SIKU mbili baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, kuwapandisha kizimbani askari wake wawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara kwa tuhuma za wizi wa risasi, siri nzito imefichuliwa.

Juzi askari, Michael Leus (55), Sajenti wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) katika kituo cha Polisi cha Musoma na Ally Majembe Koplo wa kituo cha polisi wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani walifikishwa kizimbani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Mwendesha mashkata, Jonathan Kaijage mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ngikwama alidai kuwa askari hao walikutwa na risasi 1556 za SMG na Shortgun.

Kosa jingine walilokutwa nalo ni wizi wakiwa kazini ambapo walikana mashtaka hayo yote mahakamani hapo.

Hata hivyo kwa mujibu wa chanzo chetu, inadaiwa kuwa mtandao huo wa askari ni mkubwa na kwamba silaha hizo na risasi zinazoibiwa zinasafirishwa hadi mpakani mwa Kenya na Tanzania na kuuzwa kwa wapiganaji wa kundi la waasi la Al-Shabab la nchini Somalia.

Kundi la Al-Shabab limekuwa tishio nchini Somalia kwa matukio ya mashambulizi ya kuuwa watu na kufikia hatua ya kuvuka mpaka hadi Kenya, hatua iliyoilazimu nchi hiyo kupeleka jeshi lake Somalia kupambana na kundi hilo.

Wakizungumza kwa simu na Tanzania Daima Jumatano kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini ili kulinda ajira zao, watoa siri hao walisema kuwa biashara hiyo haramu waliyoifananisha na uasi ndani ya jeshi hilo iliripotiwa mapema lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Hii biashara inawahusisha watu wazito maana tangu imeripotiwa hakuna hatua zilizochukuliwa na wahusika wamekuwa wakiendelea kuvusha silaha hizo hadi walipokuja kunaswa baadhi yao.

“Hali sasa ni tete kwa wale waliotoa siri hiyo kwani mtandao huo umeanza kuwapa vitisho vya kuwaua ili wasije kufichua mpango mzima wa ushahidi dhidi yao,” walisema.

Hata hivyo, watoa taarifa hao walitilia shaka kuwa huenda wakubwa wao wanafahamu mpango mzima na hivyo kumuomba Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP), Saidi Mwema, kuunda tume ya kuchunguza kashfa hiyo na kuliepusha taifa lisivamiwe na maadui.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, kulitolea ufafanuzi suala hilo, alikataa kata kata akisema liko mahakamani na hivyo haruhusiwi kulizungumzia.

Alipoulizwa kama ana taarifa za vitisho vya baadhi ya askari wake waliofichua siri hiyo, Kamanda Mwakyoma alisema waripoti malalamiko hayo polisi ili yafanyiwe uchunguzi.

Katika kesi inayowakabiri askari wawili kwa tuhuma za kuiba risasi na silaha, mwendesha mashtaka aliielezea mahakama hiyo kuwa walikutwa na risasi hizo katika upekuzi wa ndani ya basi la Mohamed Trans usiku wa Juni mosi mwaka huu. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 24.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top