Alfred Tibaigana alipokuwa kazini siku chache kabla ya kustaafu
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Buganguzi
wilayani Muleba, Kamishna Tibaigana alisema suala la maandamano
halikumsumbua kwa kuwa alielewa kuwa sheria inayaruhusu, hivyo
alichokuwa akifanya ni kuwaita viongozi wa vyama vinavyotaka kuandamana
na kufanya nao makubaliano ya namna maandamano hayo yanavyopaswa
yafanywe kabla ya kuyaruhusu.
“Pengine hiyo ndiyo sababu sikuwahi kushambuliwa
kwa maneno ya kejeli au matusi na wanasiasa kwa kuwa sikuwahi kuzuia
maandamano yao bila sababu na hata kama kulikuwa na sababu niliwaita na
kuwaeleza na tulikubaliana.
“Kikubwa ni kujenga tabia ya kuwaita viongozi wa
waandamanaji na kujadiliana nao, vinginevyo wanaweza pia hata
kukufikisha mahakamani wakipinga kuzuiwa maandamano yao,” alisema
Tibaigana ambaye alikumbana na sakata la kudai maandamano wakati akiwa
Kamanda kwenye mikoa ya Tanga, Arusha na Dar es Salaam.
“Nilikuwa nawaita viongozi nakaa nao
tunakubaliana. Hata kama ningeambiwa na kiongozi gani nisitoe kibali,
kama hakuna sababu za kweli, nilikataa kwa kuwa kisheria mimi ndiye
nawajibika kama vyama vikishtaki. Ili uzuie maandamano unapaswa kuwa na
sababu za msingi ambazo ukiwaeleza waandamanaji wanakuelewa.”
Tibaigana anakumbuka jinsi CUF kilivyoandaa
maandamano makubwa kushinikiza kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani
Zanzibar baada ya kutoridhishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2005,
lakini anasema kutokana na msimamo wake, haikuwa vigumu kwake kuruhusu
jambo hilo.
“Wakati wa uongozi wangu CUF ilikuwa na nguvu
sana, lakini mimi sikuwa na tatizo nao. Walipotaka kibali cha kuandamana
niliwapa bila woga na tuliishi vizuri,” anaeleza Tibaigana.
Vuguvugu la maandamano pia lilitanda wakati wa
maandalizi ya ziara ya Rais wa zamani wa Marekani, George Bush nchini
kutokana na wasomi na baadhi ya wanaharakati kutaka kufanya maandamano
kupinga vitendo vya taifa hilo kubwa dhidi ya raia wa Palestina na
sehemu nyingine ambako wananchi wasio na hatia walikuwa wakiuawa.
“Nilichofanya ni kukutana nao na kuwaeleza njia
ambazo wangeweza kutumia katika maandamano hayo na hali ilikuwa shwari,”
alisema Kamanda Tibaigana.
Katika kipindi chake cha uongozi wa Polisi Dar es
Salaam, Kamanda Tibaigana pia alikumbana na vurugu za kidini ambazo
zilisababisha askari mmoja kupoteza maisha, lakini anasema kwa
kushirikiana na wadau wengine, walijipanga na hali ikawa shwari.
Alivyomng’ang’ania Ditopile
Moja ya matukio makubwa wakati akiwa Kamanda wa
Kanda ya Dar es Salaam ni tukio la mkuu wa zamani wa Mkoa wa Tabora,
Ditopile kumuua dereva wa daladala baada ya kutokea kutoelewana
barabarani, hali iliyolazimu sheria kufuata mkondo wake. Jeshi la Polisi
lilitakiwa limkamate mkuu huyo na kumfikisha mahakamani.
Ditopile alituhumiwa kufanya mauaji hayo Novemba
5, 2006.
Akidaiwa kumuua kwa kumpiga risasi dereva wa daladala, Hassan Mbonde. Alikamatwa na kufikishwa mahakamani, lakini alifariki dunia Aprili 20, 2008 wakati kesi yake ikiendelea.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Akidaiwa kumuua kwa kumpiga risasi dereva wa daladala, Hassan Mbonde. Alikamatwa na kufikishwa mahakamani, lakini alifariki dunia Aprili 20, 2008 wakati kesi yake ikiendelea.
