OFISI ya Rais  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Idara yake ya Uratibu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeeleza majukumu yake katika kutoa huduma kwa jamii huku ikieleza juhudi inazozichukua katika kukabiliana na uzururaji wa wanyama katika maeneo ya miji.
 
Maelezo hayo yametolewa leo na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.
 
Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee alishiriki kikamilifu pamoja na uongozi na watendaji wa Ofisi hiyo ya Rais.
 
Uongozi huo chini ya Waziri wake, Dk. Mwinyihaji Makame ulieleza kuwa juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda na uzururaji wa wanyama katika maeneo ya miji hasa ngombe umeanza kupungua kwa kiasi kikubwa.
 
Katika maelezo yao uongozi huo ulieleza kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na kuishirikisha jamii kikamilifu katika zoezi hilo huku kukitolewa zawadi maalum na Idara husika kwa yeyote atakayemkamata ngombe akizurura kinyume na taratibu na sheria zilizopo.
 
Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa licha ya juhudi hizo pia, mashirikiano na vikosi, Manispaa pamoja na kuunda Kamati maalum nako kumesaidia kwa kiasi kikubwa katika kupambana na kadhia hiyo ndani ya miji.
 
Uongozi huo ulieleza kuwa juhudi kubwa zinachukuliwa katika kuhakikisha maeneo ya miji yanakuwa safi, aidha, katika baadhi ya maeneo operasheni maalum zilifanyika katika misingi ya maji machafu kwa kuwashirikisha wananchi, Masheha na Madiwani.
 
Katika kuongeza nguvu ya utekelezaji wa azma hii, taasisi za Idara hiyo zimehamasisha uundwaji wa vikundi mbali mbali vya kijamii vinavyosaidia nguvu za Serikali za Mitaa kuweka usafi katika maeneo ya mijini.
 
Aidha, matangazo mbali mbali yametolewa ya kuelimisha jamii juu ya elimu ya afya, usafi wa mazimgira, udhibiti wa mifugo pamoja na vipindi vya ‘usafi ni tabia’. Katika maelezo yao, uongozi huo ulieleza mikakati iliyoiweka katika kuliimarisha na kulirejesha hadi yake soko la mbogamboga lililopo Mombasa mjini Unguja.
 
Uongozi huo ulieleza hatua ambazo umekusudia katika kuliimarisha soko hilo kwa lengo la kupunguza ama kuondosha kabisa msongamano katika soko kuu la Mwanakwerekwe.
 
Kwa upande wa changamoto inazozikabili Idara hiyo, uongozi huo ulieleza juhudi inazozichukua katika kuhakikisha changamoto. Pia Idara hiyo ilieleza jinsi inavyoratibu  shughuli za maendeleo ya wananchi.
 
Kwa upande wa wizi wa mifugo, hasa katika eneo la Vitongoji Pemba, uongozi ulieelza kuwa mikakati ya ulinzi shirikishi kwa kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama, mafanikio yamepatikana kwani wizi wa mifugo umepungua sana.
 
Uongozi huo pia, ulieleza kuwa tayari utafiti  wa sababu zinazopelekea kuwepo kwa unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji katika baadhi ya maeneo hasa katika Mkoa wa Kaskazini ambapo kwa maelezo ya uongozi huo utafiti umekamilika na mapendekezo yake yameanza kufanyiwa kazi.
 
Pamoja na mambo mengineyo, uongozi huo ulipongeza juhudu za Rais, Dk. Shein katika kuimarisha sekta za maendeleo sanjari na kutekeleza ahadi alizoziahidi kwa wananchi.
 
Nae Dk. Shein kwa upande wake aliipongeza Idara hiyo ya kuratibu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa juhudi zake inazozichukua huku akisisitiza haja ya kukuza mashirikiano na kutoa huduma bora kwa wananchi Unguja na Pemba.
 
Aidha, Dk. Shein aliunga mkono hatua za kuliimarisha soko la Mombasa katika kuhakikisha linatoa huduma kwa wananchi kama ilivyokuwa makusudio yake huku akikisisitiza kuwa msongamano katika soko la Mwanakwerekwe hasa nyakati za asubuhi umekuwa ukileta usumbufu mkubwa kwa wananchi.
 
Hivyo alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondosha msongamano hasa wa magari pamoja na kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kupata eneo muwafaka la kuuza bidhaa zao kwa ufanisi zaidi.