
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samueli Sitta
MWENENDO wa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta,
umeanza kutiliwa shaka huku baadhi ya wajumbe wenzake wakidai anateswa
na dhambi ya unafiki.
Sitta, ambaye aliongoza Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano kwa
uwezo mkubwa chini ya falsafa yake ya viwango na kasi, alichaguliwa kwa
kura nyingi kuongoza Bunge la Katiba akiahidi kuendeleza falsafa hiyo.
Hata hivyo Sitta ameanza kushindwa kuitekeleza ahadi hiyo baada ya
kuruhusu kufinyangwa kwa kanuni za Bunge pamoja na kufanya uteuzi wa
wajumbe wa kamati ya uongozi akiwapendelea wajumbe kutoka CCM.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kuyumba huko kwa Sitta
kunachangiwa na ndoto zake za kutaka kuwania urais mwaka 2015, hivyo
anatafuta kuungwa mkono na CCM.
Sitta anatafuta kuungwa mkono na CCM kwakuwa chama hicho mwaka 2010
mara baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu kilimtosa kuwania uspika kwa
madai ni zamu ya mwanamke.
Miongoni mwa sababu zilizokuwa zikitajwa chinichini ni kuwa kiongozi
huyo wakati akiwa spika aliruhusu mijadala iliyozusha makundi ndani ya
chama na serikali.
Katika utawala wake Sitta, aliunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza
zabuni iliyoipa ushindi wa kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura
Kampuni ya Richmond, iliyokuwa ikilipwa sh milioni 152 kwa siku.
Kamati teule hiyo iliyokuwa chini ya Dk. Harrison Mwakyembe, ilitoa
ripoti iliyobaini kulikuwa na utata katika kuipa ushindi zabuni ya
Richmond, waliodai ni ‘hewa’ na yenye mkono wa ‘bwana mkubwa’.
Kashafa hiyo ilimfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu baada ya kuguswa na kashfa hiyo.
Hata hivyo mchakato huo ulifungwa na Sitta, katika mazingira ya
aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), aliyeguswa pia na kashfa
hiyo akitaka iundwe tume huru ya majaji watatu kuchunguza sakata hilo.
Tangu hapo Sitta, amekuwa kwenye uahasama mkubwa na makada wenzake
pamoja na chama ambacho kinaamini utawala wake ndio uliozalisha
wapinzani wengi bungeni hivi sasa.
Kutokana na dhana hiyo, Sitta hivi sasa amekuwa akifanya mambo
yanayoonekana kutafuta huruma ya chama chake ambapo pia nusuru kisimpe
ridhaa ya kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, nafasi iliyokuwa ikitajwa
kukaliwa na Andrew Chenge.
Miongoni mwa mambo anayoshutumiwa kuyafanya Sitta ni kuwakemea
wenzake kwa ufisadi wanaoufanya wanapotoa fedha kwenye harambee na
shughuli za kijamii ilhali naye amekuwa akipita makanisani kuomba huruma
ya wananchi.
Sitta pia analaumiwa kwa kuruhusu uvunjwaji wa kanuni za kuliongoza
Bunge kwa kuruhusu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe
rasimu ya katiba kabla ya Rais Jakaya Kikwete.
Inadaiwa alifanya hivyo ili kumtengenezea mazingira Rais Kikwete,
kujibu mapendekezo yaliyokuwamo kwenye Rasimu ya Katiba ili kuipa ahueni
CCM inayopinga mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa kwenye rasimu.
Sitta pia anadaiwa kufanya uteuzi wa wajumbe watatu kati ya watano
kuingia katika kamati ya uongozi ambayo inaongozwa na wenyeviti 12
kutoka CCM.
Miongoni mwa walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni Profesa Ibrahim
Lipumba, ambaye alikataa uteuzi huo huku akimlaumu Sitta kwa kufanya
uteuzi unaoangalia zaidi masilahi ya chama chake kuliko taifa.
Baadhi ya wajumbe hususan wapinzani wanadai Sitta anayumbishwa na
Chama chake Cha Mapinduzi (CCM), hivyo kufikia hatua ya kuzivunja kanuni
za Bunge na kuibua mivutano.
Udhaifu wa Sitta
Baadhi ya wajumbe wa upinzani wanasema tabia ya kutokuwa na msimamo
aliyoanza kuionyesha Sitta hivi sasa kwa kufuata matakwa ya chama chake
bila kujali uzito wa hoja husika kumemvunjia heshima.
Hoja yao ni kuwa falsafa ya ‘Kasi na Viwango’ aliyoitangaza
ameshindwa kuionyesha katika Bunge Maalumu kiasi cha kuyumbisha mchakato
wa mijadala bungeni.
Pia ndani ya CCM, Sitta anatazamika kwa sura mbili. Mosi, washindani
wake kisiasa wanadai anaongoza Bunge hilo kwa kuwasikiliza zaidi
wapinzani ili kujijengea uhalali wa kugombea urais 2015.
Kundi la wafuasi wake, lenyewe linaona kama Sitta yuko imara
kusimamia mchakato wa Katiba isipokuwa anakwazwa na mahasimu wake ndani
ya chama wanaomuundia zengwe aonekane dhaifu.
Kangi Lugola (CCM), alikuwa wa kwanza kumtahadharisha Sitta kuhusiana
na uongozi wake, akisema nafasi yake ni sawa na Jaji wa Mahakama Kuu
aliyepelekewa mtuhumiwa wa mauaji amhukumu.
“Sitta ndiye amepewa jukumu la kuhakikisha anasimamia mchakato huu
ili wananchi wapate Katiba mpya na nzuri, kushindwa kufanya hivyo
wananchi wataondoa imani kwake na chama,” alisema Lugola ambaye pia ni
Mbunge wa Mwibara.
Lugola aliongeza kwamba licha ya CCM kuwa na wajumbe wengi katika
Bunge hilo lakini Sitta alichaguliwa kwa kuaminiwa kutokana na utashi
wake wa kisiasa, hivyo anapaswa kutumia busara.
Naye Godbless Lema (CHADEMA) alimtaka Sitta kuwa makini na kila aina
ya ushauri anaopewa na wenzake ndani ya CCM, kwamba mwingine una lengo
la kumchafulia rekodi yake.
Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, alisema kuwa wabaya wa
Sitta wamekuwa wakijidai kumshauri hata mambo ambayo baadaye yanaleta
matatizo kwa lengo la kutaka kuonyesha kuwa alishindwa kusimamia
mchakato wa kuandika katiba.
“Wako wabaya wako wanataka mchakato huo usifanikiwe ili ionekane
ulishindwa kusimamia wananchi wapate katiba, hivyo waseme haufai hata
kugombea urais,” alisema Lema bungeni.
Naye John Shibuda, anasema Sitta anatafunwa na dhambi ya unafiki wake ambao hauwezi kumfikisha katika anachokifikiria.
Shibuda alisema Sitta amejikuta wakati mwingine akifanya uamuzi wa
kuibeba CCM ili kujinafikisha aonekane ni kada mwaminifu na wakati huo
huo anataka kujijengea ushujaa ili katiba mpya ipatikane, atumie turufu
hiyo kujipigia debe la urais 2015.
Wiki iliyopita Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema
Sitta ni dhaifu na ndiyo maana anashindwa kuongoza Bunge Maalumu la
Katiba kwa sababu ya kuegemea zaidi kwenye chama chake.
Dk. Slaa alisema uongozi wa Sitta bungeni utasababisha mivurugano
mikubwa na kutoelewana baina ya wajumbe waliopewa jukumu la kuandika
Katiba inayopendekezwa, ambayo itakwenda kupigiwa kura ya maoni na
wananchi.
Sitta amekuwa akilalamikiwa na baadhi ya wajumbe tangu siku ya kwanza
alipokalia kiti hicho kuwa anavunja kanuni alizotamba kuzisimamia kwa
kasi na viwango.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment