Taarifa za uhakika kutoka katika kikao hicho zinaeleza kuwa baadhi ya
maneno makali waliorushiana viongozi hao ni pamoja na ‘andazi’…,
‘kiazi’…, ‘mpuuzi umehongwa’.
Kwa mujibu wa habari hizo, hali hiyo ilimfanya Mwenyekiti Diallo
amtimue katibu wake katika kikao hicho kilichafanyika katika ofisi ya
Mwenyekiti huyo.
Inaelezwa kuwa kikao hicho cha Juni 27 mwaka huu, kilivunjika muda
mfupi baada ya kuanza ajenda ya yatokanayo na kikao kilichopita.
Katika yatokanyo, ilidaiwa kuwa vikao vya CCM vya Wilaya ya Misungwi
vimekuwa vikiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa
Wilaya hiyo, Dalali Shibiliti, badala ya mwenyekiti wa wilaya.
Wakati wa kulijadili suala hilo, Katibu wa Mkoa, Joyce Masunga,
alitoa ufafanuzi akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha katiba ya
CCM.
Masunga alieleza kuwa anayepaswa kuendesha vikao hivyo ni Mwenyekiti
na siyo mjumbe wa NEC wa wilaya hali iliyosababisha mjumbe, Bernard
Polycarp, kunyoosha mkono na kumshambulia katibu huyo.
Polycarp alidai kuwa Masunga anampigia debe Mbunge wa Jimbo la
Misungwi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati),
Charles Kitwanga, ili apite bila kupingwa katika uchaguzi mkuu ujao.
“Masunga alimjibu kwamba alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani
humo, viongozi mbalimbali wa Chama walieleza mafanikio ya utekelezaji wa
Ilani na kumtaja mbunge huyo kwa kuyafanikisha.
“Kwa sababu hiyo Masunga aliwahoji iwapo viongozi karibu wote
wamemfagilia atakuwa anachukiwa kwa lipi na kwamba ingekwa ni
Kilimanjaro viongozi wangesema apite bila kupingwa,” kilieleza chanzo
chetu kikimnukuu Masunga.
Ilielezwa kuwa baada ya maelezo hayoya Masunga, Diallo aliingilia
kati na kumtaka atulie na kumkumbusha kwamba hatakiwi na anapaswa
kuondoka Mwanza.
Taarifa zinasema matamshi hayo ya Diallo yalizua vurugu ambako yeye
(Diallo) walirushiana maneno makali hadi Mwenyekiti akamwamuru Masunga
kutoka nje ya kikao.
“Mwenyekiti alicharuka na kumtolea maneno makali Katibu… naye
alimjibu kuwa yeye siyo andazi la kutoka tu vinginevyo yeye ni kiazi…
lakini ukweli ndiyo huo MNEC hawezi kuongoza vikao vya wilaya,”
kilieleza chanzo chetu.
Ilielezwa kuwa hali hiyo iliwaacha baadhi ya wajumbe wakiduwaa huku
wengine wakisisitiza katibu atoke naye ikabidi atoke nje ya kikao
akifuatiwa na makatibu wake wasaidizi; Sukwa na Zubeda Mbaruku na kikao
kuvunjika.
Chanzo cha mgogoro
Kuibuka kwa mgogoro huu kunadaiwa kunatokana na makovu ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010 ambako Diallo akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa
(NEC) Mkoa wa Mwanza alidaiwa aliendesha kampeni za kumkwamisha Charles
Kitwanga kushinda ubunge Misungwi ili mshindi awe Jacoub Shibiliti (sasa
MNEC wa Misungwi) ambaye Diallo alikuwa akimuunga mkono.
Sababu nyingine inayotajwa kuwa chanzo cha mgogoro huo ni hatua ya
Mbunge Kitwanga kufuatilia na kusimamia kwa ukamilifu mapato ya
Halmashauri ya Misungwi yaliyokuwa yakifujwa na baadhi ya viongozi na
watendaji.
Hatua hiyo ilisababisha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Polycarp
ambaye inaelezwa ni rafiki wa Diallo, kusimamishwa uenyekiti na CCM.
Wakati huo Marehemu Clement Mabina ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa
Mwanza na Katibu akiwa Masunga.
Polycarp alisimamishwa uenyekiti kutokana na ripoti ya Mkaguzi na
Mdibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo iliibua ubadhirifu wa zaidi
ya Sh bilioni 2 zilizodaiwa kutafunwa na baadhi ya watendaji. Ripoti
hiyo pia ilieleza kuwa Polycarp alikuwa akifanya biashara na halmashauri
yake.
Kauli ya Joyce Masunga
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu kuhusu kuvurugika kwa kikao hicho,
Masunga alikuja juu akisema aliyevujisha taarifa hizo hafai kwa kuwa
kikao hicho kilikuwa ni kikao cha ndani.
“Aliyekueleza taarifa hizo hafai, mwambie afuate ya kwake… kikao
hicho kilikuwa cha ndani na cha siri hakuna mhudumu au mtu yeyote
asiyehusika aliyehudhuria… anakuambia wewe mwandishi wa habari ili
iweje,” alihoji Masunga na kueleleza kuwa masuala yote ya kikao hicho
anapaswa kuulizwa Mwenyekiti wake.
Mwenyekiti Diallo
Diallo naye alipotafutwa alisema hawezi kuzungumzia mambo yaliyotokea
katika kikao hicho kwa kuwa vikao vya kamati ya siasa ni vikao vya
siri.
Kuhusu makundi yaliyopo ndani ya Chama hicho, alisema yeye anasimamia
kitu kiitwacho CCM na kamwe katika uongozi wake hawezi kuongoza chama
hicho kwa kufuata makundi.
“Ninawatumikia wana CCM wote walionichagua kuwaongoza katika kipindi
cha miaka mitano. Kama kuna watu wana makundi mie siwezi kuyumbishwa,
ninasimamia Katiba ya CCM na si vinginevyo,” alisema Diallo.
Mtanzania
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mtanzania
0 comments:
Post a Comment