mfano wa kuigwa wa
utumishi uliotukuka wa umma.”
“Kutokana na
kifo hiki, nakutumia wewe Katibu Mkuu Kiongozi salamu zangu za rambirambi na
kupitia kwako kwa familia nzima ya Mzee Apiyo ambao wameondokewa na Baba, Babu
na Mhimili wa familia. Napenda kukujulisha kuwa niko nawe na familia nzima ya
Mzee Apiyo katika kuomboleza msiba huo. Naelewa machungu yenu katika kipindi
hiki kigumu. Nawaombea huruma ya Mwenyezi Mungu muwe na subira ya kuweza
kuwavusha kipindi hiki. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu
aiweka peponi roho ya Marehemu Timothy Apiyo. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
11 Juni, 2013
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment