Wachezaji wa Timu ya Azam
Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
AZAM FC ya Dar es Salaam, imefungwa mabao 2-0 na Shark FC ya hapa, katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi B, Kombe la Hisani, kwenye Uwanja wa Martyrs jioni hii.
Mabao ya washindi, timu inayomilikiwa na mdogo wake rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila yalifungwa na Ndibu Kalala dakika ya 23 na Kalala Kabongo dakika ya 34.
Hata hivyo, kipigo hicho kimechangiwa kwa kiasi kikubwa na uchezeshaji mbovu wa marefa, ambao tangu mwanzo walionekana kuwapendelea wenyeji.
Azam leo imenyimwa penalti mbili za halali, moja kila kipindi, ya kwanza baada ya shuti la mshambuliaji Gaudence Mwaikimba kuzuiwa kwa mkono na beki wa Shark na ya pili kiungo Humphrey Mieno aliangushwa kwenye eneo la hatari, tena ndani ya sita akiwa amekwishamtoka kipa, lakini zote refa akapeta.
Washika vibendera nao walizima mashambulizi kadhaa ya Azam kwa kudai wachezaji walikuwa wameotea.
Mabao yote Azam walifungwa wakitoka kushambulia na hayakuwa na mushkeli, makosa ambayo walirekebisha na hawakuyarudia kipindi cha pili. Kipindi cha kwanza, timu zilishambuliana kwa zamu, lakini kipindi cha pili Azam walitawala zaidi mchezo na kama si ‘madudu’ ya refa, matokeo yangeweza kubadilika.
Kwa matokeo haya, Shark inaongoza Kundi B kwa pointi zake tatu, ikifuatiwa na Dragons iliyotoka 1-1 na Azam katika mchezo wa kwanza.
Azam sasa itaomba Shark iifunge zaidi ya mabao 2-0 Dragons katika mechi ya mwisho ya kundi hilo Desemba 23, ili ifuzu kuingia Nusu Fainali.
Azam imecheza mechi zote mbili bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na Msaidizi wake, Kali Ongala ambao walibaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche raia wa Ivory Coast, kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
Nusu Fainali zitachezwa Desemba 25 wakati Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu.  Kundi B, lina timu za DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa. 
Kocha wa makipa, Iddi Abubakar aliyeiongoza timu hiyo katika mechi hizo mbili alilalamikia uchezeshaji wa marefa, ambao walisindikizwa na Polisi kutoka uwanjani baada ya mechi, kutokana na kuwakera hata mashabiki wa timu za hapa waliotaka kuwafanyia fujo.
Kikosi cha Azam leo kilikuwa; Mwadini Ally, Malika Ndeule/Uhuru Suleiman dk 85, Samih Hajji Nuhu, Luckson Kakolaki/Omar Mtaki dk 65, David Mwantika, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo/Himid Mao dk80, Humphrey Mieno, Seif Abdallah, Gaudence Mwaikimba na Waziri Salum/Abdi Kassim ‘Babbi’ dk 65.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top