
SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli kutoa taarifa yake bungeni
iliyowang’oa mawaziri wanne, vita kali imeibuka kati yake na mbunge wa
Msalala, Ezekiel Maige (CCM).
Itakumbukwa kuwa kamati hiyo ya Lembeli ndiyo ilishinikiza kung’olewa
kwa Maige katika nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na
mawaziri wengine mwaka jana kwa kashfa ya utoroshwaji wa wanyamapori hai
nje ya nchi.
Kufuatia hatua hiyo, wakazi wa Msalala wilayani Kahama, Mkoa wa
Shinyanga, wamemtaka Lembeli ambaye pia ni mbunge wa Kahama, amuombe
radhi mbunge wao, Maige kutokana na walichodai ni fitina alizomzushia
hadi akapoteza wadhifa wa uwaziri mwaka jana.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti juzi mjini
Kahama, wakazi hao walisema wamelazimika kumtaka Lembeli amuombe radhi
Maige kufuatia kitendo chake cha kutaka kumsafisha aliyekuwa waziri wa
wizara hiyo, Balozi Khamis Kagasheki.
Lembeli katika kuhitimisha hoja ya taarifa ya kamati yake bungeni
hivi karibuni, alimtetea Waziri Kagasheki aliyeamua kujiuzulu akidai
hakuhusika moja kwa moja katika kashfa ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Wakazi hao walisema wanamtaka Lembeli aombe radhi ili amsafishe Maige
kutokana na tuhuma kali alizomzushia wakati akiwa waziri kwa kumtuhumu
kwamba alihusika na utoroshaji wanyamapori hai kwenda nje ya nchi.
Walisema kama Lembeli alikiri bungeni kuwa Waziri Kagasheki
hakuhusika moja kwa moja na vitendo viovu vilivyotendwa na askari wakati
wa kutekeleza operesheni hiyo, anapaswa kumwomba radhi na Maige ambaye
pia hakuhusika moja kwa moja.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Masanja Joseph alifafanua kuwa
katika taarifa yake bungeni, Lembeli alionyesha wazi dhamira ya kutaka
kumsafisha Kagasheki akidai hakuhusika moja kwa moja licha ya unyama
uliofanyika katika operesheni hiyo.
Joseph alisema Lembeli katika taarifa yake alidai watendaji ndani ya
wizara hiyo wakiongozwa na Katibu Mkuu wao, Maimuna Tarishi ndio
wanaostahili kubeba lawama na kuwajibishwa kwa vile Kagasheki hakuwa
mtendaji wa moja kwa moja.
“Kauli hii ilitutia wasiwasi maana katika uamuzi wa kamati hiyo dhidi
ya Maige, kuhusiana na kashfa ya utoroshwaji wa wanyama hai, huyo
alibebeshwa msalaba peke yake ambapo hata maofisa usalama wa taifa
hawakuguswa kabisa tofauti na ilivyokuwa kwa taarifa ya Operesheni
Tokomeza Ujangili.
“Hii ni ajabu sana, wakati wa tuhuma za kutoroshwa wanyama hai,
Lembeli alimbebesha moja kwa moja tuhuma Maige kuwa alizembea na
kusababisha wanyama watoroshwe, leo katika kashfa ya Operesheni Tokemeza
Ujangili anadai Kagasheki hakuhusika moja kwa moja, hapa hajatenda
haki,” alieleza Joseph.
Wananchi hao walisema ni jambo la kushangaza kuona mtu ambaye tuhuma
zake hazikuhusisha kupoteza maisha ya Watanzania alihukumiwa peke yake
bila watendaji wengine.
Kwamba huyu ambaye ameguswa na tuhuma za mauaji ya binadamu na mifugo
kuibwa na mingine kuuawa, anatetewa na kamati ikitaka mzigo wake ubebwe
na watendaji ndani ya wizara.
“Kwa hali hii kuna kila sababu sasa Lembeli akamsafisha mbunge wetu
kwamba hakumtendea haki, na ikibidi ifike wakati na yeye mwenyewe
ajipime katika uhakimu wake anaoufanya mara kwa mara kama kweli huwa
anatenda haki.
“Kwa taarifa hii aliyoitoa bungeni juzi ilionyesha wazi huenda
alitofautiana na katibu mkuu wa wizara au watendaji wengine walioonyesha
nia ya kutaka kupingana naye na hivyo kutaka awabebeshe zigo lote peke
yao,” alisema.
Waliongeza kuwa kitendo cha Lembeli kuwawajibisha mawaziri wawili
ndani ya wizara moja kimewashtua, huku tukio la mbunge wao Maige
likibakia gumzo kwani hakupewa nafasi yoyote ya kutoa utetezi wake
bungeni.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment