BAADHI yetu tumeamua kugomea kampuni za simu kama ishara ya kupinga kodi ya laini za simu na ongezeko la gharama za simu hususan kwenye matumizi ya intaneti.

Bila ya shaka utakuwa umesikia kuwa kuanzia Julai 1 serikali – na magenius wake – wameamua kuweka kodi ya sh 1,000 kwa kila laini ya simu ambayo mtu anayo kwenye simu yake; kodi ambayo italipwa kila mwezi.

Magenius wetu hawa wakiongozwa na Andrew Chenge walikuja na mapendekezo ya kodi hii wakiamini kuwa kwa vile Watanzania wengi wana simu za mkononi na kwa vile wengi wanatumia sim card zaidi ya moja basi kodi hata ndogo kiasi gani italeta mapato makubwa sana kwa serikali.

Katika mawazo yao ni kama watu walioamua – baada ya kunywa kidogo au wakiwa timamu – kuwa wakiamua kumchangia mtu mmoja sh 100 tu basi watakuwa wamemsaidia huyo mtu. Kwamba sh 100 ni hela ndogo sana kiasi kwamba kuitoa hata mtu hawezi kusikia maumivu yake. Hoja ni kuwa “shilingi mia moja itanunua nini?” Sasa hii inaweza kuwa kweli kama mtu hatofikiria sana; watu 100,000 wakiamua kumchangia mtu mmoja sh 100 kila mmoja mtu huyo atakuwa na sh milioni 10! Sasa sh 1,000 kwa kila laini ya simu ni rahisi sana kupuuzia lakini tukiangalia kwa karibu tutaona tatizo la msingi.

Ni kodi ya kijinga
Serikali ina kodi nyingi mno; kodi za kila namna na kwa vitu vingi sana. Kuna kodi kwenye mishahara, kwenye bidhaa, huduma, n.k. Kodi nyingi zinaeleweka na zinakubalika (hata kama ni kubwa mno) na serikali imekuwa ikibadilisha badilisha viwango vya kodi mbalimbali na wakati mwingine kufuta kodi fulani au kuleta kodi nyingine.

Serikali inapoamua kufuta kodi inakuwa na sababu zinazoweza kueleweka na inapoleta kodi nyingine mantiki yake lazima ionekane. Kodi hii ya laini za simu ni miongoni mwa kodi ambazo siamini kama zimefikiriwa vya kutosha.

Ni kodi ya kijinga – na ujinga hapa si tusi ni hali tu ya kutokujua – kwa sababu moja kubwa; wakati mataifa makubwa yaliyoendelea yanahitajidi kufanya gharama za teknolojia ya mawasiliano kuwa ndogo sisi tunajaribu kufanya iwe kubwa.

Wakati wenzetu wanajaribu kuhakikisha kuwa watu wao wanapata mawasiliano ya simu na huduma ya intaneti kwa bei ya chini inayowezekana sisi tunajaribu kufanya vitu kuwa vigumu zaidi.

Na huu ndio ujinga ambao unatulazimisha sisi wengine kupinga hii kodi pamoja ongezeko la kodi ya huduma ya simu ambayo imefikia asilimia 14.5.

Ni kodi mbaya vile vile kwa sababu inamlipisha mtu kwa kuwa na kitu ambacho tayari ameshakilipia na huduma yake ameishailipia. Fikiria kwa mfano unaponunua gari unalipia bei ya gari na ushuru wake wote unaotakiwa kulipia.

Sasa itakuwaje kama magenius wetu serikalini wakiamua kuwa kwa vile yapo magari mengine (ishara ya maendeleo kama alivyosema Kikwete) basi magari yaanze kutozwa kodi ya sh 10,000 kwa mwezi kwa kutumia barabara. Kwamba fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya maendeleo.

Sasa hoja hiyo ni rahisi kuiona na inavutia, lakini ukiangalia ni kodi ya kuwa na gari. Watu wenye simu wameshalipia ununuzi wa simu, wamelipia huduma ya simu, bado watalipia huduma ya intaneti (na kodi yake juu) na walishalipia kununua laini za simu na sasa wanatakiwa kulipia kuwa nazo.

Tatizo la Tanzania sio kukosa mapato. Hapa naweza kuzua mjadala. Siamini kuwa tatizo la nchi yetu ni kukosa vyanzo vya mapato kiasi cha kuanza kutoza kodi vitu ambavyo kimsingi vilitakiwa visiwe na kodi na vingine vingeweza kuwa vya bure kabisa kutokana na umuhimu wake.

Ukisikiliza maneno ya wanaohalalisha kodi hii unaweza kabisa kushawishika kwanini watu wasikubali tu kulipa.

Hoja yao kubwa ni kuwa watu wanalia wanataka huduma na huduma zinahitaji fedha na fedha zinatokana na kodi, hivyo watu wanaotaka huduma wasilalamike serikali inapowatoza kodi.

Sasa tatizo la Tanzania ni zaidi ya kutokuwa na kodi za kutosha; na pia ni zaidi ya kusema watu wengi hawalipi kodi (yote mawili si kweli). Lipo suala zima la uzalishaji. Je, tunazalisha vya kutosha kiasi cha kuwa na vyanzo vingi zaidi vya mapato?

Je, uwezo wetu wa kiuchumi umetumia fursa zote zinazowezekana kusababisha uzalishaji wa huduma na bidhaa nchini? Ukikaa chini kufikiria uwezo wetu wa kiuchumi, Tanzania haijafikia hata asilimia 10 ya uwezo wake wote.

Fikiria tu kwa haraka kama yote yanayofanyika nchini yanatokana na umeme unaopatikana kwa watu asilimia kama 15 hivi. Ni wazi kuwa nishati ikipatikana kwa watu wengi zaidi na ya kuaminika uzalishaji wa vitu mbalimbali nao utaongezeka.

Sasa, kama watawala wetu katika ugenius wao hapa ndipo walipofikia, kwa kweli siwezi kushangaa na siku moja wakikosa mapato zaidi wataanza na kodi ya mbuzi na sungura alimradi watoze kitu fulani kodi. Kwani wakulima wengi wanalipa kodi? Kwanini wasilazimishwe na wao kulipa kodi kwa kuuza ng’ombe mmoja kila mwezi!?

Lakini pia ni zaidi ya suala la uzalishaji, ni suala la matumizi. Tuna watu wanatumia fedha zetu vibaya, wametuingiza kwenye mikataba mibovu; wametengeneza mifumo mibaya ya utawala halafu wakiishiwa wanakuja tena na kusema tunataka fedha zaidi.

Yaani, wanatumia fedha vibaya – na mifano ipo mingi sana – halafu hali ngumu wanasema ‘tuwatoze tena kodi’! Na wapo watu kati yetu ambao hawaoni tatizo kabisa ati kwa vile serikali imesema inahitaji kodi!

Rafiki yangu mmoja juzi baada ya hili jambo kuibuka aliniuliza: “Kama watu wana uwezo kwanini wasilipe tu hii kodi mbona si nyingi?”

Jibu langu ni hili, kama wapo wenye uwezo na wanapenda kuichangia serikali si tu sh 1,000 watu hao wajiandikishe kwa hazina ili wawe wanatoa michango yao huko.

Na kama wapo watumishi (wa umma au binafsi) ambao wanaamini hii ni hela ndogo na hawajli sana kuchangia sh 1,000 kila mwezi, basi hawa nao waandikishwe ili wakatwe kwenye mishahara yao fedha zaidi ili wachangie hazina kutoka katika moyo wao.

Kama tukiwaacha waendelee kulipana posho za ajabu ajabu, kama tukiwaacha waendelee kutoa misamaha ya kodi kubwa sana (ambayo zingeliingizia taifa mara zaidi kadhaa ya fedha za laini za simu) na kama tukiwaacha waendelee kutengenezeana ulaji mwingine (si juzi juzi wameanzisha kitengo cha chini ya rais cha kupima maendeleo ya miradi mbalimbali nchini!?) kwanini basi tusiwaache waendelee kutoza kodi mbalimbali na hata hizi za kijinga?

Pamoja na hili ni kuwa serikali yetu imeishiwa ubunifu. Leo hii wanatoza huduma za intaneti kodi ya asilimia 14.5 kwa ajili ya watu kutumia intaneti na makampuni ya simu yanapitisha gharama hii kwa wateja na hivyo kupandisha gharama ya vifurushi vya intaneti inabidi kujiuliza hivi ni nani aliyekuwa anawaza vitu hivi?

Tanzania ni nchi maskini; na ujio wa teknolojia kama hizi za simu na intaneti unatakiwa utiwe moyo ili watu wengi zaidi waweze kuzitumia na hivyo kurahisisha maisha yao.

Sasa sisi badala ya kuhakikisha tunaondoa vikwazo vya watu kufikia (access) teknolojia hii magenius wetu wanajiona wao mabepari kweli wanaamua kupandisha kodi!

Na tena wanapandisha kodi ile ile kwa kila mtu! Mashirika ya umma hayana tatizo si zipo fedha za umma kulipia? Watu binafsi matajiri hawana matatizo wao watalipia tu; lakini watu maskini ambao ndio intaneti inaanza kuwafikia tena kwa njia ya simu – si kompyuta hawa kweli wataitumia teknolojia hii? Si kwamba tunafanya gharama za intaneti kuwa kubwa pasi ya sababu huku mtu huyo huyo bado analipia na simu na sasa analipia na kodi ya laini ya simu?

Hivi kuna ubaya gani kwa serikali kufuta – siyo kupunguza – kodi ya intaneti? Mtu tayari kanunua simu na amenunua huduma ya simu kwanini tusiweke mfumo mzuri wa kodi ambao utachochea watu kutumia teknolojia hii na watu kuwekeza ili kuifikisha kwa watu wengine?

Tena tunaweza kuuliza swali la kufikirisha kwanini tusifanye intaneti kuwa ni ya bure kwenye miji yetu na hata vijijini?

Teknolojia ipo, uwezo upo na hitaji lipo! Hivi hatufikirii kuwa tukifanya intaneti bure tutachochea biashara na uchumi kuliko tunavyofanya hivi? Ni sawasawa na kurejesha UDA mikononi mwa wananchi na kuifanya iwe kampuni ya huduma badala ya biashara, siyo kwamba watu wengi wataweza kwenda kazini mapema, kwenye huduma mbalimbali n.k si ndivyo wanavyofanya kwenye nchi za wenzetu au hawa watawala wanapoenda huko ng’ambo hawajifunzi wao wanaenda kufanya shopping tu na kung’aa macho?
Ni kwa sababu hiyo na nyingine nyingi sisi wengine tumeamua kuipinga kodi hii ya lainmi za simu na ongezeko la kodi ya intaneti.

Tunapinga kwa sababu kodi hii ni kandamizi na kwa kweli imekuja bila kuzingatia mahitaji na hali ya taifa kwenye suala hili. Ni kodi ya tamaa tu; ni kana kwamba wameona watu wenye simu ‘wanafaidi saaaaana’ sasa wameamua kuwakomoa!

Tumeamua kuwa kwa kadiri kodi hii itaendelea kuwepo basi na sisi tutaigomea na kuwanyima makampuni ya simu mapato ambayo yatazidi hii sh 1,000 kwa mwezi.

Kama watu watalazimika kulipa kodi hii basi watu watatumia nguvu yao ya fedha kunyima mapato kampuni na kushusha mapato ya serikali. Kwa kuamua kuzima simkadi hizi kwa hizi siku tatu watu watatuma ujumbe kuwa wamechoka kugeuzwa mbuzi; wanaswagwa tu popote!

Uzuri wa kugomea huku ni kuwa hakuna mtu anayeweza kukulazimisha kutumia laini ya simu yako. Hapa hakuna mabomu, hakuna polisi, wala hakuna mtu wa kumpiga mwingine. Serikali haiwezi kuja na kusema “tumieni laizi zenu za simu ili tupate mapato.”

Na hapa ndipo unapoona kuwa hii ni kodi ya hiari kabisa si ya lazima; kama hutaki kulipa hununui kadi. Na tena hili ndilo litakalotokea; watu itabidi wachague kuachilia laini nyingine na kubakiwa na moja na hivyo ile ndoto ya serikali kuwa watu watalipia laini mbili au tatu itakufa.

Tunagomea wazo, tunagomea mpango na tunagomea nadharia nzima ya kodi hii. Serikali kama inataka ipate mapato na kuwa haina watu wa kuwasaidia kufikiri tunawapa ushauri wa bure tu:

(a) Sitisha kupandisha mshahara na posho za wabunge na mawaziri na watendaji wote wa ngazi za juu wa vyombo vya umma kwa miaka miwili ijayo. Futa kodi zote za kikao kwa watumishi wote wa serikali na uone kama hutapa zaidi ya sh bilioni 300 kwa miezi iliyobakia (zaidi ya fedha zinazotarajiwa kukusanywa na laini za simu)
(b) Ziba matundu au inayoitwa "mianya ya kodi kama misamaha ya kodi n.k Haiwezekani huku wanataka kuwakamua Watanzania upande mwingine wanaachilia makampuni makubwa kukwepa kodi! Kama ni Lazima kwa mwanakijiji wa Nyamisa au Ileje kulipa kodi basi iwe ni lazima kwa watu wanaochuma nchini nao kulipa kodi.
(c) Ongeza uzalishaji ili uongeze mapato; ng'ombe unaweza kumkamua kwa kiasi kile tu unamlisha na anaweza kutoa maziwa. Huwezi kuendelea kumkamua wakati hali na humlishi. Maziwa yana kikomo chake mwisho utaanza kukamua damu! Huwezi kukazana kuongeza mapato bila kuongeza uzalishaji kwani mwisho wa siku kuna kikomo na hili ndilo limetokea, naamini.

(d) Bana matumizi - badala ya kung'ang'ania kuongeza mapato tu kutoka vyanzo vingine angalia unatumia zile fedha ambazo tayari unazo. Binafsi nilitarajia kusikia serikali inakuja na ‘some kind of austerity plan’ kama kuna tatizo la mapato na kama kuna ‘deficit’ kubwa kwenye bajeti yetu.

Hivi hawa wenzetu zile ripoti za CAG huwa wanasoma au wanapitia juu juu tu na kusubiri ya mwaka ujao? Huwezi kuwa na fedha kama utumiaji ni huu! Serikali badala ya kuja na kodi juu ya kodi ikae chini na kuja na mpango wa kubana matumizi.

Wao wamechora mstari; na sisi tuchore mstari... Julai 29, 30 na 31 mwanzo kukataa kugeuzwa mbuzi. Mbuzi akiona kisu anapiga kelele. Kama unataka kushiriki kwenye mgomo huu wa kimya fuata maelekezo haya na unaweza kumtumia mtu mwingine kwa SMS:
Siku 3 za Vitendo: Julai 29 tunagomea (Voda), Julai 30 (Airtel), Julai 31 (Tigo na laini nyingine zote). Tumia nguvu yako ya fedha kulazimisha mabadiliko ya sera. Chomoa SIM Card siku hizo kugomea kodi hiyo kwa mwezi kutumia line. Gomea Kodi ya SIM CARD: Huu ni mgomo wa mwanzo: Sambaza kwa angalau watu 10!!
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top