STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20.2.2013
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
leo ameongoza maelfu ya wananchi katika mazishi ya Padri Evarist Mushi
huko Kitope, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika
mazishi hayo, viongozi mbali mbali wa dini na serikali walihudhuria
akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Mawaziri wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Wawakilishi, Wabunge, viongozi wa vyama vya siasa kutoka
Zanzibar na Tanzania Bara na wananchi kutoka maeneo mbali mbali.
Mapema asubuhi, Dk. Shein alitoa salamu za mwisho kwa Padri Evarist Mushi huko katika kanisa la Minaramiwili, mjini Zanzibar.
Katika
Kanisa la Minaramiwili sala ya mazishi iliongozwa na Askofu Mkuu wa
Jimbo Katoliki la Dar-es-Salaam Muadhama Kadinali Policap Pengo na ibada
ya mazishi huko Kitope iliongozwa na Mhashamu Baba Askofu Antoni Banzi
ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga.
Akitoa
salamu za Serikali katika mazishi hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais Mhe. Mohammed Aboud alisema kuwa Serikali imesikitishwa
sana na kifo cha kiongozi huyo wa dini na kwamba ni msiba mkubwa kwa Taifa.
Waziri
Aboud aliwaomba wanafamilia wa marehemu pamoja na waumini wa dini ya
Kikiristo kuwa watulivu na wastahamilivu katika kipindi hichi kigumu cha
maombolezo ya kiongozi huyo.
Alimuelezea
Padri Mushi kuwa alikuwa kiongozi aliyehubiri upendo, umoja na amani
miongoni mwa waumini na wananchi wote wa Zanzibar na kuhimiza maadili
mema, hivyo kumuenzi kwa kumuombea maisha mema ya milele.
Nazo salamu za familia zilitolewa na Fransis Mushi na kutoa shukurani kwa niaba ya familia kwa
mashirikiano makubwa waliyoyapata katika msiba huo tokea siku ya tukio
la mauaji ya Padri huyo hadi leo alipofikishwa kwenye nyumba yake ya
milele.
Nae
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Zanzibar Agostino Shao alieleza
kusikitishwa na msiba huo na kumuomea marehemu amani ya milele.
Padri Mushi alizaliwa Juni 15, 1957 katika kijiji cha Uru Kimanganuni, katika Mkoa wa Kilimanjaro
na baada ya kumaliza elimu ya juu ya Sekondari mwaka 1976, alijiunga na
Seminari Kuu Kibosho ambako alipata elimu ya Falsafa kati ya mwaka 1978
na 1979.
Mwaka
1980 alijiunga na Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Kipalapala Mkoani
Tabora alipopata elimu ya tauhidi (Theology) hadi mwaka 1982.
Mwaka
1984 alirudi Kipalapala Mkoani Tabora kuendelea na masomo na mwaka huo
huo alipata Daraja la Ushemasi katika Parokia ya Bikira Maria wa Rosari
Kitope Zanzibar.
Katika
maisha yake ya Upadri alishika vyeo mbali mbali ikiwemo Paroko wa
Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Kitope mwaka 1985, Paroko wa Parokia
ya Moyo safi wa Maria wa Wete Pemba na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu
Antoni wa Padua Machui.
Padre Mushi aliuwawa kwa kupigwa risasi Februari 17 huko Mtoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar na watu wasiojulikana.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment