
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Jakaya Mrisho Kikwete
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinaanza wiki ngumu ya kusaka theluthi
mbili ya kura za wajumbe kutoka Zanzibar ili kiweze kubatilisha
mapendekezo ya rasimu ya Katiba ya muundo wa muungano wa serikali tatu.
Chama hicho kinachotetea muundo wa serikali mbili, kimekuwa katika
harakati za hapa na pale kutafuta uungwaji mkono wa wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba wenye msimamo tofauti.
Wajumbe wa Bunge hilo kupitia kamati zao kumi zenye wajumbe kati ya
52 na 53, kesho wanaanza kuijadili rasimu kwa kuchukua sura ya kwanza na
ya sita.
Sura hizi ni nyeti, kwa sababu ndizo zitatoa mwelekeo wa ama muungano
utabaki kuwa wa serikali mbili kama CCM inavyotaka au serikali tatu
zilizopendekezwa na wananchi kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Sura ya kwanza ya rasimu imegawanywa katika sehemu mbili, ambapo
sehemu ya kwanza inazungumzia jina, mipaka, alama, lugha na tunu za
taifa.
Sehemu ya pili ya sura hiyo, inazungumzia mamlaka ya wananchi, utii na hifadhi ya Katiba.
Sura ya sita inahusu muundo wa Jamhuri ya Muungano. Mambo yaliyowekwa
ni muundo wa muungano, vyombo vya utendaji vya Jamhuri ya Muungano,
mamlaka ya Serikali ya Muungano, mambo ya muungano na nchi washirika.
Yapo pia mamlaka ya nchi washirika, uhusiano kati ya nchi washirika,
mawaziri wakaazi, mamlaka ya wananchi na wajibu wa kulinda muungano.
Katika taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyotolewa na Jaji
Joseph Warioba, wakati akiwasilisha rasimu ya katiba bungeni, alisema
kuwa waasisi wa taifa waliacha muungano wa nchi moja, serikali mbili
lakini sasa kuna nchi mbili serikali mbili.
Warioba alisema kuwa muungano umefikia hapo kutokana na kile
kilichoitwa mchafuko wa kisiasa visiwani Zanzibar mwaka 1984 na hatimaye
kuzaa mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar, ambayo yanakinzana na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Kwa mantiki hiyo, Jaji Warioba alisema muundo wa serikali mbili
hautekelezeki tena kutokana na viongozi kushindwa kusimamia azimio la
kutoka serikali mbili kuelekea serikali moja.
Mapendekezo hayo ya tume ya Jaji Warioba yameivuruga CCM, hivyo
kutumia kila aina ya mbinu kuhakikisha serikali tatu hazipiti katika
Bunge Maalumu la Katiba.
Mbinu zilizofanywa tangu Warioba awasilishe rasimu hiyo ni kumtumia
Rais Jakaya Kikwete, kuiponda tume hiyo akidai takwimu zao kuhusu idadi
ya watu waliotoa maoni juu ya muundo wa muungao hazina mashiko.
Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya rasimu kama
wakiamua kuendelea na serikali mbili mambo mengi yatatekelezeka lakini
kwa serikali tatu hayawezekani.
Alisema kuwa serikali tatu hazitekelezeki kwa sababu rais wa
shirikisho ana dola isiyokuwa na ardhi na rasilimali za kiuchumi, hivyo
serikali yake haiwezi kukopesheka.
Katika kupigia debe serikali mbili, rais aliwatisha wajumbe wa Bunge
la Katiba akisema muundo wa serikali tatu ulivyo iko siku jeshi linaweza
kupindua serikali za washirika, kupiga na kufukuza watu kisha wakavua
magwanda na kuingia madarakani.
CCM katika kujiimarisha kuhakikisha inahodhi mchakato huo, makada
wake wakiwemo mawaziri ndio wamechaguliwa kuongoza kamati 12 za Bunge
hilo kati ya 14 ambazo wenyeviti wake ndio wanaunda kamati ya uongozi.
Pia chama hicho kimefanikiwa kutumia wingi wake kuamua wajumbe wa
Bunge hilo watumie kura mseto (wazi au siri) wakati wa kupitisha ibara
na sura za rasimu kwa kuhofia kusalitiwa na wajumbe wake.
Hata hivyo, juhudi hizo ni sawa na kazi bure endapo CCM itakosa
uungwaji mkono wa idadi ya theluthi mbili ya wajumbe kwa pande zote
mbili za Bara na Visiwani.
Pamoja na kudhibiti mfumo wa upigaji kura uwe wa mseto, sura ya sita
kuhusu muundo wa muungano CCM haitaweza kuwabana wajumbe kutoka Zanzibar
kwani wengi wao wanataka serikali tatu.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa walitarajia kuona CCM ikijenga
ushirikiano na CUF kwa upande wa Zanzibar kutokana na wote kuwa katika
serikali ya umoja wa kitaifa ili kutumia kura zake chache na zile za
washirika kupata idadi inayotakiwa lakini haikuwezekana.
Kwa mujibu wa sheria iliyounda Bunge Maalumu la Katiba, ili uamuzi
wowote uweze kufikiwa wakati wa kupitisha ibara au sura kwenye kamati na
Bunge, sharti kuwe na theluthi mbili ya kura kwa pande zote.
CCM katika kujirahisishia njia, ilijaribu kutumia wajumbe kupitia
kamati ya uongozi kuleta mapendekezo ya marekebisho ya kanuni kadhaa za
Bunge hilo ikiwemo kanuni ya 64(1).
Katika mapendekezo hayo ambayo yalikataliwa na wapinzani, kamati
ilitaka kurekebisha hanuni hiyo ya 64(1) kwa kuondoa sharti la uamuzi
wowote kwenye kamati kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe kutoka
Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.
Badala yake ilipendekezwa kwamba mwenyekiti wa kamati atawahoji
wajumbe ambapo walio wengi watashinda. Hapa ndipo CCM imegonga kisiki
kingine katika harakati zake za kutetea serikali mbili.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, John Mnyika, aliliambia Tanzania Daima
Jumapili kuwa CCM ilishikilia msimamo wa upigaji kura mseto ikiamini
kwamba watautumia kutekeleza azima yao kuhusu waraka wao wa siri na
maelekezo ya hotuba ya Mwenyekiti wao, Kikwete.
“Matokeo ya juzi yatatusaidia kujipanga kudhibiti mbinu zao za
kuhujumu rasimu ya Warioba kinyume cha maoni ya wananchi na uchambuzi wa
wataalamu.
“Hata hivyo, kura hizo hazitoi picha kamili ya kura zitakavyokuwa
kwenye sura ya kwanza na ya pili, kwa kuwa; kura za juzi zilikuwa juu ya
utaratibu wa kura,” alisema.
Kwa mujibu wa Mnyika, wapo wajumbe waliokubaliana tu na utaratibu ili
Bunge lisonge mbele lakini likija suala la muungano, watapiga kura
tofauti.
Aliongeza kuwa kura juzi ilikuwa ya wajumbe kwa pamoja wakati kura
kuhusu rasimu kila upande wa muungano utapiga tofauti na kura
hazitahesabiwa kwa wingi wa kawaida bali theluthi mbili ya kila upande
wa muungano na CCM haina theluthi mbili Zanzibar.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment