SAKATA la muwekezaji wa kampuni moja ya madini kudaiwa kutumia kemikali Katika kuyeyushia mawe ili kupata madini ya dhahabu kisha kutiririsha maji mtoni limechukua sura mpya baada ya wanakijiji kuagiza serikali ya kijiji chao kumzuia muwekezaji huyo asiendelee na kazi Katika eneo la kijiji chao.

Barua aliyoandikiwa muwekezaji huyo na Afisa Mtendaji wa kijiji cha Katuma inamzuia muwekezaji huyo aliyetambulika kwa jina la LUKMAK MINING (T) LTD ya jijini Mwanza asiendelee na kazi hadi atakapoweka wazi kazi zake ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nyaraka zinazotakiwa Katika ofisi yake.

Katika barua hiyo yenye kumb Na. MDC/KTM/ VC 28/ 1/64 (nakala tunayo) afisa mtendaji aliitaka kampuni hiyo kusimamisha shughuli zote Katika eneo hilo hadi atakapokamilisha kutekeleza ushauri wa kitaalamu kutoka ofisi ya madini kanda ya Magharibi mjini Mpanda pamoja na kuweka wazi shughuli zake.

Kamera ya Mtandao huu lilifika Katika eneo la uwekezaji la kampuni ya Lukmak Mining (T) Ltd Katika kijiji cha Katuma kilometa moja kutoka sekondari ya Katuma na kuwakuta wafanyakazi watano wakiendelea na kazi ambapo walieleza kuwa wanalipwa mshahara wa shilingi elfu nane kwa wiki na kampuni hiyo na kuwa bosi wao aliondoka wiki mbili zilizopita kwenda jijini Mwanza

Wakifafanua namna wanavyotumia kemikali Katika eneo hilo walisema huku wakionesha matanki kuwa yamejengwa matanki kumi na sita yenye ujazo wa lita elfu kumi na tano za maji, wakishajaza maji humwagia humo mawe yaliyotoka kwenye mashimo ya madini ambayo wanayaita kwa jina la Kanyero ambapo humwagia humo kemikali ya kuyeyushia

Licha ya kuomba kuhifadhiwa majina yao kwa usalama wa ajira zao walisema baada ya kuyeyuka na kubaki uji mchemko huo huo hupitishwa Katika mambomba matatu yanayotoka Katika kila tanki na kuelekea kwenye maabara ambayo imejengwa kwa bondeni ambako hutenganishwa madini ya dhahabu na tope la takataka yenye kemikali ambalo humwagiwa Katika mashimo yaliyoko nje ya maabara hiyo

Katika eneo hilo kuna mwinuko ambao hutiririsha maji Katika mto Katuma na hilo ndo linaloibua hofu kwa wanakijiji ambao ni watumiaji wakubwa wa maji ya mto Katuma kwa shughuli za binadamu na wanyama hoja ambazo ziliibuliwa na wananchi Katika mkutano wa hadhara wa jumuiya ya watuamiaji wa maji ya bonde dogo la mto Katuma uliofanyika Julai 28, 2013 katika ofisi ya Kata ya Katuma mchana

Wanajumuiya hao ambao ni wanakijiji wote walilalamikia namna serikali inavyosita kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kumzuia kabisa muwekezaji huyo kufanya kazi zake Katika eneo la kijiji chao na kuwa Baraza la Mazingira la Taifa NEMC kufika kijijini hapo ili kujionea hali halisi kwa lengo la kuepusha madhara yanayoweza kuwakumba wanakijiji hao.

Akizungumza na mtandao huu, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka ofisi ya Bonde la mto Katuma, Thadeusi Ndeseiyo, alisema kumbu kumbu za ofisi yake zinaonesha kampuni hiyo ya Lukmak (T) Ltd haina kibali cha Wizara ya Maji cha kutumia maji ya mto Katuma kwa shughuli zake kinyume cha utaratibu uliopo ambapo makampuni yote yanayotumia maji Katika shughuli zake hutakiwa kulipia maji hayo Wizarani na kupewa kibali cha kutumia maji. 
Chanzo: Sumiablog














TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top