Kamishna Tibaigana anasema tukio hilo lilimtia katika msukosuko
mkubwa kutokana na kupata shinikizo kutoka kwa viongozi mbalimbali
waliokuwa wakitaka asitekeleze wajibu wake wa kumkamata na kumfikisha
mahakamani.
“Nilihojiwa na baadhi ya viongozi baada ya kuamuru
Ditopile akamatwe, lakini nikasisitiza kuwa amevunja sheria kama
walivyo wahalifu wengine,” alisema.
Kamanda Tibaigana alisema kuwa alifanya uchunguzi
wa tukio hilo hatua kwa hatua, tangu Ditopile alipokuwa akifukuzana na
gari hilo hadi alipompiga risasi dereva wake, akajiridhisha kuwa
alivunja sheria.
“Baada ya hapo niliamuru Ditopile akamatwe kama
watu wengine. Sasa tatizo ni kwamba watu wengine walichukulia suala hilo
kisiasa na baadhi walikuwa wakinitisha kwamba nikimkamata nitafukuzwa
kazi. Lakini mimi niliamini sheria iko palepale. Kwangu halikuwa tukio
kubwa,” anasema.
Tibaigana ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alisema
katika masuala ya sheria, uwezo au hali ya mtuhumiwa haina nafasi
katika uamuzi wa mashtaka yanayomkabili.
‘Niliulizwaulizwa na viongozi sababu ya kumkamata
Ditopile na kumweka ndani. Niliwajibu ushahidi tulioukusanya unatosha
kumpeleka mahakamani, hilo suala halikunishtua sana,’’ anasema
Tibaigana.
Ziara ya Clinton
Kamanda Tibaigana pia anajivunia jinsi alivyoweza
kuimarisha ulinzi wa Taifa wakati wa ziara ya marais wawili wa zamani wa
Marekani, akiwa na majukumu ya kipolisi mkoani Arusha na Dar es Salaam.
Akiwa Kamanda wa Polisi wa Arusha, Tibaigana
alihusika na ulinzi wakati wa ziara ya Rais wa zamani wa Marekani, Bill
Clinton. Pia anasema alifanikiwa kuimarisha ulinzi wakati wa ziara ya
Rais Bush nchini wakati akiwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Anasema ziara hizo za marais wa nchi hiyo, ziliwatia woga viongozi wa hapa nchini na wa Marekani.
Baada ya kuondoka salama nchini, Tibaigana anasema
viongozi hao wa Marekani walimwandikia barua maalumu ya kumshukuru
kutokana na kazi kubwa ya ulinzi waliyoiona, jambo ambalo alisema
lilikuwa sifa kubwa kwa Taifa.
Matukio mengine makubwa
Tibaigana pia anajivunia kulipaisha jina la Jeshi la Polisi la
Tanzania kimataifa baada ya kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa ugaidi
aliyekuwa akisakwa na Serikali ya Marekani.
Anasema mwaka 1995 wakati huo akiwa Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Arusha, Marekani ilitangaza donge nono
kwa mtu ambaye angefanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye alidai
kwamba alikuwa anatega mabomu na kulipua kumbi za starehe katika nchi
mbalimbali duniani.
Anasema baada ya kupitia nyaraka mbalimbali
zilizohusiana na taarifa za awali za mhalifu huyo, ilibainika kuwa
alikuwa amejificha nchini na kuwa alipewa maelekezo na Inspekta Jenerali
wa Polisi wakati huo, Omary Mahita kumtafuta mtuhumiwa huyo.
Alisema aliomba wiki moja, lakini akafanikiwa kumtia nguvuni ndani ya siku moja.
Anasema pamoja na kauli yake kutoaminika kwa
viongozi wake, aliishangaza dunia kwa kumkamata mhalifu huyo ambaye
hakumtaja jina ndani ya siku moja akiwa na dereva wake pamoja na
msaidizi mmoja.
Baada ya kumkamata, Ubalozi wa Marekani
ulijulishwa na baadaye nchi hiyo kutuma wapelelezi wake ambao
walimtambua kuwa ndiye mhalifu aliyekuwa akitafutwa.
Anasema suala hilo liliweka jina la Jeshi la
Polisi katika sura ya Kimataifa na nchi ikapata pongezi nyingi kutoka
Marekani kwa kufanikisha kumkamata mhalifu wa kimataifa aliyekuwa
anasakwa na dunia nzima na kwamba walipewa donge lililoahidiwa na
wakagawana kwa utaratibu waliojiwekea.
“Kwa wakati huu huyo mhalifu angeweza kufananishwa
na (kiongozi wa kundi la Al Qaeda, marehemu) Osama bin Laden kwa jinsi
alivyokuwa anasakwa na dunia.”
Kamanda Tibaigana alibainisha kuwa kukamatwa kwa
mtuhumiwa huyo kuliondoa hisia zilizokuwa zimeanza kujengeka kuwa nchi
imeshindwa kumtafuta na kumkamata. Anasema taarifa za mitandao ya
Marekani zilionyesha kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amejificha hapa nchini.
Uhalifu wa mtandao
Akizungumzia tatizo la uhalifu wa kutumia mtandao
ulioanza kushika kasi nchini, Kamanda Tibaigana anasema wakati wa
uongozi wake suala hilo halikuwa kubwa na kuwa polisi haina budi
kubadilika ili kwenda na mazingira ya sasa.
Anasema Serikali inawapeleka askari wake nje ya
nchi kupata mafunzo mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu, lakini hilo
pekee halitasaidia katika utendaji kwa kuwa hakuna vifaa vya kisasa
vinavyohitajika kwa kazi hiyo.
“Mimi nimekwenda kozi mbalimbali dunia nzima, lakini ukirudi
hapa nyumbani vifaa vya kufaya kazi hiyo havipo kwa sababu ya ufinyu wa
bajeti. Matokeo yake tunabaki kujivunia takwimu kuwa tuna askari
waliopata mafunzo nje ya nchi,” anasema Tibaigana.
Anasema hata baadhi ya vifaa huchukua muda mrefu
kununuliwa na hivyo huwakuta wale waliopata mafunzo ya jinsi ya
kuvitumia wakiwa tayari wamestaafu kazi, hali inayofanya kukosekana kwa
wataalamu wa kuvitumia.
Anaishauri Serikali iache kusuasua katika ununuzi
wa vifaa vya kisasa kuwezesha utendaji wa ufanisi wa jeshi hilo katika
kukabiliana na uhalifu.
Polisi kushirikiana na wahalifu
Pia alizungumzia tuhuma za polisi kushirikiana na
wahalifu. Katika hilo, Kamanda Tibaigana anasema tuhuma hizo ni kweli
akisema tatizo hilo ni sawa na msafara wa mamba kujumuisha kenge pia.
Alisema polisi ni sehemu ya jamii na kwamba wapo
askari wachache wanaochafua taswira ya jeshi hilo, lakini suala hilo
linakuzwa sana.
“Matatizo hayo yapo tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi na viongozi wengi wa jeshi wanayashughulikia,” alisema.
Alisema polisi wengi wanaotuhumiwa kuhusika katika
uhalifu, hufikishwa kwenye mahakama za kijeshi ambako uamuzi hufanyika
haraka, lakini kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya askari kuwa
kupelekwa kwenye mahakama hizo ni kukiuka haki za binadamu.
Kuhusu ubunge
Tibaigana aligombea ubunge wa Jimbo la Muleba
Kusini baada ya kustaafu, lakini akashindwa katika kura za maoni ndani
ya CCM na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, lakini hana mpango wa kurudi tena ulingoni kugombea nafasi
hiyo.
“Wakati naomba kura ili niteuliwe na chama changu
cha CCM kugombea ubunge, niliwaambia wananchi kuwa wanipe miaka mitano
tu. Sasa, kwa kuwa muda huo umeshapita, nawaachia wengine,” anasema
Tibaigana.
Alisema kuwa kama angetaka angeweza kugombea kama
mgomea binafsi bila kupitia chama chochote kama suala hilo lingepitishwa
katika Katiba Mpya, lakini ameamua kupumzika.
Mchakato wa Katiba Mpya
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Tibaigana anasema
awali, alikuwa muumini wa Muungano wenye wa serikali tatu, lakini
amebadilisha msimamo wake baada ya kuridhika na hoja za wanaotetea
muundo wa serikali mbili.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment