Davis Mwamunyange na Said Mwema 
WAKATI shinikizo la kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kujiuzulu ama awajibishwe kutokana na kashfa ya ukatili mauaji dhidi ya wananchi wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili likizidi kushika kasi, vumbi jipya la maofisa wa juu wa serikali wanaotakiwa kuwajibika limewaangukia Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange.
 
Shinikizo hilo jipya limetoka kwa madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam jana, ambao wamesema Mwema na Mwamunyange hawawezi kujinusuru katika kadhia hiyo.

Katibu wa madiwani wa jiji hilo, Julian Bujugo, alisema wakuu hao wa vyombo vya dola wanapaswa kujiuzulu kwa kuwa ndio wanaotoa amri kwa askari walio chini yao.

“Pamoja na mawaziri, viongozi hao wanatakiwa kujiuzulu kama hatua ya kuonyesha uwajibikaji kwani askari wao wamefanya maovu makubwa,” alisema.

Madiwani hao wengi wao wakitoka Chama Cha Mapinduzi, walisema ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili ilibainisha uozo katika Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo ilisimamiwa na askari wa vyombo vyao.

Walisema kubainika kwa ukiukwaji wa haki za binadamu katika operesheni hiyo, ndiko kulimsukuma Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne ambao ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Balozi Khamisi Kagasheki (Malisili na Utalii), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na Mathayo David (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).

Hivyo, kwa kuwa mawaziri hao waliwajibika, Mwema na Mwamunyange hawana sababu ya kuendelea kushikilia nafasi zao zaidi ya kuwajibika wenyewe ama wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.

Pamoja na wakuu hao wa polisi na JWTZ, madiwani hao wametaka pia wakuu wote wa wilaya waliohusika kusimamia operesheni hiyo nao wawajibike kwa kuwa walijua na waliona vitendo walivyofanyiwa wananchi, lakini hawakuchukua hatua yoyote.

Bujugo alisema kama viongozi hao watakaidi agizo la madiwani kuwataka wajiuzulu, watalipeleka suala hilo kwa Rais Kikwete.

Pinda ang’ang’aniwa
Nalo shinikizo la kumtaka Rais Kikwete kumng’oa Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika nafasi yake limezidi kuongezeka licha ya hatua ya kiongozi huyo mkuu wa serikali bungeni kupuuza maoni ya wabunge.

Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumatano, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kuwa ili serikali ionekane inaheshimu misingi ya haki za binadamu lazima Pinda awajibike.

“Pinda lazima awajibike bila kujali kiasi cha gharama ambazo zitapotea kwa kuwatunza wastaafu kwani  tukio la kuuawa kwa Watanzania ni kubwa kuliko la kuwahudumia wastaafu,” alisema Lipumba.

Alisema kuwa kama tunajipambanua kwa kufuata misingi ya kulinda haki za binadamu, ni lazima Pinda aachie ngazi kutokana na namna alivyolishughulikia suala hilo kimzaha kwa mara ya kwanza lilipoingia bungeni.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema kuwa lazima Pinda awajibishwe kwa sababu hata mwenyewe alikiri kwamba kazi ya uwaziri mkuu ni mzigo kwake.

“Kwa maneno yake mwenyewe anaonyesha huo ni mzigo mzito aliobebeshwa na hauwezi. Hivi Rais Kikwete kwanini asimuache mtoto wa mwenzake asije kuvunjika kwa ajili ya mzigo huo,” alisema Mallya.

Akizungumza wale wanaofikiria kwamba iwapo atawajibishwa atasababisha kuwepo kwa gharama kubwa serikalini, Usu alisema hakuna gharama kwa sababu kwa mujibu wa sheria atapoteza haki zake na hivyo serikali haina haki ya kuingia gharama za kumtunza.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema alipingana na wanaoshinikiza kujiuzulu kwa Pinda, akiwataka Watanzania kuridhika na hatua ya kung’oka mawaziri wanne.

“Iwapo tutamng’oa Waziri Mkuu, tutakuwa na mlundikano wa mawaziri wastaafu hali itakayosababisha kuwepo kwa ongezeko la gharama za kuwatunza. Kumbuka hata mimi nilikuwa Naibu Waziri Mkuu  mstaafu mpaka sasa sijalipwa fedha zangu, sasa tuongeze tena Pinda.

“Sisi tumeongoza nchi, hivyo tunatakiwa kuondokana na ushabiki ingawa hata mimi napenda kuondolewa kwa Mizengo Pinda, lakini kwa wakati huu ambao tunataka kuisafisha serikali niko tayari hata kumuongezea Rais Kikwete watu wengine ambao hata yeye hawajui,” alisema.

Mrema aliongeza kuwa wapo baadhi ya mawaziri wabovu ambao Rais Kikwete hawajui na ndio wamekuwa wakihusika kuvuruga utendaji wake.

Kamati hiyo iliyoongoza na James Lembeli iliwasilisha taarifa yake bungeni mwishoni mwa wiki iliyopita.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top