Siku moja baada ya wabunge kuwataka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kujiuzulu kwa kushindwa
kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili, pembe 706 za ndovu zimekamatwa
jijini Dar es Salaam.
Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa
katika hifadhi za wanyama pori mbalimbali hapa nchini. Tukio hilo
lililotokea jana jioni katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani
Kinondoni, liliongozwa na Waziri Kagasheki ambaye aliambatana na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarish Maimuna.
Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe za ndovu ni
raia watatu wa China ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote
kutoka mji wa Guandung .
Raia hao wa China wamekuwa wakiishi katika nyumba
hiyo kwa miaka mingi wakifanya biashara ya kuingiza nchini vitunguu
swaumu kutoka China na kusafirisha nje ya nchi makombe yanayopatikana
baharini.
Alipoingia ndani ya nyumba hiyo, Kagasheki ambaye
aliambatana na askari polisi na baadhi ya maofisa usalama alishuhudia
shehena kubwa ya pembe za ndovu ikiwa imehifadhiwa kwenye viroba vyenye
uzito wa kilo 50.
Mbali ya kushuhudia shehena ya pembe hizo,
alionyeshwa gari maalumu aina ya Toyota Noah ambalo watuhumiwa hao
hulitumia kutoa pembe porini na kuziingiza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo la tukio mara baada ya
kuwakamata alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na matokeo ya
Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo imesitishwa na Serikali juzi baada
ya wabunge kuilalamikia.
Waziri Kagasheki alisema kwamba katika harakati za
kutaka kuwakamata watuhumiwa hao walitoa Sh30 milioni kwa ajili ya
kujaribu kuwahonga askari.
“Walitaka kuwahonga askari ili wasikamatwe,” alisema huku akionyesha noti za fedha hizo.
Alisema wabunge wanaomtaka ajiuzulu kwa madai
kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya watu na
mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya
Kikwete pekee.
“Sasa mimi nasema kunitoa haitakuwa rahisi anayeweza kunitoa ni yule aliyeniweka,” alisema.
Alisema ipo mikakati inayofanywa na baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Itakuwa ni jambo la ajabu kwamba kila mtu akiingia madarakani
wanataka atoke, watatolewa wangapi?” alihoji na kuongeza kuwa operesheni
hiyo ni muhimu kwa ajili ya kunusuru tembo wasiishe.
Alisema kwamba ni kweli kuna baadhi ya dosari
zimejitokeza kwenye operesheni ikiwamo kuuawa kwa baadhi ya mifugo,
lakini siyo kwamba zoezi zima halina manufaa.
Kagasheki alisema kama kasi hii ya kuuawa kwa tembo itaachiwa iendelee baada ya miaka 10 tembo wote watakuwa wameisha nchini.
Alisema hataki kuona utawala wa Rais Kikwete ukiondoka madarakani ukiwa na lawama ya kuachia majangili wawamalize tembo.
Mmoja wa watuhumiwa hao, Huang Qin alisema shehena
yote ya pembe za ndovu iliyokamatwa nyumbani kwake ilikuwa ikiletwa
kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina.
Akiongea kwa Kiswahili Qin alisema: “Mimi hii si yangu, kichwa yangu mbovu. Rafiki yangu alileta hii (pembe) kidogo kidogo.”
Januari mwaka huu, Gazeti La Daily Mail la
Uingereza liliripoti kwamba Serikali ya Kenya imekamata shehena ya
vipande 638 vya pembe za ndovu ambavyo ni sawa tembo 320 waliouawa.
Mzigo huo wa tani mbili ulikuwa kwenye kontena la mawe ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa tani nne za pembe
za ndovu zenye thamani ya Dola za Marekani 3.4 milioni sawa na takriban
Sh5.4 bilioni zilikamatwa Hong Kong Oktoba 20, mwaka jana, huku
ikielezwa kuwa meno hayo yalikamatwa yakisafirishwa kutoka Kenya na
Tanzania.
Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa
Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam
akiwa na pembe za ndovu yenye thamani ya Sh18.4 milioni
yaliyotengenezwa kama bangili tayari kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment