Matokeo ya kwanza ya utafiti juu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umeonyesha kwamba jumuiya hiyo iliundwa kama chombo kilichoandaliwa kuwepo kwa maslahi ya serikali na wafanyabiashara wakubwa.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wataalam la Afrika Mashariki (VEAF),lililofanya utafiti huo imebaini pamoja na mambo mengine kwamba mpaka sasa mwenendo wa ushirikiano huo ni kutoka juu kwa watawala kwenda chini huku raia wengi wa kawaida wakiwa hawana taarifa juu yake, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki linaripoti.
Theluthi moja ya watu kama wa Tanzania na Kenya hawajahi kusikia juu ya mtangamano wa EAC ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Dr Azaveli Lwaitama.
Jumuiya hiyo yenye wananchama watano ingawa ilianzishwa upya kuwa ‘’jumuiya yenye misingi ya watu’’ wenyewe wa Afrika Mashariki, imebainika ushiriki wa raia wa kawaida katika mchakato wa mtagamano huo ni mdogo mno. Wanachama wa EAC ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.
Taarifa hiyo imedokeza kuwa na malengo ya kuboresha uelewa wa raia juu ya mwenendo mzima wa ushirikiano kwa kushughulikia hofu za wananchi wa pande zote za nchi husika, ndipo awamu hii ya pili ya kihistoria ya kurejesha upya jumuiya hiyo inaweza kufanikiwa.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ilizinduliwa upya mwaka 1999 baada ya jumuiya ya kwanza kuvunjika mwaka 1977 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo tofauti za kisiasa na kiuchumi miongoni mwa wanachama watatu wa awali wa jumuiya hiyo, Kenya, Uganda na Tanzania.
Ripoti kamili ya utafiti huo ilitaraji kuzinduliwa rasmi na Rais Mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam .

0 comments:
Post a Comment