Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu wakuu kumi na mmoja na naibu makatibu wakuu 14 wapya katika wizara mbalimbali.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Katibu Mtendaji wa
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Sifuni Mchome ambaye sasa
anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na aliyekuwa
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deodatus Mtasiwa ambaye anakuwa Naibu
Katibu Mkuu, Tamisemi.
Mtasiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni walisimamishwa kazi na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda Februari, mwaka jana kupisha uchunguzi dhidi yao, kutokana
na kukithiri kwa migomo ya madaktari nchini, pamoja na utendaji wao
kulalamikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu
Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema: “Mtasiwa ameteuliwa kwa kuwa
uchunguzi dhidi yake haujaonyesha kuwa ana kosa lolote, lakini wenzake
(Nyoni) na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David
Jairo bado wanachunguzwa.
Katika uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu, Peniel Lyimo amehamishiwa Ikulu kusimamia Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN), kuwa Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha
na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo.
Makatibu wakuu walioachwa kwa maelezo kuwa
watapangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda (aliyekuwa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Kijakazi Mtengwa (Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto) na Omary Chambo (Uchukuzi), huku aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick
Rutabanzibwa akistaafu wa hiari.
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete ameanzisha
kitengo kipya katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), kitakachokuwa
kikishughulikia afya ambacho kitasimamiwa na Dk Mtasiwa.
Aidha, aliwataja makatibu wakuu waliohamishwa
wizara kuwa ni Florens Turuka kutoka Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia
kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Joyce Mapunjo kutoka Viwanda na Biashara
kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Makatibu wakuu wapya
Alisema Jumanne Sagini ambaye alikuwa Naibu Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa
wizara hiyo.
Dk Servacius Likwelile ambaye alikuwa Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo. Dk
Patrick Makungu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa
wizara hiyo.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Tamisemi), Alfayo Kidata ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Dk Shaaban Mwinjaka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Viwanda na Biashara ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.
Uledi Mussa ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara
na Masoko.
Charles Pallangyo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Waziri Mkuu sasa anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya. Aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna
Maembe ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Sihaba Nkinga ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa
wizara hiyo na Sophia Kaduma ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara
hiyo.
Naibu makatibu wakuu wapya
Naibu makatibu wakuu wapya wizara zao katika
mabano ni Angelina Madete (Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira), Regina
Kikuli (Ofisi ya Waziri Mkuu), Zuberi Samataba (Ofisi ya Waziri
Mkuu-Tamisemi anayeshughulika na Elimu), Edwin Kiliba (Ofisi ya Waziri
Mkuu-Tamisemi), Dk Yamungu Kayandabila (Kilimo, Chakula na Ushirika),
Profesa Adolf Mkenda (Fedha-Sera), Dorothy Mwanyika (Fedha-Fedha za Nje
na Madeni), Rose Shelukindo (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk
Selassie Mayunga (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Monica
Mwamunyange (Uchukuzi).
Consolata Mgimba (Elimu na Mafunzo ya Ufundi),
Profesa Elisante ole Laizer (Habari, Utamaduni na Michezo) na Armantius
Msole (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Waliohamishwa
Naibu makatibu wakuu waliohamishwa ni John Mngodo
(Uchukuzi kwenda Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Selestine Gesimba
(Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwenda Wizara ya Maliasili na
Utalii).
Injinia Ngosi Mwihava (Ofisi ya Makamu wa Rais
kwenda Wizara ya Nishati na Madini), Maria Bilia (Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kwenda Viwanda na Biashara na Nuru Milao (Maliasili
na Utalii kwenda Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto).
Aidha, Dk Donaldo Mbando amethibitishwa kuwa
Mganga Mkuu wa Serikali baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu kusimamishwa
kwa Dk Mtasiwa.
Via Mwananchi
0 comments:
Post a Comment