MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi (61), amevamiwa na watu wasiojulikana na kujeruhiwa kwa mapanga sehemu za kichwani na usoni.

Dk. Mvungi ambaye ni mwanasheria maafuru nchini na mwanachama wa NCCR-Mageuzi, alivamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi saa 6:30 usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake Kibamba, Kata ya Mpiji Majohe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alikolazwa Dk. Mvungi kwa matibabu, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema watu hao kabla ya kuvunja milango ya nyumba walilipua kitu ambacho kilitoa moshi mwingi na cheche kisha kuingia ndani na kuanza kudai wapewe fedha.

Alisema kuwa hatua hiyo ilisababisha Dk. Mvungi kupambana nao bila mafanikio, ndipo wakamjeruhi vibaya kwa kumcharanga mapanga kichwani, usoni na kisha kuondoka na kompyuta mpakato (Laptop) yake, pisto na kiasi cha fedha ambacho hakijajulikana.

Mbatia alisema majirani na ndugu walifanikiwa kumbeba Dk. Mvungi na kumkimbiza katika Hospitali ya Tumbi mkoani Pwani ambako alipatiwa matibabu ya awali na kisha kuhamishiwa Muhimbili saa 10:00 alfajiri.

Alisema kuwa alipokelewa na kuingizwa katika wodi ya huduma ya dharura na ilipofika saa 4:16 asubuhi gazeti hili lilishuhudi Dk. Mvungi ambaye alikuwa hajitambui akitolewa kwenye chumba hicho na kuingizwa kwenye gari la wagonjwa lenye namba za usajili STK 8767.

Wakati huo, Dk. Mvungi alikuwa akipelekwa katika Hospitali ya Aghakan kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha siti scan kwa ajili ya kuona ameathiriwa vipi katika eneo la kichwa.

Mbatia aliongeza kuwa ndugu na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba walifikia uamuzi wa kumpeleka Dk. Mvungi akapimwe kipimo hicho Aghakan na kisha arejeshwe kwa sababu uongozi wa MOI uliwaeleza kuwa mtaalamu anayefahamu kutumia kipimo hicho hakuweza kupatikana mara moja.

Majira ya saa 5:58, Dk. Mvungi alirejeshwa MOI huku akiwa bado anavuja damu maeneo ya puani na kichwani na kisha akaingizwa tena katika chumba cha huduma ya dharura.

Baadaye saa nane mchana alihamishwa katika chumba hicho na kupelekwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

“Jamani Watanzania, Dk. Mvungi hali yake ni mbaya kama mlivyomuona, kwani tangu alivyopigwa jana saa sita usiku hadi sasa bado anavuja damu…tumeumizwa sana na kitendo hiki na tunaamini serikali inafanya kazi yake ya kubaini ni wakina nani wamefanya unyama huu,” alisema Mbatia.

Shuhuda wa tukio hilo, ambaye ni dereva wa Dk. Mvungi, alisema kuwa wahalifu hao walikuwa wakisema wanahitaji fedha ila walimpiga sana na mapanga na kwamba ndiye aliyembeba kumkimbiza Tumbi na baadaye Muhimbili.

Mke wa Dk. Mvungi, Anna Mvungi, alisema watu hao walipoingia ndani walitembeza mapanga huku wakimtaka asiwatazame usoni.

Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliofika kumjulia hali Dk. Mvungi ni pamoja na Prof. Paramaganda Kabudi, Joseph Butiku na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Prof. Costa Mahalu na wahadhiri wengine.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top