Nelson Rolihlahla Mandela ‘Mzee Madiba’ enzi za uhai wake.
SHUJAA na mwamba wa Afrika, Nelson Rolihlahla Mandela ‘Mzee Madiba’ amefariki dunia Desemba 5, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 95 kwa maradhi ya mapafu.

Hakuna ngozi nyeusi na hata nyeupe anayeweza kubisha kuwa rais huyo mstaafu wa Afrika Kusini na mtetezi wa watu weusi amepitia mambo mengi. Tukiacha kukua kwake, ujana na mengine, tujikumbushe mwisho wake wa enzi;

 
Mwaka 1966 gerezani Mandela anaonekana akiitia viraka nguo yake ya jela.
Februari 11, 1990
Baada ya miaka 27 jela, hatimaye Mzee Madiba aliachiwa na serikali ya makaburu wa Afrika ya Kusini iliyokuwa ikiongozwa na Rais Fredrick Willem de Klerk.

Julai 5, 1991
Chama cha African National Congress (ANC) kilimchagua kuwa Rais wa Afrika Kusini. Mandela alipewa nafasi hiyo akichukua nafasi ya swahiba wake wa kisiasa, Oliver Tambo aliyefariki dunia.
 
Mandela na mtoto wake wa kwanza wa kiume Themi.
 
Aprili, 1992
Alitangaza kuachana na aliyekuwa mkewe, Nomzamo Winnie Madkizela Mandela baada ya uhusiano wao wa zaidi ya miaka 30 uliotawaliwa na misukosuko mingi.

Mandela alimuacha Winnie kutokana na mwanamama huyo kudaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na vijana wadogo ndani ya ANC.

Oktoba 15, 1993
Alijitwalia Tuzo ya Nobel kwa pamoja na De Klerk kutokana na mchango mkubwa katika kuleta upatanishi na maelewano Afrika Kusini.
 
Ndoa ya Madiba na Winnie.

Mei 10, 1994
Alichaguliwa kwa kura nyingi kuwa Rais wa Kwanza Mweusi katika Uchaguzi wa Kwanza wa Kidemokrasia Afrika Kusini. Urais wake ulimaanisha kumalizika rasmi kwa zama za ubaguzi wa rangi nchini humo.

Julai 18, 1998
Akiwa ziarani nchini Canada, ofisi yake ilitangaza kuwa anamuoa Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Msumbiji, Samora Machel.

Ndoa hiyo inaelezwa kumaliza upweke aliokuwa nao Mandela kutokana na uamuzi wake wa kumuacha Winnie.
 
Mandela akiwa amevaa mavazi ya kabila lake la Xhosa; alitoka katika familia ya kichifu.

Mwaka 1999
Baada ya miaka mitano ya urais, Mandela alitangaza kutowania nafasi hiyo katika uchaguzi uliofuata na badala yake akamuachia makamu wake, Thabo Mvyelwa Mbeki.

Mandela aliachia ngazi wakati bado akipendwa na wananchi wake. Hatua yake ya kuachia ngazi ilikwenda kinyume na viongozi wengi wa Afrika ambao hupendelea kung’ang’ania madaraka.

Mwaka 2000
Mandela alichaguliwa kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi akichukua nafasi ya Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia mwaka 1999.
 
Mandela akisalimiana na Mama Maria Nyerere alipotembelea Tanzania mwaka 1990. Katikati ni Mwalimu Julius Nyerere

Mwaka 2001
Mandela alibainika kuwa na ugonjwa wa kansa ya tezi ya kiume ya uzazi (prostate cancer).

Taifa la Afrika Kusini lilipatwa na mshtuko mkubwa kutokana na habari hizo kumhusu kiongozi wao.

Mwaka 2003
Kutokana na hatua ya Marekani na washirika wake kuivamia Iraq kwenye vita ya pili ya Ghuba ikidai ina silaha za maangamizi, Mandela alizungumza hadharani na kukemea sera za nje za taifa hilo kubwa duniani.

Mwaka 2004
Mandela alitangaza kurejea kijijini kwake Qunu na kusema hatakuwa akionekana mara kwa mara.
 
Aprili 19, 2009
Mandela alitoa hotuba ya mwisho ya kisiasa baada ya kuongea kupitia hotuba iliyorekodiwa kwenye mkutano wa hadhara wa ANC wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Afrika Kusini.

Januari 26, 2011
Alilazwa hospitali kutokana na kile kilichoelezwa kuwa na matatizo katika mfumo wake wa kupumua.

Februari 25, 2012
Alilazwa hospitali kutokana na kusumbuliwa na maumivu makali ya tumbo.

Desemba 8, 2012
Alikimbizwa hospitalini na kulazwa kwa takribani mwezi mmoja baada ya kukutwa na mawe kwenye kongosho lake.
 
Machi 28, 2013
Mandela alilazwa tena hospitali kutokana na kusumbuliwa na vichomi.

Juni 8, 2013
Alilazwa hospitali kutokana na matatizo katika mapafu.

Desemba 5, 2013
Mzee Madiba alifariki dunia nyumbani kwake Johannesburg, Afrika Kusini.
GPL 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top