Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umeshauri Kamati
ya Maadili ya CCM kuwaonyesha mlango wa kutokea wote walioanza kampeni
za kugombea urais, ubunge na nyingine kinyume cha maadili ya chama.
Umesema wagombea hao ambao umewaita wasio rasmi,
wameonywa mara kadhaa na viongozi wa chama ikiwamo kupitia kwenye vyombo
vya habari, lakini wameshindwa kujitambua na kujirekebisha.
UVCCM umedai wagombea hao wasio rasmi katika
kampeni zao tayari wameanza kusababisha kutoweka kwa mshikamano ndani ya
chama, kwani wamekuwa wakipita nchi nzima kushawishi kwa fedha na
rushwa nyingine mbalimbali makundi ya jamii ili kuungwa mkono.
Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Taifa,
Paul Makonda alisema Kamati ya Maadili ya CCM ina wajibu wa kutafsiri
hasira ya wanaCCM dhidi ya kampeni hizo ambazo zinakijeli chama, uongozi
wa nchi uliopo na kuleta nyufa.
“Tunachokiona sasa ni tofauti kabisa na malezi na
makuzi yetu ndani ya chama, kwani tayari baadhi ya wanaCCM bila uoga
wala aibu wameshajitangaza ni wagombea urais, ubunge, udiwani na nafasi
nyingine za kupigiwa kura, wameanza kampeni za kishindo za rushwa na
vishawishi mbalimbali nje kabisa ya utaratibu, kanuni na maadili ya
chama,” alisema Makonda na kuongeza:
“Watu hawa waonyeshwe mlango wa kutokea, tusipoziba ufa huu sasa tujiandae kujenga ukuta mwakani kwa gharama kubwa kupindukia.”
Makonda alisema kwa sababu mwaka huu kuna mchakato
wa chaguzi mbalimbali zitakazohitimishwa mwakani na ushaguzi mkuu,
mshikimamo wa hali ya juu unahitajika ndani ya chama.
“Kwa sasa ilani ya CCM ya mwaka 2010 imewekwa
pembeni, kinachonadiwa ni ilani binafsi za kumwaga fedha nchi nzima,
kusambaza elimu kama njugu, bila kueleza vyanzo vya mapato ya Serikali
zao za kusadikika,” alisema. Alisema hatua hiyo ni ukiukwaji mkubwa wa
sheria za chini, maadili, miiko ya chama.
pamoja na Serikali kwa ujumla ambapo ipo wima
katika kuhakikisha kuwa ilani ya CCM ya mwaka 2010 inatekelezwa kwa
ufanisi mkubwa.
Alisema CCM inataratibu zake za kupata viongozi na
wote tunazijua, kufanya kinyume na taratibu hizi ni uasi, upungufu wa
busara, na ukosefu wa sifa ya uongozi.
“Hivyo vijana wa CCM tunamuunga mkono Mwenyekiti
wa CCM taifa Dk Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti, Philiph Mangula na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama Nape Nnauye waliokemea tabia hii
mpya hatarishi kwa chama chetu ya kuhaha kupata uongozi nje ya taratibu
na kutumia vishawishi vyenye sura ya rushwa vitakavyokitia doa chama,”
Makonda alisema kuwa maadili na kanuni za chama ni
kuwaunganisha wanaCCM wote kuwa kitu kimoja, hivyo dalili zozote nje ya
tunu hizo ni usaliti, uasi ambao hauna budi kupigwa vita kwa nguvu zote
kwa vijana.
“ Hapa hatutakiwi kumwangalia nyani usoni, gharama ya kuendelea kuvumilia kauli na vitendo hivi vipya na hatarishi katika historia ya chama chetu ni majuto kwa kuwa waswahili hunena bandu bandu humaliza gogo, na bandu bandu hii iliyoanza tusiivumilie, itatuweka pabaya wanaCCM, “ alisema Makonda.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“ Hapa hatutakiwi kumwangalia nyani usoni, gharama ya kuendelea kuvumilia kauli na vitendo hivi vipya na hatarishi katika historia ya chama chetu ni majuto kwa kuwa waswahili hunena bandu bandu humaliza gogo, na bandu bandu hii iliyoanza tusiivumilie, itatuweka pabaya wanaCCM, “ alisema Makonda.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment