Wachambuzi kadhaa wa mwenendo wa siasa nchini wameliambia gazeti hili
jana kwamba njia ya kuihakikishia CCM ushindi mwakani ni kuhakikisha
Mbowe na Dk. Slaa hawawi sehemu ya uongozi wa chama hicho kikuu cha
upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.
Kwa mujibu wa watoa habari wetu, ambao hawakupenda kutajwa gazetini,
hata chokochoko za wanachama wasaliti na waliofukuzwa ambao bado wanaona
fahari kujihusisha na kile wanachoita jitihada za “kusafisha CHADEMA”,
ni sehemu ya mkakati mzito wa CCM kutumia watu wanaoonekana kuwa ndani
au karibu ya chama hicho, ili kuonyesha umma kwamba kina migogoro.
“Imewachukua CCM muda mrefu kutambua uwezo wa Mbowe kuongoza na
kupanga chama kimkakati. Kama wangejua zamani wangeshammaliza kabla
hajaonyesha makali. Hata hivyo, bado wanasema wana muda, na wana vijana
wanaoweza kuifanya kazi hii kwa malipo kidogo tu,” alijitapa mmoja wa
wachambuzi hao, akidai anajua kwa karibu mipango ya baadhi ya vigogo wa
CCM.
Alisema kwamba awali walijaribu kutumia mbinu zile zile walizotumia
kuua au kudhoofisha vyama vya upinzani huko nyuma, hasa NCCR-Mageuzi,
Chama cha Wananchi (CUF) na Tanzania Labour Party (TLP), lakini
wamegundua kuwa haziwezi kufanya kazi kwa CHADEMA kwa sababu kina
viongozi wasio wepesi.
Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, CCM walitumia ruzuku na ushushushu kama
silaha ya kuua vyama kwa kupandikiza migogoro. Mahali pengine walitumia
pesa, na hisia za udini, ukabila na ukanda, lakini kwa CHADEMA
wamegundua hoja hizo hazina mashiko kwani chama kimekuwa kinakua kila
sehemu ya nchi.
“Kwa NCCR-Mageuzi ilikuwa rahisi kusema wanagombania ruzuku. Wakati
huo ruzuku kwa vyama lilikuwa jambo jipya, na ni kauli ambayo iliaminika
kirahisi. Hata pale walipoanza kushambuliana kwamba mashushushu
wamevamia chama, ilikuwa rahisi kwa umma kuamini.
“Viongozi waligombanishwa bila kujua, chama kikameguka. Mwenyekiti
akaondoka na pande lake, na katibu akabaki na lake. Kwa CHADEMA
imeshindikana kuwatenga mwenyekiti na katibu mkuu, hivyo chama kimebaki
kimoja. Hata hawa walioondoka, wameondoka na makundi ya watu, lakini
hayana nguvu ya kubomoa chama. Mbinu kuu iliyobaki sasa ni kuhakikisha
Mbowe na Dk. Slaa wanaondoka kwenye uongozi. Hapo hutaona CHADEMA tena,”
alidokeza.
Mchambuzi mwingine ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mzumbe,
alisema kinachowatisha CCM ni kwamba Mbowe na Dk. Slaa hawatingishiki
kwa pesa wala kwa vitisho.
Alisema: “Hata hii mbinu ya kutumia akina Zitto imeshindwa kuleta
matunda waliyotaka. Sasa hapa kuna mambo kadhaa ya kuchunguza. Tazama
vijana waliokimbilia kwenye chama kipya kilichoanzishwa na kusajiliwa
haraka haraka. Sikiliza lugha wanayotumia kujenga chama chao.
Wanashambulia viongozi wa CHADEMA.
“Ukitazama juhudi kubwa za kujenga na kukuza CHADEMA katika kipindi
cha uongozi wa Mbowe na Dk. Slaa, utaelewa kwanini CCM na baadhi ya
wasiotakia mema CHADEMA, wanawashambulia viongozi hawa kwa kishindo.
“Kumbuka kauli na tambo za Wassira na Mwigulu kwamba CHADEMA itakufa.
Wanajua kuwa CHADEMA chini ya Mbowe na Slaa haiwezi kufa. Kwa hiyo, ili
ife inabidi wawili hawa waondoke, ishikiliwe na wengine ili CCM
wabahatishe tena.
“Si kwamba chama hakina watu wengine wenye uwezo, lakini ukweli ni
kwamba uongozi wa Mbowe na Slaa umeijenga CHADEMA ikawa tishio ambalo
CCM wasingependa kuliona likisitawi hadi uchaguzi mkuu ujao.”
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba wakati Mbowe anapewa dhamana ya
kuongoza chama hiki mwaka 2004, CHADEMA ilikuwa na wabunge wanne tu wa
kuchaguliwa na mmoja wa viti maalumu. Madiwani hawakuzidi 100.
Mwaka 2005 kilipata wabunge 11, na mwaka 2010
kilipata wabunge 49, na mamia ya madiwani. Kinaongoza mamia ya mitaa,
vitongoji na vijiji. Kinazidi kuaminiwa na kupata maelfu ya wanachama.
Hamasa na umaarufu wa CHADEMA vimeongezeka nchi nzima.
Wasomi na wafanyabiashara wamezidi kujiunga na CHADEMA, ujasiri wa
wananchi umeongezeka, na chama tawala kimeyumba katika maeneo mengi.
Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba Mbowe na Slaa
hawahongeki. Kwa hiyo, CCM imedhamiria kuwachonganisha na wanachama, na
kuhakikisha wanaondolewa kwenye uongozi kwa mbinu zozote zile.
Mbinu ya sasa inayotumiwa ni kutumia makundi ya waasi ndani ya
CHADEMA, na waliokwishapoteza uanachama kudai kwamba Mbowe hastahili
kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kabla
ya mwisho wa mwaka huu.
Wiki hii baadhi ya vyombo vya habari vilimnukuu ofisa mwandamizi
kutoka Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa akisema maneno hayo hayo,
ingawa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, John Mnyika
alitoa kauli haraka haraka kupinga kauli hiyo, akisema mtoa kauli
amekurupuka, na hizo ni dalili za ofisi hiyo kutumika vibaya.
Wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema uongozi wa CHADEMA
uliondoa kipengele cha ukomo wa muda wa uongozi bila kufuata utaratibu
wa kikatiba, gazeti hili limegundua jambo tofauti.
Mawasiliano ya kimaandishi kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama, Jaji
Francis Mutungi na CHADEMA, yanaonyesha kuwa mambo yote yalifuata
utaratibu.
Kwa mujibu wa barua ya Januari 15, 2014 (Kum.Na.DA.112/123/16A/19),
Msajili alidai kuwa Ibara ya 6.3.2c ya Katiba ya CHADEMA ilichomekwa
kinyemela bila kupitishwa na mkutano mkuu wa chama.
Lakini barua ya CHADEMA kwenda kwa makatibu wa wilaya na mikoa nchi
nzima, Julai 13, 2006 (Kumb. C/HQ/ADM/CIR/15/139), inaeleza wazi maeneo
yaliyokuwa kwenye mchakato wa kufanyiwa maboresho.
Aya ya mwisho inasomeka hivi: “Pia pendekezo la Ibara ya 6:3.2 (c) ya
rasimu inasomeka: ‘Kiongozi aliyemaliza muda wake wa uongozi ana haki
ya kugombea na kuchaguliwa tena, ilimradi awe ametimiza masharti ya
kuchaguliwa kuwa kiongozi.’ Badala ya Ibara ya 6:3.2 (c) iliyokuwa
inaweka kikomo cha muda wa awamu mbili kwa viongozi kuwa madarakani
katika cheo kimoja kwa ngazi moja ambacho kimeondolewa.”
Barua hiyo ilisainiwa na Shaibu Akwilombe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, ambaye sasa ni katibu wa CCM .
Mkoa wa Mtwara.
Mwezi mmoja baadaye, Agosti 13, 2006, Mkutano Mkuu wa CHADEMA
ulipitisha maboresho hayo na mengine yaliyokuwa yamependekezwa na
kupitiwa na wajumbe.
Mkanganyiko Ofisi ya Msajili
Juzi CHADEMA ilisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilikurupuka
kutoa tamko kuhusu ukomo wa viongozi wao pasipo kuzingatia kwa ukamilifu
maelezo na vielelezo vilivyopelekwa kwenye ofisi yake baada ya
mabadiliko ya katiba ya mwaka 2006.
Tanzania Daima imeona barua nyingine, Kumb. DA/112/123/01/125,
iliyosainiwa na Msajili Msaidizi Sisty Nyahoza. Inasema, “Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa inatoa ufafanuzi kuwa vipindi vya uongozi
katika vyama vya siasa huwekwa na katiba za chama husika.
“Msajili wa Vyama vya Siasa anaviasa vyama vya siasa kuzingatia
katiba zao na si kumwomba msajili kusogeza mbele chaguzi zenu za ndani,
kwani sheria haimpi msajili mamlaka hayo.
Kwa mujibu wa barua hiyo, msajili amesema kuwa anaelewa changamoto zinazovikabili vyama vya siasa.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment