MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu kwenda
jela miezi sita au kulipa faini ya sh 1,000, raia wa Kenya, Joshua
Mulundi, ambaye alikuwa akikabiliwa na kosa la kutoa taarifa za uongo.
Mulundi alidaiwa kutoa taarifa za uongo kwa ofisa wa polisi katika
Kituo cha Polisi Oystebay jijini Dar es Salaam, kwamba yeye na wenzake
walikodiwa kwenda kumteka na kumjeruhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Alocye Katemana, akisema
kuwa kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya upande wa Jamhuri kumsomea
maelezo ya awali mshitakiwa huyo.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, alimsomea maelezo ya
awali mshitakiwa na baada ya kumaliza, mshitakiwa huyo alikiri kutenda
kosa hilo kinyume cha kifungu cha 122 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya
mwaka 2002.
Kabla ya Hakimu Katemana kutoa adhabu yake aliutaka upande wa Jamhuri
uzungumze lolote kama wanalo, ambapo Wakili Kweka alidai kuwa anaiomba
mahakama itoe adhabu inayostahili.
Kwamba, kwa mazingira ya kesi hiyo, hali iliyojengeka katika jamii
kuhusu sakata la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka ni tete na kuwa si
vema kwa mtu mzima kama huyo kutoa taarifa za uongo polisi.
Aidha, kwa upande wake Mulundi, alieleza kuwa yeye ni raia wa Kenya na
kwamba lengo na madhumuni ya kuja Tanzania ni kuja kufanya biashara ya
kuuza nguo.
Alidai kuwa Juni 27, mwaka jana akiwa Arusha, alitekwa na mtu
asiyemfahamu na kumwamuru afanye kila jambo atakalomtaka, kwamba yeye
alikubali kufanya yote aliyoamriwa na mtu huyo ambaye alikuwa na silaha.
“Mheshimiwa hakimu kwa kuwa nilikuwa naogopa vitisho hivyo nilifanya
kama alivyokuwa akinielekeza na baadaye mtu huyo aliyekuwa ameniteka
akanipeleka hadi Tanga sehemu ambayo sikuwa nimewahi kufika.
“Akanieleza kuwa yeye ni Mkristo na kwamba ananituma kwa Mkristo
mwenzie na akanipa taarifa hizo nizipeleke kwa Mkristo mwenzake na
taarifa hizo ndizo zilizosomwa hapa mahakamani na mwendesha mashitaka
wakati akinisomea maelezo ya awali,” alisema.
Alidai kuwa alikwenda hadi katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo
Kawe, Tanganyika Parkers na kumkuta Mchungaji Joseph Kiliba ambaye yule
mtekaji alimwagiza amfikishie taarifa hizo.
Mulundi aliongeza kuwa alimpelekea taarifa zile mchungaji kama
alivyoelekezwa lakini baada ya hapo alijikuta anakamatwa na kupelekwa
Kituo cha Polisi Oystebay, ambako alirudia taarifa ile na kisha
kufunguliwa mashitaka.
Akitoa adhabu yake baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili,
Hakimu Katema alisema kwa kuwa mshitakiwa amekiri kosa kabla hata
mashahidi wa Jamhuri hawajaletwa kutoa ushahidi wa kesi hiyo, mahakama
yake inamhukumu kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya sh 1,000.
Hata hivyo mwandishi wa habari wa Radio Times, Chipangula Nandule, aliyekuwapo mahakamani hapo alijitolea kumlipia faini hiyo.
Lakini sekunde chache baadaye askari polisi walimkamata Mulundi,
wakidai ni raia wa Kenya, hivyo wanamshikilia ili waweze kuandaa
taratibu za kumrejesha nchini kwao.
Agosti 6, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), alimfutia Mulundi kesi ya kujaribu kumuua na kumteka Dk. Ulimboka.
0 comments:
Post a Comment