MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo
inatarajia kutoa uamuzi wa kumpa au kutompa dhamana Mkurugenzi wa Ulinzi
na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred
Lwakatare na Ludovick Joseph wanaokabiliwa na kosa la kula njama kutaka
kumuua kwa sumu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msaki.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Alocye
Katemana, baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ponsian Lukosi,
kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuwa imekuja kwa ajili ya
kutajwa.
Hakimu Katemana alisema uamuzi wa dhamana ya Lwakatare na mshirika
wake, itatolewa leo baada ya kupitia maombi ya dhamana yaliyowasilishwa
na mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatara na Abdalah Safari Mei 13,
mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, wakati hakimu huyo
alipokuwa likizo.
Katika maombi hayo ya dhamana yaliyowasilishwa Mei 13, mawakili wa
Lwakatare walidai kuwa kosa la kula njama linadhaminika kwa mujibu wa
sheria.
Hata hivyo Wakili wa Serikali, Prudence alililipinga ombi hilo kwa
madai kuwa shauri hilo lipo hatua za uchunguzi, kilichopo mahakamani ni
jalada la tuhuma zinazowakabili washitakiwa ambazo zipo katika hatua za
uchunguzi na kwamba tuhuma hizo mwisho wa siku zitafunguliwa kesi rasmi
Mahakama Kuu, kwani ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza, hivyo mahakama
hiyo haiwezi kutoa dhamana kwa kesi ambayo haipo.
“Na kwa mazingira ya shauri linalomkabili Lwakatare hapa Mahakama ya
Kisutu, lipo katika hatua za uchunguzi na bado DPP hajafungua kesi
rasmi Mahakama Kuu, sasa tunashangaa mawakili wa washitakiwa
wanawasilisha ombi la dhamana leo hii katika mahakama hii wakati maamuzi
ya Mahakama ya Rufaa yapo na bado hayajatenguliwa,” alisema.
Machi 20 mwaka huu, Lwakatare na wenzake walifunguliwa rasmi kesi Na.
6/2013 ya tuhuma za ugaidi ambapo kosa la pili, tatu, na la nne
yalikuwa hayana dhamana, hivyo Mei 8 mwaka huu, Jaji Kaduri aliyafuta
makosa hayo kwa maelezo kuwa hajaona kama kuna maelezo ya kutosha ya
kuwafungulia mashitaka ya ugaidi.
0 comments:
Post a Comment