Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
Viongozi wa Serikali wakiwamo mawaziri, wameingia kwenye kashfa
inayowaweka katika wakati mgumu, baada ya kubadili matumizi ya nyumba za
Serikali walizonunua, kinyume na mikataba inavyoeleza.
Nyumba hizo ambazo zilianza kuuzwa mwaka 2002 enzi
ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ziliuzwa kwa
mawaziri, makatibu wakuu na watumishi wengine wa ngazi mbalimbali za
umma.
Mikataba ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za
Serikali inaeleza kuwa, mfanyakazi wa Serikali anaponunua au kukopeshwa
nyumba, hatakiwi kubadili matumizi au kuuza hadi baada ya miaka 25
kupita.
Kwa mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na 9 na
10, mtumishi aliyeuziwa nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba
hiyo mpaka hapo itakapotimia miaka ishirini na mitano (25), kuanzia
tarehe ya hatimiliki.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Ujenzi, John
Magufuli mwenye dhamana na nyumba za Serikali kwa muda wa miezi miwili
kutoa ufafanuzi wa suala hilo bila mafanikio, huku akitoa sababu
mbalimbali kwa mwandishi kukwepa kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson
Lwenge alisema kuwa anahitaji kupata ripoti kamili kutoka kwa Wakala wa
Nyumba za Serikali (TBA), ili ajionee mikataba na afahamu ni wapi
ilipovunjwa.
“Serikali ina nia nzuri kabisa kuwauzia watumishi
wake nyumba, lakini kama kuna mikataba inakiukwa, basi TBA inafahamu kwa
kina ni kwa vipi watu hao wachukuliwe hatua,” alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, viongozi
wengi ambao nyumba zao zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na
Mwanza wamezibadili matumizi na kuwa za biashara.
Kwa Jiji la Dar es Salaam baadhi ya nyumba
zilizouzwa kwa vigogo hao wa Serikali na kubadilishwa matumizi zipo
katika maeneo ya Oysterbay.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya nyumba hizo
zikiwa zimebadilishwa matumizi na kuwa klabu za starehe, kupangishwa
taasisi au balozi, huku nyingine zikiwa tayari zimeuzwa.
Moja ya nyumba hizo ni ya aliyewahi kuwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano, Mohamed Seif Khatib,
iliyopo Oysterbay, Mtaa wa Bongoyo katika Barabara ya Hillpark. Nyumba
hiyo kwa sasa imevunjwa na kujengwa klabu na baa iitwayo Ocasa.
Alipoulizwa kuhusu nyumba hiyo na mkataba wake
unavyosema, Khatib alisema kwamba hajavunja sheria yoyote kwa sababu
hajauza nyumba hiyo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Alifafanua kuwa yeye amebadili matumizi sehemu ndogo ya nyumba
hiyo huku akimtaka mwandishi aandike tu kuhusu sehemu kubwa na siyo
mabadiliko aliyodai ni madogo.
“Nyie waandishi ndivyo mlivyo, kwa nini msiandike
mazuri yetu. Mnapenda kuandika mambo mabaya tu, mnataka tuishi
kimaskini. Nyumba imejengwa tangu enzi za ukoloni, mnataka mpaka leo
ibaki hivyohivyo?” alihoji.
Eneo la Kinondoni, palipokuwa na nyumba ya
aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya katika Serikali ya Rais Kikwete,
nayo kwa sasa imevunjwa na kujengwa ghorofa, huku kibao cha mkandarasi
kikionyesha kuwa ujenzi wa jengo la biashara unaendelea.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha
kuwa nyumba nyingine za viongozi wa Serikali zilizobadilishwa matumizi
zipo eneo la Msasani na Masaki.
Nyumba nyingine iliyobadilishwa matumizi
inamilikiwa na waziri mmoja eneo la Barabara ya Hindu, Kinondoni mkabala
na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ambayo imebadilishwa na kujengwa
nyumba za kupangisha watu.
Mjini Arusha baadhi ya nyumba za Serikali zilizouzwa na kubadilishwa matumizi zipo eneo la Uzunguni.
Moja ya nyumba hizo ipo karibu na Ikulu ndogo
mjini humo, ambayo hivi sasa imebadilishwa na kuwa baa. Nyumba hiyo ipo
Mtaa wa Haile Selassie.
Katika Jiji la Mwanza, nyumba zilizobadilishwa matumizi zipo katika eneo la Isamilo na Kapiripointi.
Historia ya nyumba za Serikali
Nyumba za watumishi wa Serikali zilianza kujengwa
na watawala wa Kijerumani na Waingereza. Nyumba hizo ambazo sasa idadi
yake inakadiriwa kufikia 10,000 ni za daraja la tatu, pili na la kwanza,
kulingana na nyadhifa za watumishi wa Serikali.
Sababu za kuuza nyumba hizo hazikuwekwa bayana,
lakini maelezo mengine yanaonyesha kuwa hatua hiyo imefikiwa ili
kuwasaidia watumishi wa Serikali kuwa na nyumba. Hata hivyo, maelezo
mengine yanaonyesha kwamba nyumba hizo ziliuzwa kwa kuwa ni mzigo kwa
Serikali.
Hadi kufikia mwaka 2012, nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watumishi wa umma ni 6,000.
