Kamanada wa Polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman
MWANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Katenga, wilayani Mbarali,
Hans Mbogo (17), kidato cha tatu, amekutwa amefariki dunia na mwili
wake kutupwa kichakani katika Kitongoji cha Itange, Kijiji cha Madabaga
wilayani Mbarali.
Tukio hilo lilitokea Agosti 19 mwaka huu katika kijiji hicho na
taarifa za awali zinaeleza kuwa mwanafunzi huyo aliuawa na watu wasio
julikana na mwili wake kutelekezwa katika vichaka hivyo.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya Polisi mkoani hapa, zinaeleza
kuwa Agosti 19, majira ya saa 12 jioni, mwanafunzi huyo akiwa nyumbani
kwake na pipipiki (bodaboda) yake aina ya T-Better, yenye namba za
usajili T263 BZC, alikodishwa na watu wasiojulikana na kumtaka
awapeleke katika kijiji jirani.
Taarifa zinaeleza kuwa baada ya kukodishwa na watu hao ambao
inasadikiwa ni majambazi, hakurudi nyumbani na mwili wake ulikutwa siku
ya pili, Agosti 20, mwaka huu vichakani ukiwa na matundu yanayohisiwa
kuwa ni ya risasi.
Kamanada wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athuman, alisema mwili wa
marehemu umefanyiwa uchunguzi na umeshakabidhiwa kwa ndugu, tayari kwa
mazishi.
Alisema jeshi lake bado linawasaka wahusika na kuwataka wenye taarifa
zozote kuhusiana na mauaji hayo wazitoe kwenye mamlaka husika.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment