Zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba Septemba mwaka huu, wamefaulu.
Matokeo hayo yalitangazwa jana na Kaimu Katibu
Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde
aliyesema ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 19.89 ikilinganishwa na
mwaka jana.
Alisema jumla ya watahiniwa 844,938 walifanya
mtihani huo na kati yao 427,606 sawa na asilimia 50.61, wamefaulu kwa
zaidi ya alama 100 kati ya 250.
Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa hao
waliofaulu, wasichana ni 208,227 sawa na asilimia 46.68 na wavulana ni
219,379 sawa na asilimia 55.01.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa, wanafunzi wengi
wamefanya vibaya zaidi kwenye somo la Hisabati huku wakifanya vizuri
kwenye somo la Kiswahili.
Dk Msonde alisema wavulana wamefanya vizuri zaidi kwenye mtihani huo ukilinganisha na wasichana.
Alieleza pia kuwa, mwaka huu udanganyifu kwenye mtihani huo umeshuka kwa kiasi kikubwa, kwani waliofutiwa matokeo ni 13.
Dk Msonde alisema kati ya hao, watano walibainika
kukariri mtihani huo jambo ambalo kisheria hawaruhusiwi na wengine
walikamatwa na karatasi za majibu kwenye vyumba vya mtihani.
Ufaulu
Alisema miongoni mwa waliofaulu, wenye ulemavu ni
476, kati yao wasichana wakiwa ni 219 sawa na asilimia 46.01 na wavulana
ni 257 sawa na asilimia 53.99.
Dk Msonge alisema kuwa, mwaka 2012 watahiniwa
waliopata zaidi ya alama 100 walikuwa ni asilimia 30.72, hivyo mwaka huu
kuna ongezeko la asilimia 19.89.
Kuhusu sababu za ongezeko la ufaulu, Dk Msonde alisema baraza bado halijafanya tathmini ya kubaini chanzo cha ongezeko hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Sisi tulicholetewa ni kile kilichofanyika kwenye chumba cha mtihani na haya hapa ndiyo majibu yake,” alisema Dk Msonde.
Ufaulu kimasomo
Alisema mwaka huu ufaulu kwa masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya sita mpaka 28.06, ikilinganishwa na mwaka 2012.
Somo ambalo watahiniwa wengi wamefanya vizuri ni
Kiswahili ambalo ufaulu wake umefikia asilimia 69.62 na walilofeli zaidi
ni Hisabati ambalo ufaulu wake ni asilimia 28.62.
Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2012 ufaulu kwenye
somo la Kiswahili ulikuwa ni asilimia 41.00 na Hisabati ulikuwa ni
asilimia 18.74.
Kwenye somo la Kiingereza ufaulu mwaka huu ni
asilimia 35.52 wakati mwaka jana ilikuwa ni asilimia 21.06, huku kwa
Sayansi mwaka huu ufaulu ukiwa ni asilimia 47.49 na mwaka jana ilikuwa
ni asilimia 41.48 na Maarifa ya Jamii mwaka huu ufaulu ni asilimia 53 na
mwaka jana ilikuwa asilimia 28.61.
Usahihishaji wa mashine ni bora zaidi
Alisema ili kujiridhisha na usahihishaji wa
kutumia Mashine Maalumu za OMR (Optical Mark Reader), sampuli 20,795 za
karatasi za majibu ya watahiniwa wa shule 200 kutoka wilaya 48 za mikoa
tisa ya Iringa, Kagera, Shinyanga, Manyara, Njombe, Mbeya, Morogoro,
Katavi na Tanga zilisahihishwa kwa mkono.
Alisema baada ya kufanya ulinganifu wa usahihi wa
karatasi zilizosahihishwa kwa mkono na zile zilizosahihishwa kwa
mashine, ilibainika kuwa zile zilizosahihishwa kwa mashine zilikuwa na
usahihi wa hali ya juu.
“Usahihishaji wa kutumia kalamu ulikuwa na makosa
machache ya kibinadamu, makosa hayo yalikuwa ya kukosea kusahihisha
swali kwa kutumia mwongozo wa usahihishaji na dosari za kujumlisha
alama,” alisema Dk Msonde.
Alibainisha kuwa, kati ya sampuli za karatasi za
watahiniwa 20,795 zilizosahihishwa kwa mkono, 249 sawa na asilimia 1.2
ndizo zilizobainika kuwa na makosa aliyosema ni ya kibinadamu.
Mbali na usahihi wa usahihishaji, alisema pia
mfumo huo umesaidia kupunguza wasahihishaji kutoka 4,000 waliokuwa
wakitumika awali na kufikia 301 waliofanya shughuli hiyo mwaka huu.
Alibainisha pia kuwa, OMR imepunguza siku za kusahihisha mtihani huo kutoka 30 za awali mpaka 16 zilizotumika mwaka huu.
Waliofanya mtihani
Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani
huo walikuwa ni 867,982 wakiwamo wasichana 455,896 sawa na asilimia
52.52 na wavulana 412,087 sawa na asilimia 47.48.
Alieleza kuwa, kati ya watahiniwa hao walikuwemo wenye ulemavu wa kuona, 597 walikuwa na uono hafifu na wengine 88 ni wasioona.
“Watahiniwa 844,938 sawa na asilimia 97.34 ya
waliosajiliwa walifanya mtihani huo. Wasichana walikuwa 446,115 sawa na
asilimia 99.85 na wavulana walikuwa 398,823 sawa na asilimia 96.78,”
alisema Dk Msonde.
Alisema kuwa, watahiniwa ambao walisajiliwa na
hawakufanya mtihani huo ni 23,045 sawa na asilimia 2.66, kati yao
wasichana wakiwa 9,781 sawa na asilimia 2.15 na wavulana 13,264 sawa na
asilimia 3.22.
Alieleza kuwa utoro na ugonjwa ni miongoni mwa sababu za wanafunzi hao kutofanya mtihani huo.
Lengo la BRN halijafikiwa
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa akizungumza katika warsha ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
(BRN-Big Results Now), kwenye sekta ya elimu iliyotolewa kwa watendaji
wa elimu ngazi ya kanda, mkoa na wilaya, Agosti 14, mwaka huu, alisema
moja ya lengo la mpango huo ni ufaulu kwa darasa la saba mwaka huu
kufikia asilimia 60 kutoka 31 ya mwaka jana.
“Katika kutekeleza vipaumbele hivyo, kila mmoja
wenu atakuwa na eneo la kutekeleza na atapimwa kutokana na utekelezaji
katika eneo lake, hii ni katika kuhakikisha kuwa kuanzia mwaka huu
ufaulu katika elimu ya msingi unaongezeka kutoka asilimia 31 hadi
kufikia 60,” alisema Dk Kawambwa.
Mara baada ya Dk Kawambwa kutangaza suala hilo,
baadhi ya wadau walisema itaongeza hali ya kupata matokeo yasiyo halisi
kwani hakukuwa na muda wa kuandaa mikakati ya kufikia lengo hilo, kwani
mpango huo ulitangazwa Agosti na Septemba watoto wa darasa la saba
walikuwa wanaanza mitihani.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment