Bunge nchini Afrika Kusini, leo linatarajiwa kuwa na kikao maalum cha kumkumbuka Nelson Mandela, huku viongozi duniani wakijiandaa kwa misa ya wafu itakayofanyika Jumanne.

Kikao cha leo kinafanyika mwonzoni wa wiki ya shughuli mbali mbali za kumuenzi Mandela kabla ya mazishi yake tarehe 15 Disemba.

Zaidi ya viongozi miamoja wa sasa na wa zamani wanatarajiwa kuhudhuria misa hiyo au mazishi mwishoni mwa wiki hii.

Mnamo siku ya Jumapili, mamilioni ya wanachi walijitokeza kuhudhuria maombi maalum ya kumkumbuka Mandela aliyekuwa rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo.

Kikao cha leo cha Bunge kitakuwa kikao maalum kwa ajili tu ya kumkumbuka Hayati Mandela.

Mke wa zamani wa Mandela, Winnie Madikizela-Mandela na mjukuu wake Mandela Mandla, wote ni wabunge katika bunge la taifa, lakini haijulikani ikiwa watahudhuria kikao cha leo.

Msemaji wa chama tawala, ANC, Moloto Mothapo amesema, anatumaini kuwa baadhi ya jamaa za familia ya Mandela, watakuwepo bungeni.

Rais wa zamani wa nchi hiyo, FW de Klerk, amealikwa kwenye kikao hicho.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top