Wakala wa Majengo
Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),
Elius Mwakalinga alisema kuwa kuna masharti ya nyumba za Serikali ambayo
miongoni mwake ni kutobadili matumizi na kutohamisha mali hiyo hadi
baada ya miaka 25.
Mwakalinga alisema pia kwamba mfanyakazi wa umma
hatatakiwa kuhamisha mali hiyo wala hatimiliki kwa mtu wa tatu na iwapo
atahitaji kufanya ukarabati, basi atatakiwa kuomba kibali.
“Kama kweli kuna watu wanaofanya ujanja katika
hilo, hata kama ni viongozi, watashughulikiwa kulingana na sheria,”
alisema Mwakalinga.
Waziri Lwenge
Akizungumzia zaidi suala hilo, Naibu Waziri Lwenge
alihoji maswali kadhaa, ikiwamo sababu za watumishi kubadili nyumba
hizo na kuzifanya klabu au maeneo ya biashara na wakapewa ruhusa na
mamlaka ya mipango miji. Hata hivyo, alisisitiza kuwa hajaifahamu kwa
kina mikataba hiyo inasema nini.
Lwenge alisema kwamba wizara yake itaketi na
wanasheria wake na kuangalia upya mikataba hiyo, ili iwapo kuna
vipengele vyenye upungufu virekebishwe.
“Inawezekana kuna vitu vinakosekana kwenye
mikataba hiyo, au havijafafanuliwa na ndiyo maana watumishi wa Serikali
wanavitumia vibaya kuvunja masharti ya mikataba yenyewe,” alisema.
Lwenge pia alisema kwamba kuna mambo mengi kwenye mikataba hiyo anayodhani yanatatiza na kuhitaji kutupiwa jicho.
Alitaja mfano wa mtumishi aliyestaafu na kuiachia nyumba hiyo familia yake, ambayo haifahamu masharti ya mikataba.
“Nia yetu ni kusaidia wafanyakazi. Ni hilo tu,
hatuna jingine, lakini kama kuna upungufu kama huo ni lazima uangaliwe.
Ila nashukuru kwa kuwa waandishi mnafanya kazi ya kubaini vitu kama
hivi,” alisema.
Manispaa Kinondoni
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Kaiohela alisema
kuwa TBA wana kazi yao na nyumba zao na wanaifahamu mikataba ya wateja
wao.
“Sina uhakika kama TBA ina nyumba maeneo ya
Oysterbay, ila kwa upande wa nyumba za Serikali zinazosimamiwa na
manispaa, tuna orodha ya mikataba na waliobadili matumizi,” alisema.
Ushawishi kutoka kwa wawekezaji
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa baadhi ya
viongozi na watumishi wengine wa Serikali wamepangisha nyumba hizo kwa
kampuni binafsi, baadhi kujenga maduka ya biashara na ofisi nje ya uzio
wa nyumba hizo.
Ilibainika kuwa, viongozi wengi wanaomiliki nyumba
hizo huingiwa tamaa ya kuziuza au kubadili matumizi kwa sababu ya
ushawishi wa wawekezaji wa nje, ambao huahidi kuwalipa kiasi kikubwa cha
fedha na kuzirudisha nyumba hizo baada ya miaka 20.
Septemba mwaka jana, nyumba ya Serikali iliyoko
eneo la Mafiati, mjini Mbeya, yenye namba 162, Block ilipigwa mnada na
Kampuni ya Udalali ya J.A Kandonga.
Nyumba hiyo inadaiwa kuuzwa kwa mfanyabiashara wa
jijini Dar es Salaam kwa Sh250 milioni kutoka kwa mfanyakazi wa
Serikali, Simboleo Gibson.
Mohamed Seif Khatib
Akizungumzia zaidi kuhusu nyumba aliyoinunua
serikalini Khatibu ambaye pia ni Katibu wa NEC Oganaizesheni wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), alisema kwamba sehemu kubwa ya nyumba yake
ameibadilisha kuwa nyumba ya kuishi na kuwa ghorofa yenye vyumba kadhaa
ili iwe katika hadhi nzuri, huku pia akikiri mabadiliko katika eneo
ilipo baa ya Osaka.
“Sehemu kubwa nimebadilisha kuwa makazi ya kuishi
vilevile sasa kwa nini nyinyi mnataka kukuza hili jambo katika sehemu
ndogo tu? Haya andika utakavyo, andika nimebadili matumizi kama
unavyotaka,” alifoka Khatib.
Rais Kikwete
Rais Jakaya Kikwete, aliwahi kusema kuwa Serikali
yake imefikia uamuzi wa kuzirejesha baadhi ya nyumba za Serikali
zilizouzwa kwa watumishi wa umma, baada ya kubaini kwamba zilijengwa
katika mazingira nyeti.
Kikwete aliyasema hayo Ikulu Dar es Salaam alipokuwa akijibu
maswali ya wahariri wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari aliokutana nao
chini ya kivuli cha utaratibu aliojipangia wa kuzungumza na wananchi
kila mwishoni mwa mwezi.
“Hatukusudii kuzichukua nyumba zote…kwa mfano kuna
OCD kauziwa nyumba ya OCD iliyo katika eneo la polisi, na yule OCD
aliyeuziwa kahamishwa kutoka Mtwara kwenda Mafia…au kastaafu na nyumba
kapangisha…Kwa kweli kuna maeneo ambayo lazima tufanye marekebisho,”
alisema Kikwete.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment