Waziri Mkuu, Mizengo pinda
HOFU ya kung’oka kwa mawaziri wasiopungua watano akiwamo Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, imeanza kushika kasi ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba, huenda safari hii usiwe upepo
unaopita tu bila madhara, bali kikawa kimbunga cha kuwaondoa madarakani
mawaziri hao kwa madai ya kushindwa kuwajibika.
Pinda na mawaziri wenzake, Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi),
Mathayo David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Khamis Kagasheki (Maliasili na
Utalii) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa)
wanashinikizwa kujiuzulu.
Mawaziri hao juzi walishambuliwa na wabunge kuwa taasisi na watendaji
walio chini yao wameendesha operesheni za kupambana na ujangili na
kuhamisha mifugo zilizosababisha vifo, ubakaji, majeruhi na uharibifu wa
mali kwa wananchi wasio na hatia.
Tayari Bunge limepitisha azimio la kuunda kamati teule ambayo
inatarajiwa kutangazwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, bungeni kesho.
Hatua ya kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kumekitia hofu Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambacho tangu mwaka 2008 kimekuwa kikihaha kutibu
majeraha ya makundi yanayohasimiana yanayodaiwa kushamiri mara baada ya
Edward Lowassa kujiuzulu.
Majina ya kamati teule yanayotarajia kutangazwa kesho, ndiyo yatakayotoa picha ya mwelekeo wa siasa za chama hicho.
Iwapo kamati teule ikibaini tuhuma walizotoa wabunge, za watu
kubakwa, kuuawa, kuteswa, ng’ombe kupigwa risasi, wafugaji kutozwa faini
kubwa, kulazimishwa kuuza mifugo yao kwa bei ndogo, Pinda na mawaziri
wenzake waliotajwa watalazimika kujiuzulu au rais kutengua uteuzi wao.
Wadadisi wa mambo ya siasa wanadokeza kuwa kuendelea kuwapo
madarakani kwa Pinda kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na Rais Jakaya
Kikwete, ambaye mara kwa mara amekuwa akimkingia kifua licha ya
kupelekewa malalamiko ya utendaji hafifu wa Pinda.
Baadhi ya makada waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili, wamedokeza
kuwa kitendo cha wabunge kuunda kamati teule ya kuchunguza migogoro ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hakitamnusuru Pinda.
Makada hao wanasema Pinda hawezi kuepuka kimbunga hicho kwa madai
kuwa baadhi ya wabunge na hata mawaziri hawaridhishwi na utendaji wake,
hivyo matokeo ya tume hiyo yatatoa fursa ya azima yao ya siku nyingi ya
kutaka kumng’oa madarakani.
Rais Kikwete ndiye tegemeo pekee la kusalia madarakani kwa Pinda
anayedaiwa kushindwa kuimudu ofisi hiyo iliyoachwa na mtangulizi wake,
Lowassa, aliyejiuzulu Februari mwaka 2008, baada ya kuguswa na kashfa
ya Richmond.
Historia ya kamati inaonyesha kuwa ripoti zake mara nyingi
zimesababisha kujiuzulu au kuondolewa madarakani kwa watu wanaoguswa
nazo.
Mtangulizi wa Pinda ambaye ni Mbunge wa Monduli, Lowassa, alilazimika
kuondoka madarakani baada ya ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyokuwa
chini ya Dk. Harrison Mwakyembe, kubaini kulikuwa na upendeleo katika
zabuni iliyoipa ushindi Kampuni ya Richmond.
Pinda inadaiwa amekuwa si mtoaji maamuzi kwa masuala yanayowagusa
watendaji walio chini yake, hivyo kuathiri utendaji kazi wa serikali.
Kama Pinda atajiuzulu, Rais Kikwete atalazimika kuunda baraza jipya
la mawaziri ambalo litakuwa la nne tangu aingie madarakani mwaka 2005.
Rais Kikwete aliunda serikali mwaka 2006 mara baada ya kuingia
madarakani lakini Aprili 2008 alifanya mabadiliko baada ya Lowassa
kutuhumiwa na kamati teule iliyoundwa kuchunguza kashfa mbalimbali
zilizohusu kampuni za kuzalisha umeme.
Baada ya Uchaguzi Mkuu 2010 Rais Kikwete alifanya mabadiliko kwa
mara ya pili, baada ya kuchaguliwa tena kwa awamu ya pili, huku
waliokuwa mawaziri 2005-2010 wakiangushwa katika kinyang’aro cha ubunge
kwenye majimbo yao.
Kikwete alifanya mabadiliko mengine Mei mwaka jana, mabadiliko
yaliyomwacha aliyekuwa Waziri wa Fedha Mustapha Mukulo, aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, aliyekuwa Waziri wa
Maliasili na Utalii Ezekiel Maige, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na
Biashara, Cyril Chami, aliyekuwa Waziri wa Afya Dk. Haji Mponda na
aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Waziri mmoja wa zamani anasema wabunge watakaoteuliwa na Spika kuunda
kamati teule wanaweza kutumia mwanya wa makundi ya kisiasa kumwajibisha
Pinda na wenzake kwa lengo la kujiimarisha kwa ajili ya uchaguzi wa
rais mwaka 2015.
Historia za kamati teule
Historia inaonyesha kuwa kila kamati teule ilipoundwa haikuwaacha
salama watuhumiwa, ikiwa ushahidi utatolewa wa kutosha. Juzi Spika
Makinda aliafiki wazo la kuundwa kwa kamati teule.
Hata hivyo kamati teule hizo kila zinapoundwa na ripoti yake kusomwa
zimekuwa zikisababisha kuondoka madarakani kwa watendaji mbalimbali.
Februari 8, 2008, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu
baada ya kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza zabuni iliyoipa
ushindi wa kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond kumgusa.
Mwaka juzi, Bunge liliunda kamati teule kuchunguza matumizi ya Wizara
ya Nishati na Madini, ambayo ilidaiwa kuchangisha sh milioni 50 kwa
idara na taasisi zilizo chini ya wizara, ili kufanikisha upitishwaji wa
bajeti, na ripoti yake ilimng’oa Katibu wake, David Jairo.
Mvutano
Wakati hofu hiyo ikitanda Bunge limegawanyika katika suala hili,
kukiwapo mvutano mkubwa kama mawaziri hao wawajibishwe au la, licha ya
mawaziri hao kutoa kauli za serikali na kuomba radhi ili wahusika
waweze kuwajibishwa.
Tayari Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), amejitokeza na kusema
hoja yao imetekwa na Spika wa Bunge, Makinda, na kuifanya ni ya kwake na
si ya wabunge waliotoa hoja.
“Hoja imechukuliwa na Spika, akaanza kuamua baadhi ya mambo yaanze
kuchunguzwa na Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ambayo
imeteuliwa na yeye, tulitegemea tupewe fursa ya kuhitimisha hoja zetu
kisha iundwe kamati teule kutegemea hadidu za rejea za wabunge, lakini
kwa utaratibu uliofuatwa na Spika, watoa hoja hatujapewa nafasi ya
kuhitimisha hoja zetu,” alilalamika Lugola.
Lugola aliongeza kwamba damu zilizomwagika hazitaenda bure, watu
wakileta majibu mepesi yasiyowawajibisha Pinda na wenzake hatakubali,
maana wananchi wameuawa, wamebakwa, wameteswa, ng’ombe wakauawa kwa
kupigwa risasi, kama kuna mbunge asiyewapenda Watanzania apeleke
utetezi kwa masuala hayo mazito.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alisema kila chama kilichoko
madarakani kinapenda kutawala, hivyo mawaziri waliozembea iwapo
hawatachukuliwa hatua chama kinachoongoza kinajiandalia anguko katika
uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo baadhi ya wabunge wa chama tawala wanaona haikuwa busara
kwa Spika Makinda kuruhusu hoja ya kuundwa kwa kamati teule, hasa katika
kipindi hiki ambapo vyama vya upinzani vimeonekana kuimarika zaidi.
Kuimarika kwa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kumechangia makada wa CCM
kujawa na hofu ya kile kitakachogunduliwa na kamati teule.
Wabunge hao walisema hivi sasa bado chama chao hakijapata uungwaji
mkono katika mchakato wa sheria ya Katiba mpya, hivyo kamati teule
inaweza kuongeza utete ndani ya serikali na CCM
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment