Muungano wa vyama vitatu vya siasa nchini NCCR-Mageuzi, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) umeandaa
maandamano makubwa ya kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.
Mswada huo
ulipitishwa na Bunge Mjini Dodoma hivi karibuni lakini wabunge wa vyama hivyo,
walisimama bungeni na kupinga usipitishwe wakidai unatakiwa kufanyiwa
marekebisho.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa
CHADEMA, Bw. Bw. John Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema maandamano
hayo ni haki yao ya msingi.
Alisema
maandamano hayo yamepangwa kufanyika Oktoba 10 mwaka huu yakianzia Dar es Salaam na
kuendelea katika mikoa mbalimbali nchini ili kupeleka ujumbe kwa wananchi.
“Hatutarudi
nyuma na msimamo huu wa kufanya maandamano labda serikali iseme Rais Jakaya
Kikwete hatasaini mswada huu kwani kuna kauli zinazoashiria tusiyafanye bali
tujadiliane.
“Kama yakizuiwa kwa kigezo cha kutii amri bila shuruti
hatuwezi kukubali, tutayafanya kwa sababu kila tunapoomba maandamano
tunakatazwa,”alisema Bw. Mnyika.
Aliongeza kuwa, kamati za ufundi za vyama
hivyo, tayari zimeanza kutoa maelekezo mikoani na kuiomba Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, ijitokeze na kuelezea vifungu vyenye kasoro ambavyo wanavipigia kelele
ili vibadilishwe.
“Waziri
wa Katiba na Sheria, Bw. Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Uhusiano na Uratibu, Bw. Steven Wassira na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, Bi. Sophia Simba waache kumtisha Rais Kikwete na wananchi.
“Chikawe anaposema kama rais hatasaini mswada
huo anaweza kuingia katika mgogoro na hatimaye Bunge kuvunjika si ya kweli bali
ni kuwapotosha wananchi, kama wana hofu
wajiuzulu na kupisha watu wengine kushika nafasi zao,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi na Mawasiliano wa
CUF, Bw. Abdul Kambaya, alisema hadi sasa Serikali ya Muungano na ile ya
Mapinduzi Zanzibar, zinatambua kama kweli
mswada huo haujakamilika kutokana na kasoro zilizopo.
Majira lilipozungumza
na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova ili
kujua kama maandamano hayo yamepata kibali alisema, hadi jana hakuwa amepata
taarifa na wakizipata, watachunguza madai yao na kuangalia hoja zao kama wana
jipya.
0 comments:
Post a Comment